Said Mwishehe
MACHO yangu yanaogopa kuona yanayoendelea lakini pia masikio nayo yanaogopa kusikia.
Unashangaa nini? Huoni yanayoendelea? Maisha yetu yameanza kuwa na hofu nyingi kila kukicha. Hakuna mwenye uhakika na maisha yake ya kila siku. Nikiri nchi yetu hakuna mwenye mashaka na amani iliyopo.
Lazima tuendelee kuitunza na kuithamini. Binafsi nitakuwa wa kwanza daima katika kuliombea taifa letu liwe na amani. Kwa Ujinga Wangu najaribu kufuatilia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini kwetu.
Yapo ambayo kwangu sikuwahi kuyaona ila sasa nayaona. Sitaki kuzungumzia yanayoendelea kuhusu waliopo mahabusu za Keko au Segerea jijini Dar es Salaam.
Sitaki kuzungumzia maana kwa uwezo wangu wa kuona na kusikia umefika mahali ambapo unaona bora niwe kimya huenda nikawa salama zaidi.
Nakumbuka niliwahi kuambiwa si kila jambo la kulizungumzia nadhani hata hili kwangu ni bora niwe kimya. Kila mtu atazungumza kwa wakati wake.
Hata hivyo, macho yangu hayataki kuona na masikio nayo hataki kusikia yanayoendelea wilayani Kibiti mkoani Pwani. Juzi tumesikia tena kuna mtu mwingine ameuawa na watu wasiojulikana.
Inaumiza na kusikitisha sana maana idadi ya watu waliouawa hadi sasa ni kubwa na ndani yake wapo askari polisi na viongozi wa kisiasa. Hakuna mwenye akili timamu anayetaka kusikia habari mbaya za aina hiyo.
Utamaduni wetu Watanzania siku zote pale ambapo kuna tatizo watu hukaa pamoja na kutafuta suluhu. Hatuna utamaduni wa kupigana wala kunyoosheana vidole lakini sasa hali imeanza kuwa tofauti na hasa Kibiti na Mkuranga ambapo matukio ya watu kuuawa yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro
Kwa Ujinga Wangu natamani wauaji wakamatwe wote ili kurejesha hali ya amani kwenye maeneo hayo. Wananchi wengi wa Kibiti na Mkuranga hawana uhakika na maisha yao. Hawajui nani anaweza kukumbwa na mkasa mbaya.
Tuombe Mungu atuepushe na matukio hayo ya mauaji. Wananchi wa Kibiti na Mkuranga mnalo mjukumu la kuhakikisha mnashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa taarifa za wapi walipo wanaojuhisha kufanya mauaji hayo.
Ni kweli vyombo vya ulinzi vinaendelea na kazi yake ya kusaka wahalifu hao lakini wananchi nao ni wajibu wao kutoa taarifa sahihi.
Kwa Ujinga Wangu nieleze tu kama kuna mwananchi wa Kibiti au Mkuranga anayefurahia yanayoendelea basi atakuwa anajidanganya kwani mwisho wa siku hao wahalifu watakuja kwa hao wanaofurahia.
Macho yangu natamani kuona wananchi wa Kibiti na Mkuranga wanaishi kwa amani.Kibiti wanakuwa wamoja katika kufanya mambo ya maendeleo na kubwa zaidi ni kuuona Mkoa wa Pwani uko salama.
Pia masikio yangu yanatamani kusikia habari njema na si habari za huzuni kama ambavyo zimekuwa sikisikika mara kwa mara.
Nikiri nina imani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika juhudi zake za kusaka wahalifu katika maeneo hayo lakini nitumie nafasi hii kusisitiza kuwa wananchi nafasi yao ni kubwa kuliko ya vyombo vya ulinzi katika kukomesha mauaji yanayoendelea Kibiti.
Kwa Ujinga Wangu natamani kuona Watanzania kokote tulipo tunashiriki katika kuhakikisha maeneo yote ya nchi yetu yanakuwa salama na watu wake wanaishi bila ya kuwa na hofu.
Ni jukumu la kila mmoja wetu kuiona Kibiti ikiwa salama na maisha ya wananchi yanaendelea kama kawaida kwenye shughuli zao za kijamii. Kwa Ujinga Wangu sijui kwanini naanza kuona kama vile kuna aina ya maisha ambayo tunataka kuyaishi na hayakuwa utamaduni wetu.
Halafu nikwambie ujue siku hizi kila mtu anaishi kwa tahadhari kubwa. Si tajiri wala masikini kila mtu yupo makini kwa kila analofanya. Si unajua tena. Kwa mfano angalia hawa ambao...unasubiri unafikiri nataka kukwambia nini? Imetosha kwa leo.
Kwa maoni
0713833822
SHARE
No comments:
Post a Comment