Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekanusha kuwa nchi yake iko katika hali mbaya kiuchumi na kushikilia kuwa ni mojawapo ya mataifa yalioendelea zaidi barani Afrika.
Akizugumza katika mkutano wa jukwaa la kiuchumi duniani-World Economic Forum kwa Afrika, unaoendelea mjini Durban nchini Afrika kusini rais Mugabe amesema mataifa ya magharibi yamekuwa yakijaribu juu chini kuvuruga uchumi wa Zimbabwe.Katika mkutano huo wa Durban Rais Mugabe alisema serikali yake imepiga hatua katika kuimarisha hali ya maisha ya Wazimbabwe na hivi sasa asilimia 90 wanaweza kusoma na kuandika kinyume na ilivyokuwa awali.Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 alisema japo taifa lake linakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivi sasa mifugo wanatumika kufanya malipo mbalimbali ikiwemo karo ya shule, bado linashikilia nafasi nzuri kiuchumi ukiliganisha na mataifa mengine ya Afrika.
"Zimbabwe ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea zaidi barani Afrika na baada ya Afrika kusini sidhani kama kuna taifa lingine lilo na maendeleo makubwa kama Zimbabwe, tuna vyuo vikuu 14. Nakubali tuna matatizo yetu lakini sisi sio taifa maskini" alisema rais Mugabe.
Serikali ya Zimbabwe imekuwa ikishindwa hata kuwalipa mishahara wafanyikazi wa serikali na kwa mujibu wa ripoti ya shirika la umoja wa mataifa UNDP inashikilia nafasi ya 24 katika maendeleo barani Afrika.
Wakosoaji wanasema Rais Mugabe ameharibu uchumi wa nchi ambayo ilitegemewa zaidi kuongoza kiuchumi barani Afrika na pia kusababisha ukosefu wa ajira ambao kwasasa umefikia asimilia 80 ,kufuatia sera zake kama kuchukua kwa nguvu mashamba ya kibiashara yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu na pia uchapishaji fedha.
Licha ya maandamano ya mara kwa mara kupinga uongozi wake,rais Mugabe aliuambia mkutano huo wa Durban kuwa bado anaungwa mkono wa raia wengi.
" Uchumi haiwezi kukua kwa haraka kama watu wetu wanavyotarajia.Tunahitaji kuwekeza zaidi na uwekezaji huo unapaswa kuwa umeanzishwa zamani,lakini bado wengi wetu wamo katika kiwango cha chini.
Naye Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble ambaye ni miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huo ameitaka jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano wake na bara la Afrika ,akiongeza kuwa ushirikano mpya na nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani yaani G20 utafungua nafasi nyingi za uwekezaji Afrika.
Matamshi ya waziri huyo yamekuja siku mbili baada ya mwenzake wa mambo ya nje Sigmar Gabriel kuyataka mataifa ya Ulaya kuunganisha sera zao kuhusu Afrika, kutokana na kutozungumza kwa sauti moja.Mkutano huo unaokamilika hapo kesho unahudhuriwa na marais mbalimbali akiwemo mwenyeji Jacob Zuma,Yoweri Museveni wa Uganda miongoni mwa wengine.
SHARE
No comments:
Post a Comment