CHEMBA ya Madini na Nishati (TCME)
imetambua na kuguswa na taarifa zisizo sahihi kwamba kampuni
zinazojihusisha na uchimbaji mkubwa wa madini zimekuwa zikifanya
shughuli zake hapa nchini bila ya kulipa kodi ya mapato. Chemba hii ni
muwakilishi wa makampuni wanachama waliorasimisha shughuli zao katika
sekta ya madini kuanzia kampuni ndogo za utafiti wa madini hadi
wachimbaji wakubwa na wa kati wa madini, pamoja na makampuni yanayotoa
huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti na uchimbaji wa madini.
Chemba na wanachama wake wanaunga
mkono uwepo wa sekta ya uchimbaji madini inayoratibiwa vema na inaweka
msisitizo mkubwa katika kuhakikisha shughuli za wanachama wake
zinaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na mamlaka za
Serikali hapa nchini.
Makampuni ya uchimbaji madini hapa
nchini yanaratibiwa kwa kiwango cha juu na mamlaka zilizo chini ya
Serikali ili kuhakikisha yanafanya shughuli zake kwa kufuata sheria na
kanuni za nchi. Makampuni haya yameendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa
uchumi wa nchi kwa njia mbali ikiwemo utengenezaji wa ajira pamoja na
ulipaji wa kodi.
Katika ripoti ya utendaji ya mwaka
2015 ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini. Tanzania (TMAA) ambao wanafanya
kazi chini ya Wizara ya Nishati na Madini, imeripotiwa kwamba makampuni
makubwa ya uchimbaji madini hapa nchini, kwa ujumla wake, kati ya mwaka
2009 na 2015 yameweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 870 (USD390
Milioni) kama mrabaha, na zaidi ya Shilingi Bilioni 680 (USD305 Milioni)
kama kodi ya mapato, hii ni mbali na kodi nyingine zisizo za moja kwa
moja ambazo pia zimelipwa.
Katika mwaka wa 2015 pekee, migodi
mitano mikubwa ya uchimbaji Dhahabu pamoja na mgodi mmoja wa kuchimba
Almasi, kwa pamoja iliweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 146 (USD65.5
Milioni) kama mrabaha na zaidi ya Shilingi Bilioni 380 (USD170 Milioni)
kama kodi nyingine ikiwamo kodi ya mapato. Viwango hivi ni dhahiri
vitakuwa vimeongezeka zaidi kwa mwaka 2016.
Zimekuwepo pia taarifa kwamba
makampuni haya ya uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa yakifaidika kwa
kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pasipo uhalali wa kupata
marejesho hayo. Taarifa hizi si sahihi. Ukweli ni kwamba makampuni ya
uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa na yataendelea kusafirisha nje ya
nchi kwa ajili ya kuuza madini yote ambayo wanayazalisha hapa nchini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 (VAT
ACT 2014) wafanyabiashara ambao mauzo yao yote hufanyika nje ya nchi
hukadiriwa kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha sifuri (zero
rated) na kwa sababu hiyo basi hustahili kurejeshewa kodi ya VAT ambayo
huilipa kupitia manunuzi anayoyafanya hapa nchini.
Marejesho haya yanafanyika kwa uhalali na yanafuata matakwa ya sheria ya VAT. Ni muhimu ikaeleweka kwamba
makampuni haya bado yanalipa kodi ya VAT ambayo huwa
hairejeshwi iwapo yatafanya manunuzi ya bidhaa ama huduma ambazo
kisheria hazistahili marejesho. Kwa mfano makampuni haya yameendelea
kulipa bila kurejeshewa kodi ya VAT pale yanapofanya manunuzi hapa
nchini ya huduma za chakula kwa wafanyakazi wake pamoja na manunuzi ya
vipuri vya kwa ajili ya magari madogo ambayo ndiyo yaliyo mengi huko
migodini.
