“Kwa
mshtuko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Mkurugenzi
Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Kanda ya Afrika
Kusini Dkt. Tonia Kandiero aliyefariki dunia ghafla jana usiku tarehe 28
Juni, 2017 akiwa ofisini kwake huko Pretoria Afrika Kusini”
Hii
ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli aliyoitoa leo tarehe 29 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es
Salaam muda mfupi baada ya kupokea taarifa za kifo cha Dkt. Tonia
Kandiero ambaye kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa
AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka 2016
alikuwa Mwakilishi wa AfDB Tanzania.
“Nitamkumbuka
Dkt. Tonia Kandiero kama mchapakazi hodari aliyetoa mchango mkubwa
katika maendeleo ya nchi yetu, nikiwa Waziri wa Ujenzi nimeshirikiana
nae kwa karibu kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo
kwa nchi yetu ambayo imefadhiliwa na AfDB, ametoa mchango mkubwa
kufanikisha ujenzi wa madaraja na barabara za Dodoma – Iringa, Dodoma –
Babati, Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala, Arusha – Taveta – Voi na pia
alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha miradi mingine ambayo ipo
mbioni kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Tanga –
Mombasa, Mbinga – Mbambabay na Tabora - Katavi”.
Kufuatia
kifo cha Dkt. Tonia Kandiero Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Rais wa AfDB Dkt. Akinwumi Adesina, familia ya Dkt. Tonia
Kandiero, wafanyakazi wote wa AfDB, ndugu, jamaa na marafiki wote
walioguswa na msiba huu.
Dkt. Magufuli amemuombea marehemu Dkt. Tonia Kandiero apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Juni, 2017
SHARE
No comments:
Post a Comment