NA HAMZA TEMBA - WMU
..............................................................................
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na Balozi wa
Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke amezindua Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo
ya Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous SECAD (Selous Ecosytem Conservation and
Development Program) ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa
ushirikiano na Serikali ya Tanzania, mradi huo utatekelezwa na Wizara ya
Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA,
WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society).
Akizungumza
katika hafla iliyofanyika jana, Matambwe na Tagalala Selous, Mkoani Morogoro, Waziri
Maghembe alisema Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya KFW imechangia
Euro Mil. 18 (sawa na Shilingi Bil. 45.124) katika mradi huo wa miaka
mitano huku mashirika ya WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological
Society) yakichangia Euro laki 4 kila moja (sawa na Shilingi bil. 2.005) katika mradi huo.
Pamoja na uzinduzi huo alizindua pia Mpango Kazi wa Dharura wa kuendeleza pori
hilo.
"Mradi
huu ni muhimu sana kwakua utasaidia kuongeza nguvu kwenye jitihada zetu za
kuendeleza na kuimarisha hifadhi ya pori hili la Selous ikiwemo upatikanaji wa
vitendea kazi muhimu pamoja na kutuongezea nguvu kwenye mapambano dhidi ya
ujangili", alisema Prof. Maghembe.
Alisema
jitihada ambazo Serikali imeshazifanya katika pori hilo ni pamoja na kuimarisha
doria za ndege zenye rubani na zisizo na rubani (drones), kutoa mafunzo ya
jeshi usu kwa askari, kuongeza maaskari pamoja na vitendea kazi ambapo katika
mwaka ujao wa fedha Serikali itatoa magari mengine 15 kusaidia pori hilo.
"Pamoja
na jitihada hizo tunawekeza dola za kimarekani Milioni 156 (sawa na Shilingi
bilioni 349.441) kwa ajili ya kuboresha pori hili (Selous), Ruaha, Mikumi, Rungwa
na Kitulo kuhakikisha watalii wanatembelea maeneo haya na kuondoa kile kikwazo
cha wao kutotembelea hifadhi za kusini, hiyo inaenda sambamba na kuimarishwa
kwa shirika la ndege la Serikali la Air Tanzania na kuondoa changamoto
iliyokuwepo ya usafiri wa anga", alisema Prof. Maghembe.
Akizungumzia
changamoto ya ujangili katika pori hilo alisema Serikali imefanikiwa kwa kiasi
kikubwa kupambana na tatizo hilo ambapo majangili wengi wameshakamatwa katika
maeneo ya Tunduru, Namtumbo na maeneo ya katikati ya Selous. Alisema changamoto
hiyo bado ipo katika maeneo ya Mkoa wa Ruvuma ambapo imeripotiwa na kamati ya
ulinzi na usalama ya Mkoa huo kuwa kuna upatikanaji wa silaha za kivita kutoka
nchini Msumbiji ambazo zinapatikana kwa watu kubadilishana na magunia ya mchele
changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
Wakati
huo huo, Prof. Maghembe akijibu swali aliloulizwa na wanahabari kuhusu hatua
iliyofikiwa juu ya kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni ikiwa na dhamira
ya kuunganisha taasisi zote za uhifadhi nchini alisema, tayari ameshaunda
kamati ya watu sita ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Mweka, Prof. Japhary
Kidegesho kwa ajili kuangalia namna bora ya kutekeleza azma hiyo.
"Tayari kamati hiyo imeshaanza kazi na itaonana na wadau mbalimbali kupata
maoni yao na katika kipindi cha mwezi na nusu watatuletea ripoti",
alisema.
Kwa
upande wake Balozi Konchanke alimuahakikishia Prof. Maghembe kuwa Serikali ya
Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili hifadhi hiyo ikiwemo ubovu wa miundombinu
na uvamizi pori hilo kwa faida ya jamii kwa ujumla. Aidha, alitoa wito
kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kubuni mbinu mpya za
kukabiliana na changamoto zilizopo.
