Kaimu Waziri wa Afya Riziki Pembe
Juma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mripuko wa maradhi ya
kipindupindu Zanzibar huko Makao Makuu ya Wizara ya afya Mnazimmoja
Mjini Zanzibar.
Waandishi wa habari kutoka vyombo
mbali mbali vya Serikali na binafsi wakimsikiliza Kaimu Waziri wa Afya
Zanzibar katika mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini
Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Abdalla akijibu masuala yaliyoulizwa na
waandishi wa habari katika mkutano huo.
Picha na Makame Mshenga.
……………………..
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar 29.05.2017
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imepiga marufuku utaratibu wa kufutarishana na kupeana chakula
kilichotayarishwa nyumba moja kwenda nyengine katika mwezi huu wa
Ramadhani baada ya kubainika kuwepo kwa mripuko wa maradhi ya
Kipindupindu katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari
Makao Makuu ya Wizara ya Afya Mnazimmoja, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo
Riziki Pembe Juma alisema lengo la Serikali kuweka marufuku hiyo ni
kujaribu kudhibiti maradhi hayo yasisambae zaidi.
Alizitaja hatua nyengine ambazo
Serikali imechukua ni kuzuia uuzwaji holela wa vyakula vya kupika na vya
majimaji katika maeneo yasiyorasmi na kuwashauri wananchi kuchemsha
maji ya kunywa ama kuyatia dawa ya klorini, kukosha vizuri matunda na
mboga za majani kwa maji yaliyochemshwa.
Alisema uchunguzi uliofanywa kwa
wagonjwa waliolazwa kwa sababu ya kuharisha na kutapika katika vituo
vya afya na hospitali mbali mbali umebainisha kuwepo ugonjwa wa
kipindupindu aina ya Ogawa 01.
Waziri Riziki ameweka wazi
kupokewa wagonjwa 23 waliopatikana na vimelea vya ugonjwa wa
kipindupindu na tayari Wizara ya afya imefungua kambi maalum ya matibabu
katika eneo la Chumbuni.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika
zaidi na ugonjwa huo ni Wilaya za Mjini na Magharibi hasa katika Shehia
ya Kinuni, Darajabovu, Mtoni Kidatu, Chumbuni, Mwanakwerekwe, Fuoni na
Kwarara.
Hata hivyo Kaimu Waziri wa Afya
amethibitisha kuwa hadi sasa hajapatikana mgonjwa kutoka kwenye maeneo
ya ukanda wa pwani na zile kanda za utalii au kwenye hoteli za kitalii
na Kisiwa cha Pemba.
Amewaomba wananchi kuimarisha
usafi katika maeneo wanayoishi na watakaona dalili za ugonjwa huo
wakimbilie vituo vya afya huku Serikali imejipanga kwa dawa na
wafanyakazi na kutoa elimu ya afya katika kukabiliana na maradhi hayo .
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
Dkt. Fadhil Abdalla amewasisitiza wafanyabiashara wadogo wadogo kufuata
taratibu zilizowekwa na Wizara ikiwemo kupima afya kabla ya kuanza
biashara na kuandaa mazingira mazuri ya sehemu watakazofanyia biashara
zao.
SHARE
No comments:
Post a Comment