Ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la kutetea
haki za binaadamu la Human Rights Watch, HRW imesema wanajeshi wa Uganda
waliokuwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati walihusika na vitendo vya
unyanyasaji wa kingono
Wasichana na wanawake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekumbwa na
visa hivyo. Ripoti hiyo imesema, kiasi ya wanawake 13 na wasichana
walikabiliwa na vitendo hivyo tangu mwaka 2015.Ripoti hiyo inasema wasichana na wanawake walikumbwa na angalau kisa kimoja cha kubakwa na kuwatisha wengine kwa kuwataka kutosema lolote. Jeshi la Uganda lilipeleka askari wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2009 kama sehemu ya kikosi kazi cha kikanda cha Umoja wa Afrika cha kulisaka kundi la wapiganaji nchini Uganda la Lord's Resistance Army, LRA, lakini hivi karibuni ikatangaza kuondoa vikosi vyake.
HRW liliwafanyia mahojiano wanawake 13 na wasichana 3 mwanzoni mwa mwaka 2017, ambao walieleza kunyanyaswa kingono tangu mwaka 2010 na wanajeshi wa Uganda katika mji wa Obo uliopo Kusinimashariki ambako vikosi vya Uganda viliweka makao yake.
Mtafiti wa masuala ya Afrika wa shirika la HRW Lewis Mudge amesema Uganda haitakiwi kupuuzia madai ya wanawake hao ya unyanyasaji wa kingono na kubakwa yaliyotolewa dhidi ya wanajeshi wake. Amesema jeshi la Uganda na Umoja wa Mataifa wanatakiwa kuendesha uchunguzi wa kina, kuwaadhibu wanaohusika na kuhakikisha kwamba wanawake na wasichana waliobughudhiwa wanapata huduma wanazohitaji.
Wanawake 15 miongoni mwa wanawake na wasichana waliohojiwa wamesema walipata ujauzito, lakini hata hivyo wahusika wa ujauzito walirudi nchini Uganda na hawajatoa huduma yoyote ya malezi.
Mnamo mwaka 2016, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kamishna wa haki za binaadamu iliripoti visa 14 vya ubakaji vilivyofanywa na wanajeshi wa Uganda katika nchi hiyo, ambavyo ni pamoja na vile vilivyohusisha wahanga ambao walikuwa tayari na watoto wakati huo. Visa vinne kati yake vimo ndani ya ripoti ya HRW.
Wengine walifanyiwa unyanyasaji na kuondoka patupu.
Kulingana na ripoti za ndani za Umoja wa Mataifa za tangu mwaka 2016 zilizoonwa na HRW, wachunguzi wa Umoja huo kwenye eneo la Obo waliandikisha visa 18 vya unyanyasaji wa kingono na wa aina nyingine uliofanywa na wanajeshi wa Uganda dhidi ya wanawake na wasichana ambao hawakuweza kueleza wazi kutokana na kitisho cha adhabu kali kutoka kwa wanajeshi hao.
Ripoti hiyo pia inasema kwamba wachunguzi pia walipata taarifa za kiasi wa wanawake 44 na wasichana ambao walikuwa na watoto wa wanajeshi hao wa Uganda. Wanawake 15 pamoja na wasichana waliohojiwa walisema walikutana kimapenzi na wanajeshi hao ili kupata chakula ama fedha kutoka kwao kufuatia mzozo unaoendelea nchini mwao. Wengine walidai kutopata chochote hata baada ya kukutana na wanajeshi hao.
Aprili 19, mwaka huu wizara ya ulinzi ya Uganda ilitangaza kuliondoa jeshi lake kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na kusema mpango wake wa kuliondoa kundi la waasi la LRA umekwishafanikiwa. Vikosi vya Uganda vingeweza kuungana na walinda amani wa Umoja wa mataifa katika nchi hiyo, MINUSCA ili kuendelea na operesheni dhidi ya LRA, wizara hiyo iliongeza.
Shirika hilo la haki za binaadamu la HRW limetaka MINUSCA kutopokea wanajeshi toka Uganda, hadi baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma dhidi yao na watuhumiwa kutiwa mikononi mwa sheria.
Vikosi vya Umoja wa Afrika, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vimetuhumiwa kufanya matukio mengine mabaya zaidi ya kihalifu katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo Juni mwaka 2016, shirika la HRW lilitoa ripoti yake kuhusu mauaji ya kiasi ya watu 18, ambao ni pamoja na wanawake na watoto yaliyofanywa na wanajeshi walinda amani kutoka Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, MISCA. Hata hivyo AU haikueleza chochote kuhusu mauaji hayo.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment