Ofisa Mradi wa Chama cha Uandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Godfrida Jola (kushoto) akifafanua jambo kwa wahariri wa habari Dar es Salaam juzi. Kulia ni Mkurugeni Mtendaji wa chama hicho, Edda Sanga.
Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimesema kuna idadi kubwa ya ndoa kuvunjika pamoja na utelekezaji wa familia.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Edda Sanga wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mradi wa uboreshaji wa maisha ya wanawake.
Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kwa ajili ya kutoa msaada wa kijinsia na kutilia mkazo, utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria.
"Utekezaji familia umekuwa mkubwa sana. Nilizungumza na Polepole (Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM) akaniambia ndoa nyingi zinavunjika kabla ya kufungwa," alisema Sanga na kuongeza;
"Kuna mtikisiko mkubwa ndani ya familia. Yanayoendelea ndani ya familia yanatisha. Kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ubakaji, ulawiti na ukatili na hivi vinafanywa na watu wa karibu ndani ya familia,".
Alisema kutokana na hali hiyo hata mfumo wa kupata viongozi unakuwa na matatizo na kuwaomba wahariri na waandishi wa habari kutumia kalamu na vyombo vyao vizuri kuelimisha jamii madhara ya vitendo hivyo.
"Tunapozungumzia kuandaa viongozi tunazungumzia na wale waliobakwa na kulawitiwa...tunafanya mambo ya ovyo hapa Tanzania," alisema.
Mkurugenzi alisema vitendo hivyo viovu vinafanywa hata na watu wenye nafasi za uongozi, waendesha bodaboda na shuleni yanayoendelea ni ovyo. Tutakuwa taifa gani jamani," alihoji.
SHARE
No comments:
Post a Comment