Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Balozi Dkt. Augustine
Mahiga (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu
mazungumzo ya pamoja kuhusu mahusiano ya kibiashara kati ya Serikali ya
Tanzania na Kenya mapema jana jijini Dar es Salaam, katikati ni Mkurugenzi,
Idara ya Ushirikiano wa Kikanda toka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Balozi Innocent Shiyo na kushoto ni Kaimu Balozi wa Kenya nchini
Tanzania Peter Sang.
NA PASCHAL DOTTO - MAELEZO
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Kenya zimefanya mazungumzo ya pamoja na kutatua vikwazo
vilivyokuwa vikiikabili sekta ya biashara baina ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini
Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Dkt. Augustine Mahiga ametoa taarifa juu ya kumalizika kwa tofauti za
kibiashara baina ya nchi hizo.
“Bidhaa za Tanzania zilizowekewa vikwazo na nchi
ya Kenya ni unga wa ngano pamoja na gesi ya kupikia (LPG). Aidha
juhudi, za Serikali ya Tanzania kuona vikwazo hivyo vinaondolewa na Serikali ya
Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda, hivyo Serikali ya Tanzania nayo iliweka
vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya kuingia katika soko la
Tanzania,” amefafanua Dkt. Mahiga.
Amesema kuwa kutokana na mahusiano mazuri ya
udugu yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya na kwa kujali manufaa
mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, Rais
wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli walikubaliana kuzungumza na kutoa
vikwazo vya biashara hizo.
Aidha, Dkt. Mahiga amesema, nchi hizo zimekubaliana
kuunda Tume ya pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha tofauti za
kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi changamoto za
kibiashara kati ya nchi hizo mbili pindi zinapojitokeza.
Tume hiyo itaongozwa na Mawaziri wa mambo ya Nje
wa Tanzania na Kenya na kujumuisha mawaziri wanaohusika na masuala ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi
na Utalii wa nchi hizo.
Mkurugenzi,
Idara ya Ushirikiano wa Kikanda toka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Balozi Innocent Shiyo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu mazungumzo ya pamoja kuhusu mahusiano ya kibiashara kati ya
Serikali ya Tanzania na Kenya mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Balozi Dkt. Augustine
Mahiga.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakimfuatilia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wa Tanzania Balozi Dkt. Augustine Mahiga (hayupo pichani) wakati
akitoa ufafanuzi kuhusu mazungumzo ya pamoja kuhusu mahusiano ya kibiashara
kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya mapema hii leo jijini Dar es Salaam.(PICHA NA ELIPHACE MARWA –MAELEZO)
SHARE
No comments:
Post a Comment