Mwandishi Wetu, Dar
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imekabidhi nguo wanafunzi wasioona 60 wa Shule ya Msingi Toangoma jijini hapa zilizoshonwa na kikundi cha wasioona kinachosimamiwa na mamlaka hiyo.
Nguo hizo ni msaada ulitolewa na wahitimu 12 wa mafunzo ya ushonaji ili kuwatia moyo watoto wenye ulemavu na kuwashawishi wasikate tamaa kwa sababu ya maumbile yao.
Akikabidhi nguo hizo hivi majuzi, Ofisa Mawasiliano Mkuu wa Tantrade, Theresa Chilambo alieleza faraja ya mamlaka yao kwa kushuhudia nguo zilizoshonwa na mafundi wasioona zinatumika kwa manufaa katika jamii.
“Sisi katika mamlaka tunafarijika na kuona fahari kwa tukio hili. Lengo letu ni kuwatia moyo watoto wenye ulemavu kufanya mambo yanayowezekana. Watafanya mambo hayo kama watawezeshwa na iwapo wataweka juhudi katika jambo wanaloliwania,” alisema Chilambo.
Alieleza kuwa vijana walioshona nguo hizo wanatoa ujumbe kwa vijana wenzao wenye ulemavu kwamba njia pekee ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili ni kukubali hali waliyonayo na kujituma.
Aliwaomba wadau wa maendeleo na hasa wafanyabiashara kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa aina mbali mbali ili wapate elimu itakayowaongoza kufikia malengo waliyojiwekea.
Tantrade inasimamia Programu ya Mafunzo ya ushonaji kwa wasioona yanayoongozwa na Bw.Abdallah Nyangalio ambaye ni kipofu pia na Chilambo amesisitiza: “Tumewahakikishia soko la bidhaa zao kupitia kituo cha huduma ya biashara cha mamlaka hii.”
Nyangalio naye amesema kuwa anafarijika kupata watu wenye juhudi na moyo wa kujifunza na kushona nguo hata kufikia hatua ya kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu katika jamii. Shule ya Toangoma imo katika Wilaya ya Temeke. Nyangalio anasimamia mafunzo haya ili kutoa fursa kwa walemavu wengine kupata ujuzi na baadae kujiajiri.
Mafunzo haya yameanza katika Wilaya ya Temeke, baadaye yataendeshwa katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam na kisha nchi nzima.
Mwalimu wa kitendo cha wasioona Bibi.Subira Shedangio, amesema kitendo cha wasioona kushona nguo na kutoa msaada ni ushahidi kuwa ulemavu si sababu ya kutofanya maendeleo.
"Kikubwa ni uwezeshaji wa nyenzo na wanafunzi kuwa na nia ya dhati kwa jambo wanalotaka kufanya. Mawili yakiwepo tunaweza kujiletea maendeleo,”alisema.
Tantrade inaendesha programu hii kuwapa walemavu ujuzi waweze kujitegemea.
SHARE
No comments:
Post a Comment