NA MWANDISHI
WETU, ARUSHA
WADAU wa sekta ya mifugo mkoani Arusha wameiomba Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwasaidia katika kuendeleza sekta hiyo
kwa kuwapatia mikopo na mahitaji mengine kwa ajili ya kuongeza tija katika
ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichofanyika
katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, kwa niaba ya wafugaji wa mkoa wa Arusha,
Kaimu Meneja wa Kiwanda cha Nyama cha Arusha, Bw. Fabian Kissiagi amesema
ukosefu na ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha za mtaji kwa ajili ya
maendeleo ya kilimo hasa katika sekta ya mifugo inawapa changamoto katika uendelezaji
wa sekta ya mifugo nchini.
Bw. Kissiagi ameongeza ukosefu wa mikopo ya uhakika
inarudisha nyuma ukuaji wa sekta ya mifugo na kurudisha nyuma juhudi za
serikali katika kuendeleza sekta ya mifugo.
“Hali ya ukosefu wa mitaji ya uhakika inachangiwa kwa
kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye
upande wa biashara za bidhaa na kutusahau sisi wakulima na wafugaji, hivyo
tunaiomba TADB kutusaidia kutatua changamoto hii,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,
Bw. Francis Assenga amesema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini
kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza
mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw. Assenga ameongeza kuwa sekta ya mifugo ni mojawapo
ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani
mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa
ng’ombe wa nyama na maziwa nchini.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza
uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa.
“Benki inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili
ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya kuhudumia ng’ombe
ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea na pamoja na usindikaji wa nyama na
maziwa kwa ajili ya kuongeza thamani nyama na maziwa,” alisema Bw. Assenga.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw.
Augustino Chacha amesema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo
ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2
hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka
Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika
kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha
kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na
kupunguza umaskini,” alisema.
Mkoa wa Arusha unashika nafasi ya tatu kati ya mikoa
yenye mifugo mingi nchini ambapo inakadiriwa kuwa na zaidi ya ng’ombe, mbuzi na
kondoo milioni tatu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
(aliyesimama) akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa
Mifugo mkoani Arusha kuhusu fursa za mikopo ya TADB. Kikao hicho kilifanyika
katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
(aliyesimama) akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa
Mifugo mkoani Arusha kuhusu fursa za mikopo ya TADB. Kikao hicho kilifanyika
katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw.
Augustino Chacha (aliyesimama) akizungumza kuhusiana na mikopo na huduma
zinazotolewa na TADB katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo.
Kikao hicho kilifanyika katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
Kaimu Meneja wa Kiwanda cha Nyama cha Arusha, Bw.
Fabian Kissiagi (aliyesimama) akizungumzia changamoto zinazoikabilia sekta ya
mifugo mkoani humo katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo
mkoani Arusha.
Meneja wa Uendelezaji wa
Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (wa pili kulia aliyesimama) akitoa takwimu
za mahitaji ya mikopo ya mkoa wa Arusha. Kulia ni Afisa Mwandamizi wa
Uendelezaji wa Biashara wa TADB, Bw. George Nyamrunda.
Ugeni kutoka TADB wakiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya Wadau wa Mifugo mkoani Arusha mara baada ya katika kikao cha
pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo. Kikao hicho kilifanyika katika Kampuni
ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
SHARE
No comments:
Post a Comment