Simba SC imerejea kileleni mwa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Stand United ya Shinyanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 65 baada ya ushindi wa
leo wakiwa wamecheza mechi 29, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga
SC wenye pointi 62, ambao wanaweza kurudi kileleni kwa mabao zaidi,
wakiifunga Mbeya City kesho Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Stand United
ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa nyota wake, Suleiman
Kassim ‘Selembe’ aliyefunga sekunde ya 58 dakika ya kwanza.
Mchezaji huyo wa zamani wa Azam FC
ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga, alifunga bao hilo akitumia
makosa ya kiungo anayechezeshwa beki ya kati kwa sasa kutokana na uhaba
wa nafasi hizo, Mghana James Kotei.
Na ikawa rahidi kwa kiungo huyo, Selembe kufunga baada ya kipa
Mghana, Daniel Agyei naye kuvutika kutoka langoni, hivyo Mzanzibari huyo
akanyunyiza mpira nyavuni kiulaini.
Simba walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 23 kupitia
kwa mshambuliaji wake, Juma Luizio anayecheza kwa mkopo kutoka Zesco
United ya Zambia, aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya winga
Shiza Kichuya.
Juma Luizio tena akawainua vitini mashabiki wa Simba kwa
kufunga bao la pili na la ushindi dakika ya 35, kwa mara nyingine
akimalizia kazi nzuri ya Kichuya.
Kipindi cha pili milango ilikuwa migumu kwa pande zote mbili na
Simba ikafanikiwa kuvuna pointi tatu kwa ushindi wa 2-1 na kurejea
kileleni.
Kikosi cha Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, James Kotei, Shiza Kichuya/Abdi
Banda dk78, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Juma Luizio/Pastory Athanas
dk61, Jonas Mkude na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Mwinyi Kazimoto dk51.
Stand United; Frank Muwonge, Aaron Lulambo/Rajab Rashid dk81,
Jacob Massawe, Miraj Maka, Revocatus Richard, Erick Mulilo, Adam
Salamba, Kheri Khalifa/Sixtus Sabilo dk70, Frank Khamis, Ibrahim Job na
Suleiman Kassim ‘Selembe’.
SHARE
No comments:
Post a Comment