Benny Mwaipaja, WFM - Dodoma
29 Juni, 2017.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto pamoja na Shirika la Afya Duniani
(WHO), inakamilisha majaribio ya utafiti wa hali ya umasikini katika
mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro kabla ya kuanza utafiti huo nchi nzima
mwezi Agosti, mwaka huu.
Hayo
yamesemwa mjini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dk. Albina Chuwa wakati ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na
kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya
Takwimu mjini humo.
Amesema
kuwa ana matarajio kwamba mchakato wa taarifa za utafiti huo zitafanywa
mjini Dodoma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hiyo inayojengwa
kwa gharama ya shilingi 11.6 bilioni, zikiwa ni fedha za mkopo wenye
masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Dk.
Chuwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wakusanya taarifa
za utafiti huo ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za hali ya
umasikini nchini kwa ajili ya kutathmini programu mbalimbali na kupanga
mipango ya maendeleo ya wananchi wake.
Mshauri wa Masuala ya Takwimu kutoka Benki ya Dunia nchini Tanzania,
Elizabeth Talbert amesema kuwa Benki yake imetoa mkopo huo kwa ajili ya
ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar kutokana
na Benki hiyo kuona mchango mkubwa wa takwimu katika maendeleo ya nchi
yoyote ile duniani.
“Tumefurahishwa
na kasi ya ujenzi wa Ofisi hii hapa mjini Dodoma na tunaamini ujenzi
wake utakamilika kwa wakati ili kazi za kitakwimu ziweze kufanyika
katika mazingira mazuri na tunaamini hatua hii italeta mchango mkubwa
katika masuala ya kitakwimu hapa nchini” alisema Bibi Talbert.
Amesema
kuwa Jengo la Ofisi ya Takwimu kwa upande wa Zanzibar limekamilika na
huenda likaanza kutumika mapema Julai mwaka huu hatua ambayo inaleta
mageuzi makubwa katika tasnia hiyo ya ukusanyaji wa takwimu mbalimbali
zinazoisaidia nchi kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake.
Kwa
upande wake, Mkandarasi Msanifu Majengo, Mhandisi Ramadhani Shomvi
anayesimamia ujenzi wa jengo hilo litakalo kuwa na ghorofa 6, amesema
kuwa kampuni yake itakamilisha ujenzi huo mwezi Februari, 2018.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa (wa pili kushoto)
akingalia kitofali kinachotengezwa na mkandarasi anayejenga jengo la
Taasisi hiyo wakati Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na
kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya
Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.
Mshauri
wa Masuala ya Kitakwimu kutoka Benki ya Dunia nchini Tanzania,
Elizabeth Talbert (kushoto) akisisitiza jambo wakati Ujumbe kutoka Benki
hiyo ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya
Ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.
Mkandarasi
Msanifu Majengo, Mhandisi Shomvi (aliyevaa sweta kulia) anayesimamia
ujenzi wa jengo la ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa Mkoani Dodoma
akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo wakati Ujumbe
kutoka Benki ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo hilo
mjini Dodoma.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina chuwa (wa pili kushoto)
akifurahia jambo na timu ya wataalamu wa ujenzi na ujumbe kutoka Benki
ya Dunia ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu
ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu linalojengwa mkoani Dodoma.
(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
SHARE
No comments:
Post a Comment