Meja
Jenerali Gaudence Milanzi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema
"Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi imefanya kazi kubwa
kuhakikisha Selous haiondolewi katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia
yaliyopo hatarini kutoweka, hiyo ni pamoja na kunzishwa kwa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyanapori Tanzania TAWA, kuanzishwa kwa mkakati wa kitaifa wa
kukabiliana na ujangili na miradi mbali ikiwemo huu wa SECAD uliozinduliwa leo
ambayo kwa kiasi kikubwa imeasaidia katika kuendesha hifadhi zetu pamoja na
kusaidia kwenye mapambano dhidi ya ujangili".
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, TAWA,
Martin Loibooki aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa mradi huo na kusema kuwa
utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika pori
hilo ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi, miundombinu ya barabara na ujangili na
hivyo kuifanya hifadhi hiyo iendelee kuwa miongoni mwa maeneo ya urithi wa
dunia.
Pori
la Akiba la Selous ni hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ikiwa ukubwa wa
Kilomita za mraba 50,000. Hifadhi hiyo ambayo ipo katika mikoa ya Morogoro, Pwani,
Lindi, Mtwara na Ruvuma ina vivutio vingi vya utalii huku ikikabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, ujangili, rasilimali
watu na vitendea kazi.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akipokelewa
jana katika uwanja mdogo wa ndege wa Matembwe uliopo Selous na Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin
Loibooki (wa pili kushoto) alipowasili kwa ajili ya hafla hiyo. Nyuma
yake anayeshuka kwenye ndege ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof.
Alexander Songorwa (kushoto).
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika hafla
hiyo iliyofanyika jana katika kituo cha Tagalala, ndani ya Pori la
Akiba la Selous Mkoani Morogoro.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke akizungumza katika hafla hiyo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika hafla hiyo jana.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Prof. Faustin Kamuzora akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja
Jenerali Mstaafu, Hamis Semfuko akizungumza katika hafla hiyo.
Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),
Martin Loibooki akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana,
Tagalala, Selous.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizindua Mradi
wa Uhifadhi na Maendeleo wa Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD)
ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali
ya Tanzania katika hafla iliyofanyika jana Matambwe, Selous Mkoani
Morogoro. Wanaoshudia kulia kwake ni Balozi wa Ujerumani, Egon
Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili, Meja Jenerali Gaudence
Milanzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Faustin Kamuzora.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Prof. Alexander
Songorwa Mpango Kazi wa Dharura wa Kuendeleza Pori la Akiba la Selous
baada ya kuuzindua sambamba na mradi wa Uhifadhi na Maendeleo ya
Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD). Kulia kwake ni Balozi wa
Ujerumani, Egon Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Faustin
Kamuzora, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania, Martin Loibooki na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA,
Dkt. Dembe.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na Balozi wa
Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke wakikata utepe kuashiria uzinduzi
wa magari sita aina ya Land Cruiser ambayo ni sehemu ya Mradi
aliouzindua wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la
Selous (SECAD).
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijaribu moja ya gari
baada ya uzinduzi wa magari sita aina ya Land Cruiser ambayo ni sehemu
ya Mradi huo.
Magari sita aina ya Land Cruiser yaliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kama sehemu ya mradi wa SECAD.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi
(kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira Prof. Faustin Kamuzora (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali
Mstaafu, Hamisi Semfuko (kulia).
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe (kushoto) akipokea zawadi
ya picha yenye ujumbe wa Mashujaa wa Kuokoa Selous kutoka kwa
Mkurugenzi wa Afrika wa WWF Ujerumani, Philipp Goltenboth (kulia).
Anaeshuhudia katikati ni Mkurugenzi Mkaazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani
Ngusaru.
Picha
ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe (wa
tatu kushoto), Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke (wa pili kushoto) na
viongozi wengine wakuu wa Wizara na Taasisi pamoja na washiriki wa hafla
hiyo. Nyuma yao ni ziwa Tagalala ambalo ni sehemu ya kivutio cha utalii
ndani ya hifadhi hiyo.
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba la Selous wakiwa katika hafla hiyo.
Taswira mwanana ya baadhi ya Twiga ndani ya Pori la Akiba la Selous.
SHARE
No comments:
Post a Comment