Askofu Blaston Gaville wakati akiwekwa wakfu kuongoza Dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
KUKAMILIKA kwa mchakato wa
uaandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutasaidia
kuweka misingi imara na kuondoa changamoto zilizopo katika Katiba ya
sasa, hivyo kukomesha ufisadi na kuinua uchumi wa Tanzania.
Aidha, kukamilika huko kwa Katiba
Mpya kutaakisi jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na
Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, ambaye alimtaka Rais Magufuli
kuumalizia mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, kwani alisema mbali ya
kuakisi kasi yake anayoifanya ya kukuza uchumi pia kutasaidia kuhimiza
uwajibikaji.
“Wakristo na Watanzania kwa
ujumla tuna imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano na ni matarajio
yetu kwamba mchakato wa kuandika Katiba utamalizwa kama lengo
lilivyokuwa,” alisema.
Askofu Gaville amesimikwa ili kuchukua nafasi ya Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella ambaye amestaafu.
Alisema wanatiwa moyo na jitihada
zinazoendelea kufanywa na Dkt. Magufuli katika kufufua uchumi na
kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya Watanzania
wote.
Alisema Tanzania ina wanyonge
wengi kuliko wenye nguvu, hivyo wanatiwa moyo na jitihada zinazofanywa
na Rais Magufuli na serikali yake hasa anapowatetea wanyonge.
Aidha, pamoja na kupongeza
jitihada hizo, Askofu Gaville, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa
kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi akisema hakuna nchi inayoweza
kupata maendeleo bila mapato hayo.
“Tunaiomba serikali iangalie upya
suala la kodi kwa mashirika ya dini kwani baadhi ya kodi tunazolipa,
ikiwemo ya kuendeleza vyuo vya ufundi na ya Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi, zimekuwa mzigo mkubwa kwaetu.
“Kazi ya Kanisa ni kutoa huduma,
siyo kutengeneza faida, kodi hizo zimeleta changamoto kubwa kwa
uendeshaji wa taasisi, tunaomba serikali iziangalie upya,” alisema.
Kuhusu elimu, Askofu Gaville
alisema Kanisa linasaidia watoto maskini ili wapate haki yao ya elimu na
akaiomba serikali isiwaingize katika kundi la watoto wanaotoka katika
familia zenye uwezo kwa sababu wanasoma shule binafsi.
“Wanapojiunga na vyuo vikuu,
tunaomba Bodi ya Mikopo isiwanyime mikopo stahiki kwa kisingizio cha
shule wanazotoka, ufanyike upembuzi ili kutoa msaada kwa walengwa wote,”
alisema.
Aidha, alisema Dayosisi ya Iringa
inatoa mwaliko kwa vyama vyote vya kisiasa na jamii nzima ya Watanzania
kuendeleza na kukuza tunu ya ushirikiano na moyo wa kizalendo ili kuwa
na maendeleo yenye tija, badala ya kujenga uhasama kwa sababu za
kiitikadi.
Katika salamu zake kwa waumini wa
dayosisi hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania, Dkt. Fredrick Shoo,
alizipongeza kamati mbili za madini zilizoundwa na Rais Magufuli akisema
zimewaumbua baadhi ya Watanzania waliodhani ni sifa kusaini mikataba ya
madini inayonyonya haki ya Watanzania.
“Kama hao watu waliosaini hiyo
mikataba walidhani wanaisadia nchi huku wakijua mikataba hiyo inalenga
kuiibia nchi, wajue hayo ni mambo ya aibu na ni upumbavu mkubwa kufanya
mambo kama hayo kwa ajili ya matumbo yao binafsi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi,
Jamuhuri William, akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Amina Masenza, alisema serikali itaendelea kushirikiana na
taasisi zote za dini ili kufikia malengo yake ya maendeleo.
William alizungumzia fursa
mbalimbali za maendeleo zilizopo mkoani Iringa na akawaomba Watanzania
na wawekezaji kuzitumia ipasavyo kuunga mkono jitihada za Rais za
kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Katika hatua nyingine, Askofu
Mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dkt. Owdenburg Mdegela, aliipongeza serikali
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua mbalimbali inazochukua
kujirekebisha.
Akiungana na mamia ya wakazi wa
Mkoa wa Iringa katika maandamano ya amani siku moja kabla ya kumsimika
Askofu Gaville, Dkt. Mdegela alisema moja ya makosa makubwa yaliyofanywa
na serikali lilikuwa ni kuua Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Maandamano hayo yalifanyika mjini
Iringa kwa nia ya kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli
katika kushughulikia changamoto zinazolikabili Taifa, ambapo
yalipokelewa katika viwanja vya Mwembetogwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza, huku yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, siasa
na serikali, watumishi, wanafunzi, wafanyabiashara na wadau wengine wa
maendeleo kutoka wilaya zote za mkoa huo.
“Hatukupaswa kuua Azimio la
Arusha pamoja na kwamba kuna mambo yalipaswa kubadilishwa. Kimsingi
azimio lile lilikuwa na mambo mengi ya msingi ambayo ni ya faida kwa
Taifa, hayo ni pamoja na maadili kwa viongozi na msingi wa kujitegemea,”
alisema.
Alibainisha wazi kwamba, serikali
ya CCM ilichoka, lakini kupitia kwa Rais Magufuli imeanza kujirekebisha
ikiwa ni pamoja na kutembea katika misingi ya Azimio la Arusha, hatua
inayopaswa kupongezwa hadharani.
“Anayempinga Rais anayekamata
wezi, watumishi hewa na anayepambana kulinda rasilimali za nchi kwa
manufaa ya Watanzania wote na kuhimiza uwajibikaji lazima atakuwa
alipata matokeo mabaya ya mtihani wa darasa la saba na kidato cha nne.
“Tunapaswa kuiona falsafa ya
kiongozi wetu pamoja na kwamba wapo watu wanambeza kwa maneno mengi ya
kuudhi lakini wanaombeza Magufuli wakumbuke kwamba hata Mungu alibezwa
na theluthi moja ya malaika zake,” alisema.
Amina Masenza, katika utangulizi
wake, alisema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 inasema katika miaka
mitano ijayo, CCM itazielekeza serikali zake kutumia nguvu zake zote
kuondoa umaskini, kutatua tatizo la ajira hasa kwa vijana, katika vita
dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na kudumisha amani, ulinzi
na usalama.
SHARE
No comments:
Post a Comment