Na Ripota wetu
Watalii
wanaokuja Tanzania na kuelekea moja kwa moja kwenye hifadhi za taifa za
Serengeti, Kilimanjaro au Ngorongoro inamaanisha nini? Ni kwamba
wanakuwa wamekwishaambiwa kuwa ukifika Tanzania sehemu pekee za
kutembelea ni hizo tu? Je tunawezaje kukabiliana na hali hii ambayo kwa
namna moja ama nyingine inaweza kufifisha vivutio vilivyopo maeneo
mengine nchini kutotembelewa?
Hakuna
anayeweza kubisha kwamba sehemu ya Kaskazini mwa Tanzania imebarikiwa
kwa kiasi kikubwa kuwa na vivutio visivyopatikana duniani kote. Vivutio
kama hifadhi za kitaifa za Serengeti, bonge la Ngorongoro, Mlima
Kilimanjaro na hivi karibuni mti mrefu zaidi barani Afrika uligunduliwa.
Tunapenda
kukufahamisha kwamba tangu mwaka huu wa 2017 uanze nchi yetu
imeshuhudia watu mbalimbali maarufu duniani wakifurika nyanda za
Kaskazini wakiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Israel, Bw. Ehud Barak,
muigizaji wa filamu kutokea Hollywood nchini Marekani, Will Smith na
familia yake.
Kama
hiyo haitoshi hazijapita hata wiki mbili tangu aliyekuwa nguli wa
kusakata kabumbu nchini Uigereza, David Beckham ambaye aliwahi
kuvichezea vilabu vya Manchester United, Real Madrid, LA Galaxy na PSG
naye kutembelea hifadhi ya mbuga ya Serengeti akiwa na familia yake.
Huyo
hakuwa mchezeji pekee kutokea bara la Ulaya kufanya hivyo kwani nyota
anayechezea kwa mkopo katika klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi
kuu ya Uingereza akitokea Liverpool, Mamadou Sakho naye pamoja na mkewe
na watoto wake wa kike wawili wameonekana wakifurahi mapumziko yao
katika hifadhi ya mbuga ya wanyama ya Serengeti.
Jambo
la msingi la kujiuliza hapa ni kwanini watu hao wote mashuhuri pindi tu
watuapo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Nyerere hubadilisha ndege
na kuelekea moja kwa moja uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro
ambapo kutokea pale ni rahisi kwenda hifadhi za kitaifa za Serengeti,
Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro?
Tunafahamu
kwamba suala la watalii kutembelea sehemu wanazozitaka wanapofika
nchini Tanzania ni maamuzi yao na pia huchangiwa na sababu kadhaa kama
vile vivutio miundombinu kama vile usafiri, hoteli zenye hadhi na
kuvutia lakini pia na hali ya hewa kinaweza kuwa kigezo kingine.
Kwa
kuzingatia sababu za miundombinu na huduma bora za malazi na zenye
viwango vya kimataifa, hakuna ubishi kwamba nyanda za Kaskazini
zimejitahidi kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji ya watalii. Lakini
linapokuja suala la vivutio vya kitalii na hali ya hewa bado Tanzania
tumejaaliwa vivutio vya kila aina na hali ya hewa nzuri karibuni kila
mikoa ya nchi hii.
Kwa
mfano, ukitembelea mikoa ya Magharibi utakutana hifadhi za Gombe,
Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane. Kwa ukanda wa Mashariki kuna fukwe
safi za bahari ya Hindi, visiwa vya Zanzibara, hifadhi ya Saadani,
kisiwa cha Kilwa, mapango ya Amboni (Tanga) na Mikindani (Mtwara).
Wakati ukienda Kusini mwa Tanzania yapo mengi ya kufurahi na kuyaona
katika hifadhi za Kitulo, Mikumi, Ruaha na Udzungwa.
Utajiri
wa maliasili unaopatikana katika hifadhi hizo hapo juu ni Dhahiri
kwamba nchi ya Tanzania haijabarikiwa sehemu chache pekee. Bali tu ni
namna tunavyovitangaza, kuvitolea elimu ya kutosha na kuvipa kipaumbele
kwa wageni na watalii kuvitembelea.
Yapo mambo kadhaa ya kujifunza kutokana na ugeni wa watu hao mashuhuri kupendelea kuzuru baadhi ya sehemu tu nchini.
Kwanza
kabisa, kuwa na vivutio pekee haitoshi kuwashawishi watalii kuja nchini
kuvitembelea bila ya kuvitangaza. Dunia kwa sasa ina takribani zaidi ya
nchi 190 na zote hizo zikiwa na vivutio vya kila namna. Watalii
hawawezi kutembelea sehemu kama hawajafahamishwa ina mambo gani
yatakayowavutia na kushawishika kutoka huko walipo. Hivyo basi badala ya
kutegemea watalii na watu mbalimbali kusikia sifa za vivutio
tulivyonavyo Tanzania kutoka kwa watu wao wa karibu, serikali na
wananchi tunaowajibu wa kuvitangaza vivutio vyetu.
Lakini
pia, sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa huendena na uwepo wa miundombinu
ya kisasa na ya kuvutia itakayowawezesha watalii kuvifikia vivutio na
kufarahia muda wao pindi wanapokuwepo huko. Hapa tunazungumzia
miundombinu kama vile usafiri na huduma za malazi kitu ambacho mikoa ya
Kaskazini imejitahidi kuwekeza kwa kiasi kikubwa. Uwepo wa uwanja wa
ndege kimataifa wa Kilimanjaro, barabara na hoteli kadhaa zenye hadhi na
viwango vya kimataifa ni vichocheo vikubwa kwa watalii kupenda
kutembelea vivutio vya huko.
Hivyo
basi kwa kumalizia, bado serikali na wananchi kwa ujumla tunalo jukumu
la kuvitangaza na kuvilinda vivutio tulivyonavyo. Kwa kuvitangaza
tunaweza kulifanikisha hilo kwa kuvitembelea na kuwajulisha watu wetu wa
karibu juu ya mambo yanayopatikana huko. Pongezi kwa serikali kwani
siku chache zilizopita katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani
ilitoa ofa kwa watanzania wote kutembelea hifadhi za mbuga za wanyama
bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu mfululizo ili kujionea
mazingira na maliasili tulizojaaliwa.
SHARE
No comments:
Post a Comment