Ikumbukwe kwamba sheria ya VAT
ambayo makampuni ya uchimbaji madini yanafanya kazi chini yake ndiyo
hiyo hiyo ambayo inatumika pia kwa makampuni katika sekta nyingine za
uzalishaji ambayo mauzo yao yote hufanyika nje ya nchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya TMAA ya
mwaka 2015 sekta rasmi ya uchimbaji madini mkubwa inatoa ajira za moja
kwa moja 7,355 na zaidi ya 3,000 kupitia makampuni ya wakandarasi. Kwa
mujibu wa tafiti zilizofanyika huko nyuma ajira moja rasmi uhudumia watu
wengine 11 wasio na kazi. Kwa mantiki hiyo sekta rasmi ya madini
inawezesha wastani wa watu 114,000 kuendelea kuishi na kupata huduma za
msingi. Kodi zinazolipwa na makampuni ya madini husaidia kufanikisha
shughuli mbali mbali za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu muhimu
kwa maendeleo ya nchi yetu.
Chemba itaendelea kushirikisha
taasisi, mamlaka, vyombo mbali mbali vya habari pamoja na jamii kwa
ujumla, katika kuboresha uelewa wa wananchi na mamlaka za nchi kuhusu
jinsi gani wanachama wake wanatii sheria za nchi kuhusu kulipa kodi na
tozo mbali mbali kwa mujibu wa sheria na kanuni. Vile vile tutaendelea
kuelimisha jamii kuhusu mchango mkubwa ambao sekta rasmi ya uchimbaji
madini hapa nchini imekuwa ikiutoa katika uchumi wa nchi yetu kupitia
uwekezaji, ulipaji wa kodi, utengenezaji wa ajira, kuchangia soko la
fedha za kigeni, manunuzi ya huduma pamoja na michango ya hiyari (CSR)
kwa shughuli mbali mbali za maendeleo ya jamii.
Ni jambo la muhimu sana
kuhakikisha kwamba wadau wa sekta hii wanaielewa kwa ufasaha jinsi
inavyoendeshwa na kisha waiunge mkono ili iendelee kukua na kuchangia
zaidi katika pato la taifa.
Ni muhimu ifahamike kwamba pamoja
na kuwa na mikataba ya kisheria (MDA’s) ambazo zinatoa unafuu wa tozo na
kodi mbalimbali kwayo, bado makampuni haya yameridhia kutekeleza
matakwa kadhaa yaliyoingizwa na kanuni na sheria ya uchimbaji madini ya
mwaka 2010 (Mining Act, 2010) ili hali baadhi ya matakwa hayo yanakwenda
kinyume na mikataba (MDA’s) ambayo Serikali iliingia na makampuni haya
yalipokuja kuwekeza hapa nchini kwa mara ya kwanza. Kwa mfano badala ya
makampuni haya kulipa kiwango kisichozidi dola za kimarekani 200,000 kwa
mwaka kwa halmashauri kama ushuru wa huduma, makampuni haya yamekubali
kulipa ushuru huo kwa kiwango cha 0.3% ya thamani ya mauzo yote ya
madini. Makampuni pia yamekubali kulipa mrabaha kwa kiwango cha 4% badala ya 3% iliyo kwenye mikataba ya hapo awali.
Kuhusu Sekta ya Madini Tanzania
Historia ya uchimbaji wa madini hapa chini inaanzia enzi za
ukoloni wakati wafanyabiashara wazawa na wale wa ki-Arabu walipochimba
na kuuza maliasili za nchi hii ikiwemo Dhahabu, Shaba, Fedha, Chuma na
Chumvi. Uchimbaji wa kwanza wa kibiashara wa dhahabu ulifanyika katika
eneo linalozunguka ziwa Victoria chini ya utawala wa ki-Jerumani kati ya
miaka ya 1890. Kati ya miaka ya 1920 na 1930 miradi kadhaa ya uchimbaji
iliendelezwa na wamiliki kutoka Uingereza pamoja na Afrika ya Kusini.
Mojawapo ya miradi hiyo ilikuwa mgodi wa Almasi wa Williamson kule
Mwadui.
