Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mwanachuo wa Chuo cha
DIT, Groria Shoo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Momba zinazojengwa na Shirika la Taifa la
Nyumba katika eneo la Chitete wialyani Momba Julai 21, 2017. Gloria
anafanya kazi kwa muda akijifunza katika shirika hilo. Kushoto kwake
ni mkewe Mary na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
Nyumba la Taifa, NHC, Blandina Nyoni. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameliagiza Shirika la nyumba Nchini kwenda kujenga nyumba bora za makazi
katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa na wilaya ili
kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.
Pia ameweka jiwe la msingi katika
mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya
Momba mkoani Songwe zinazojengwa katika kijiji cha Tindingoma,
unaojengwa na Shirika la Nyumba Nchini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jumaa, Julai 21, 2017 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba
akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.
“Nalipongeza Shirika la Nyumba
kwa mikakati waliyonayo ndani ya shirika hilo na kwamba waendelee na
utekelezaji wa mipango hiyo ya ujenzi wa nyumba ili maeneo yote mapya ya
utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi watumishi.”
Pia aliwataka wakazi wa kata ya
Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya Momba kuhakikisha
wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya kwenye kata yao
kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha watumishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu
wa NHC, Bw. Nehemia Mchechu amesema mradi huo wenye thamani ya sh
bilioni 2.2 ulianza kujengwa Machi 2016 na unatarajiwa kukamilika
Septemba mwaka huu.
Amesema mradi huo ulibuniwa
baada kupokea maombi kutoka Halmashauri ya wilaya ya Momba na kwamba
unatekelezwa kwa awamu mbili ya kwanza ni ujenzi nyumba nane na tayari
zimekamilika.
Ameongeza kwamba ujenzi wa awamu
ya pili unajumuisha nyumba tisa ambapo gharama ya ujenzi wa nyumba
itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi za Halmashauri
hiyo.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya NHC ,
Bi. Blandina Nyoni amesema shirika hilo lilianzisha mpango wa ujenzi wa
nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha
wananchi kuwa na makazi bora.
Amesema katika miradi 54 ya
ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na shirika hilo katika maeneo mbalimbali
nchini kati yake miradi 24 imekamilika ikiwemo 14 ya nyumba za gharama
nafuu.
Pia Mbunge wa jimbo la Momba
(CHADEMA) Mheshimiwa David Silinde amesema anashukuru Serikali kwa
ujenzi wa nyumba hizo na kumueleza Waziri Mkuu kwamba wananchi wa Momba
wanaridhishwa na utendaji wa Serikali na kwamba maendeleo
hayana chama.
SHARE
No comments:
Post a Comment