Julian Msacky
SIKU hizi kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili ndani ya jamii
yetu, ikiwemo kwenye sekta zetu za utoaji wa huduma.
Hali hii imesababisha madhara makubwa kwa baadhi ya watu
kutokana na namna wanavyofanyia au kutendewa.
Ninasema hivi kwa sababu ukienda hospitali utakutana na kauli
za kuudhi na adha nyingine ambazo kimsingi zinaumiza moyo.
Muulizeni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, George Simbachawene atakueleza mengi.
Waziri huyo amekiri hivi karibuni kuwa yeye ni miongoni mwa
waathirika wa huduma mbaya na manyanyaso wanayofanyiwa wagonjwa.
“Haya mambo uhadithiwe tu, lakini usikutane nayo, hivi
karibuni nilifiwa na kaka binamu katika Hospitali ya Sinza Palestina, kumbe
alikuwa na tatizo la kifua kikuu ambalo halikugundulika mapema,” anasema.
Niharakishe kusema hapa kuwa anachosema Simbachawene
kimewakuta wengi na kubaki wakiumia kimoyo moyo.
Swali ni je, taalumu hizi za utaoji huduma tuliambiwa ni
wito, lakini siku hizi zimekuwa tofauti kabisa.
Ukienda hospitali ni shida. Ukienda benki ni shida. Ukienda
sehemu ya kutafuta haki ni shida. Sasa watu wakimbilie wapi?
Nini kimekwenda mrama? Wapi tulipokosea? Haya ni maswali
ambayo kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza ili kupata majibu.
Ni kweli tumefikia hatua ya kuishi mithili ya wanyama wa
porini ambako mwenye nguvu ndiye anastahili kuishi?
Au ni kwa nini siku hizi utu umepotea mno miongoni mwetu? Ni
kwa nini kitu upendo kimekuwa bidhaa adimu kwa wengi wetu?
Ninanavyoona ni kana kwamba tumechanganyikiwa au
hatujitambui. Iwe kwa aliyesoma au asiyesoma lao ni moja.
Kwenye jamii ya aina hii ni lazima tukiri kuna kosa mahali.
Ni lazima tukiri jamii la aina hii inahitaji msaada wa haraka ili isiangamie.
Maana kama upendo kwa mgonjwa haupo maana yake ni hatari.
Kama haki hakuna maana yake ni shida. Ni mzunguko hatari.
Ni lazima tutafute majibu ya matatizo yetu. Ni lazima
tujiulize ni kwa nini uzalendo umepotea miongoni mwetu kwa kiwango kikubwa.
Zamani tuliambiwa ualimu ni wito na ili mtoto wako alelewe
vizuri mahali pa kumpeleka ni kwa mwalimu. Je, hali ipo hivyo?
Ni walimu wangapi wanacharaza watoto na kufikia hatua ya
kuwavunja sehemu ya viungo vyao? Kweli hayo ndiyo malezi?
Au mama anapomchoma mtoto eti amedokoa mboga ni namna ya
kumbadilisha au kumfunza mtoto au tunamfundisha kuwa katili.
Najaribu kuwaza tu. Mtu anapokwenda Polisi, je, anahudumiwa
inavyotakiwa? Anasikilizwa? Yapo mazingira ya rafiki ya kusikilizana.
Au mwendesha gari au pikipiki anapochepuka njiani na
kusababisha ajali, anasimamisha gari au anakimbia na kumuacha aliyegongwa?
Mambo ni mengi. Hii ndiyo jamii tunayoishi. Hebu angalia
maeneo yetu ya kazi kuna amani. Lugha zinazotumika zinafaa?
Maneno kama vile “mjinga au mpumbavu” yanajenga tunapoyatumia
katika sehemu zetu za kazi au tumefilisika kifikra?
Kwa viongozi wetu wa kiraho wanatimiza majukumu yao
inavyotakiwa. Hapa tena kuna maswali mengi kuliko majibu.
Hii ni kwa sababu kondoo wametawanyika na viongozi wa kiroho
wanaona. Mmomonyoko wa maadili unatishia umoja wa familia zetu.
George Simbachawene
Ni lazima viongozi hao wa kiroho wafanyie kazi ya ziada ya
kuvunja nguvu za Ibilisi kwa sababu anaonekana kuteka roho za wengi.
Viongozi hao wana kila sababu ya kutumia vipaji vyao
kupandikiza mema kwa jamii pana ili iendelee kuishi kwa amani na upendo.
Inabidi wafanyie hivyo kwa nguvu zote ili upendo kwa Mungu na
jirani uwepo. Bila kufanya hivyo itakuwa ni tatizo kubwa.
Angalia namna siku hizi watu wanauana ovyo. Angalia
yanayoendelea Pwani. Haya yote yanahitaji nguvu ya Mungu kuyaondoa.
Ni kazi ya viongozi wa kiroho kuingilia kati kuhakikisha watu
wanaishi kwa amani. Watu wanaacha kuuana. Wanaacha uovu.
Ni imani yangu kuwa viongozi hao wakitimiza wajibu wao vizuri
mambo yote mabaya ambayo yanaitesa jamii yataondoka.
Jambo la msingi hapa ni kila mmoja wetu kubadilika. Kuacha
njia mbaya. Kuacha chuki. Kuacha visasi na mihemko isiyo na sababu.
Kwa njia hiyo tutatengeneza jamii inayojitambua. Jamii
inayopendana. Jamii inayojiheshimu na yenye hofu ya Mungu.
SHARE
No comments:
Post a Comment