Mshambuliaji amewagonga waumini waliokuwa wakitoka
msikitini kwa sala kaskazini mwa London na kumuua mtu mmoja na
kuwajeruhi wengine 10 katika shambulizi la kigaidi.
Gari kubwa lililokodishwa liligonga kundi la waumini waliokuwa
wakitoka sala za usiku muda mfupi baada ya saa sita za usiku katika
msikiti wa Finsbury Park, mojawapo ya misikiti mikubwa nchini Uingereza.
Shambulizi hilo limewalenga waumini hao wakati wa mwezi mtukufu wa
Ramadan.Abdulrahman Saleh Alamoudi aliyekuwa katika eneo la tukio amesema kuwa dereva wa gari hilo alifika nje ya msikiti akiligongesha huku na kule huku akipaza sauti akisema atawaua Waislamu wote.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amesema polisi wamethibitisha kuwa wanakichulia kisa hicho kama shambulizi la kigaidi na kuongeza ataongoza mkutano wa dharura wa kiusalama baadaye leo.
May kuitisha kikao cha usalama
Watu wanane wamekimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha huku wawili wakipokea matibabu katika eneo la tukio. Polisi imesema mtu mmoja alitangazwa kufa papo hapo na dereva wa gari hilo mwenye umri wa miaka 48 alizuiwa na umma kabla ya kukamatwa na polisi.
Polisi imesema mshukiwa huyo atafanyiwa uchunguzi wa akili hivi karibuni. Meya wa London Sadiq Khan amesema polisi zaidi wametumwa katika eneo hilo ili kuihakikishia jamii usalama wao hasa wakati huu ambapo Waislamu wanafunga.
Khan amelitaja shambulizi hilo kuwa tusi kwa maadili ya uvumilivu, uhuru na heshima. Kiongozi mkuu wa upinzani wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amesema ameshtushwa mno na shambulizi hilo ambalo limetokea katika eneo lake la uwakilishi.
Baraza la Waislamu nchini Uingereza limesema shambulizi la Jumatatu ndilo baya zaidi lenye ishara zote za chuki dhidi ya Uislamu nchini humo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni na kutoa wito wa usalama kuimarishwa katika maeneo yote ya kuabudu nchini humo.
Mwenyekiti wa msikiti huo wa Finsbury park Mohammed Kozbar amesema shambulizi lililowalenga Waislamu ni kitendo cha uoga na kuwaomba Waislamu kuwa waangalifu wanapokwenda misikitini kusali.
Kozbar amelalamika kuwa vyombo vikuu vya habari vilisita kwa saa nyingi kulitaja shambulizi hilo kuwa la kigaidi.
Shambulizi hilo la leo linakuja takriban wiki mbili tu tangu washambuliaji mnamo Juni 3 walipowagonga watu katika daraja la London na kuwadunga visu katika hoteli na baa zilizokuwa karibu na kuwaua watu wanane.
Mnamo tarehe 22 Mei, mshambuliaji wa kujitolea muhanga aliwaua watu 22 katika tamasha la muziki la muimbaji maarufu wa Marekani Ariana Grande mjini Manchester.
Tarehe 22 Machi, mshambuliaji mwingine aliyekodisha gari aliwagonga watu katika daraja Westminster mjini London karibu na bunge, akamuua afisa wa polisi kwa kumchoma kisu kabla ya yeye kuuawa.
Watu wengine watano waliuawa katika shambulizi hilo. Mashambulizi hayo yameuzonga utawala wa Theresa May anayeshutumiwa kwa kupunguza idadi ya polisi 20,000 alipokuwa waziri wa mambo ya ndani.
SHARE
No comments:
Post a Comment