
Mwezeshaji wa
Kongamano hilo, Prof. Honest Ngowi (aliyesimama) akizungumza katika
Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji. Wengine picha ni watoa mada mbalimbali
walioshiriki katika Kongamano hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TADB, Bw. Francis Assenga (aliyesimama) akichangia nafasi ya Benki yake
katika kuchagiza uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mnyororo mzima wa
ongezeko la thamani katika kilimo.

Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), Dkt. Jim Yonazi
akizungumzia nafasi ya TSN katika kuwezesha juhudi za Serikali katika
kuwawezesha wananchi kiuchumi ambapo alisema kuwa Shirika lake lina
uwezo na teknolojia ya hali ya juu katika kuwafikia sehemu kubwa ya
watanzania. Alitoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kutumia nafasi
hiyo kuwafikia walengwa wa huduma zao.

Baadhi ya Manaibu Mawaziri wakifuatilia mada wakati wa Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji.

Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji.

Baadhi ya wadau wa taasisi za uwezeshaji wananchi kiuchumi wakifuatilia kwa makini Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji.

Baadhi ya wadau wa taasisi za uwezeshaji wananchi kiuchumi wakifuatilia kwa makini Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji.
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wito umetolewa kwa Watanzania
hasa kwa wadau wanaojihusisha na uwezeshaji wananchi kiuchumi kubadili
mitazamo juu ya namna sahihi ya kuwawezesha wananchi hao katika kutimiza
lengo la serikali la kuwainua wananchi kiuchumi ili kuimarisha kipato
na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Wakizungumza katika Kongamano la
Mwaka la Uwezeshaji linalofanyika mkoani Dodoma wadau hao wamesema kuwa
kuna ulazima wa wadau hao kujua mahitaji sahihi ya wananchi wanaohitaji
huduma za uwezeshaji wa kiuchumi kwa kuwa kila kundi lina mahitaji yake.
Mwezeshaji wa Kongamano hilo,
Prof. Honest Ngowi amesema kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote
unazingatia mahitaji maalumu ya kila sekta ya kiuchumi na kutolea mfano
kuwa wakulima nchini hawahitaji rasilimali fedha pekee ili kuongeza tija
katika kilimo chao bali wanahitaji masoko ya uhakika ya mazao yao.
“Uzoefu kutoka kwa watekelezaji
wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi unaonesha kuwa rasilimali fedha si
kila kitu pekee katika kuwawezesha wananchi kiuchumi bali kila kundi
linahitaji mahitaji yake, mfano mkulima anahitaji soko la mazao yake ili
aweze kuongeza tija kwenye kilimo chake,” alisema Prof. Ngowi.
Akichangia mjadala huo, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw.
Francis Assenga alisema kuwa Benki yake ina Dira ya kuwa benki ya mfano
na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania kwa kuwawezesha
wananchi kwa kuzingatia mahitaji maalumu kuendana changamoto za
kimaeneo hili kuwezesha wananchi kiuchumi nchini ili kutekeleza kwa
vitendo dhamira ya Serikali kuwafikisha wananchi wake kufikia hadhi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Muundo wa TADB ni tija katika
kuchagiza uwezeshaji wananchi kiuchumi hasa wakulima wadogo nchini kwani
Benki inafanyia kazi mnyororo mzima wa ongezeko la thamani katika
kilimo kwa kutatua changamoto mbali mbali kama vile kiwango kidogo cha
uzalishaji; ukosefu wa mbinu na teknologia za kisasa; matumizi madogo
ya umwagiliaji,” alisema
Aliongeza: “Changamoto nyingine
ni ukosefu wa mtaji na upatikanaji wa mikopo kwa wakulima; ukosefu wa
masoko ya mazao; ufinyu wa bei za mazao; miundo mbinu mibovu ya
usafirishaji; maghala ya kuhifadhi mazao; nishati ya umeme na
miundombinu hafifu vijijini; ufinyu au kutokuwepo kwa ongezeko la
thamani kwa mazao ya kilimo; mabadiliko ya hali ya hewa; na mmomonyoko
wa udongo, pamoja na changamoto zinginezo,” aliongeza.
Kuanza kufanya kazi kwa Benki ya
Kilimo kunaleta suluhisho la changamoto nyingi zilizokuwa zinaikabili
sekta kilimo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kama inavyowekwa bayana
na dhima ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo inalenga
kuwaongoza watanzania katika kujenga uchumi wenye nguvu kwa kuboresha
mazingira ya kibiashara na kutoa fursa sawa za kiuchumi.
Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji
linafanyika katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi iliyoundwa mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji namba.16
iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
SHARE








No comments:
Post a Comment