Kufuatia kupatikana kwa Uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961, uendeshaji wa sekta ya madini uliwekwa chini ya
Serikali na taasisi zake kama vile Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)
na Shirika la Uchimbaji Madini la Taifa (STAMICO). Sera mpya na sheria
zilizopitishwa mwishoni mwa miaka ya 1990 ziliwavutia wawekezaji wageni
ambao walianzisha migodi mikubwa ya uchimbaji wa dhahabu. Mgodi
wa kwanza wa aina hii ulianza uzalishaji mwezi Novemba 1998. Kwa sasa
hivi nchi yetu ina migodi mikubwa mitano ya uchimbaji wa Dhahabu na
mgodi mmoja mkubwa wa uchimbaji Almasi. Ipo pia migodi mingine ya
Dhahabu na Almasi ya kiwango cha kati pamoja na makampuni kadhaa
yanayoendeleza utafiti wa mashapo yenye madini kwa ajili uanzishwaji wa
migodi mingine siku zijazo kwa faida ya wadau wote.
Migodi yote mikubwa ya uchimbaji
madini iwe ya Dhahabu au madini mengine yoyote ni miradi ambayo huhitaji
mitaji mikubwa kuweza kuianzisha na utaalamu wa hali ya juu kuiendesha.
Kwa mantiki hiyo miradi hii huchukua muda mrefu kabla muwekezaji
hajarudisha gharama zake za uwekezaji na kuanza kutengeneza faida
inayostahili kukatwa kodi ya mapato. Hii haimaanishi kwamba migodi hii
inapata hasara bali ina maana kwamba kipato kinachozalishwa hakijawa na
sifa ya kukatwa kodi.
Hali hii ni ya kawaida katika
ulimwengu wa uchimbaji mkubwa wa madini na Tanzania haiwezi kuiepuka.
Majira ambapo kampuni itatakiwa kuanza kulipa kodi ya mapato yanaweza
kutofautiana na makisio yaliyoonyeshwa kwenye upembuzi yakinifu wakati
mradi husika unaanza kutokana na sababu mbali mbali ikiwamo kuporomoka
kwa bei ya madini husika na kupanda kwa bei ya mali ghafi zinazotumika
kwenye uzalishaji.
Katika kipindi ambacho mwekezaji
huendelea kurejesha mtaji wake mgodi huendelea kuchangia pato la taifa
na uchumi wa nchi husika kwa kulipa kodi zisizo za moja kwa moja kama
vile ushuru wa forodha, kodi ya zuio, ushuru wa huduma, tozo ya
kuendeleza stadi, (SDL) pamoja na PAYE na michango ya hifadhi ya jamii
ambayo pamoja na kwamba inatozwa kwa waajiriwa (na sehemu fulani hulipwa
na mwajiri – kwa michango ya hifadhi ya jamii) michango hiyo
isingekuwepo kama wafanyakazi wasingekuwa wameajiriwa katika mgodi
husika.
Vile vile ni vema ikaeleweka
kwamba hali hii ya kuchelewa kulipa kodi ya mapato hadi pale gharama za
uwekezaji wa mwanzo zitakaporudi si pekee kwa kampuni za uchimbaji
madini tu bali iko hivyo hata katika sekta nyingine za uzalishaji.
Tofauti pekee ni kwamba muda wa kusubiri huwa mrefu zaidi kwa uwekezaji
kwenye sekta ya madini kutokana na ukweli kwamba mtaji wake wa mwanzo
huwa ni mkubwa mno. Chemba itaendelea kushirikiana na kuhamasisha
mashauriano na Serikali kuhusu changamoto mbali mbali zinazoikabili
sekta hii ili kuhakikisha zinatatuliwa na kuiwezesha Tanzania kunufaika
ipasavyo na maliasili zake.
Imetolewa na Mwenyekiti
Tanzania Chamber of Minerals and Energy
Tanzania Chamber of Minerals and Energy
SHARE
No comments:
Post a Comment