Na Mwandishi Maalumu, Lufilyo
Jana, Jumamosi tarehe
22 Julai 2017 ilikuwa siku ya kipekee familia ya Profesa Mwark Mwandosyak kwani Wananchi wa Busokelo
walifanya tafrija pale Lwangwa, Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya
Busokelo, ya kumuaga rasmi kama Mbunge wao kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka
2000 mpaka mwaka 2015.
Akiwa amehemewa na
tukio hilo, Profesa Mwandosya alisema hiyo ni heshima iliyoje kwake, Mke wake
Lucy Akiiki, watoto wao; Max Mwandosya, Sekela Mwandosya, Emmanuel Mwandosya,
na wajukuu Tusekile, Lusekelo, na Queen Maria, Mkwe Digna Mwandosya, na ndugu
na marafiki wa karibu.
Katika risala iliyosomwa kwa niaba yao na Mwalimu Juma
Mwakikuti, Mwalimu Mkuu wa Seminari ya Manow, Wananchi wa Busokelo, au Rungwe
Mashariki kama Jimbo lilivyojulikana kabla ya kuwa Halmashauri kamili,
walishukuru kwa kile walichoona kama mchango mkubwa alioutoa katika maendeleo
ya Busokelo, Rungwe, Mbeya na Tanzania kwa ujumla, katika kipindi ambacho
Profesa Mark Mwandosya alikuwa Mbunge wao.
Waliorodhesha mambo
mengi ikiwa ni pamoja na: elimu; afya; mawasiliano; miundombinu; utamaduni;
utawala (kuanzishwa kwa Halmashauri); maji safi karibu kila kijiji; umeme kila
kata kuanzia mwaka 2002; mshikamano wa Jimbo; michezo; Kituo cha Utamaduni,
Mila, Historia, na Desturi za Wanyakyusa; Benki ya NMB; Ujenzi kupitia Shirika
la Nyumba la Taifa; na kadhalika.
Kipekee walimshukuru Mama Lucy Mwandosya kwa kulea watoto
yatima na kuwasomesha kuanzia chekechea mpaka vyuo vikuu, na kujenga kituo cha
ufundi cha watoto hao ambacho amekikabidhi kwa Serikali na sasa kimekuwa Chuo
cha Ufundi cha VETA.
Pia walishukuru kwa kuunganishwa
na Dunia kwa kupata wageni wengi kutoka nchi mbali mbali, ikitimia ahadi ambayo
Profesa Mwandosya aliitoa mwaka 2000
kwamba si lazima Busokelo iifuate Dunia, bali Dunia itaifuata Busokelo.
Wananchi wa Busokelo
waliikabidhi familia ya Profesa Mwandosya zawadi mbali mbali ikiwa ni ishara ya
shukrani na kwa ajili ya kumbukumbu.
Akijibu risala hiyo, Profesa Mwandosya, kwa niaba ya familia
yake iliyowakilishwa na Mama Lucy Mwandosya, Emmanuel Mwandosya, Wazee wake, na
Malifumu wake, aliwashukuru sana wananchi wa Busokelo kwa heshima kubwa
waliyompa kuwatumikia kwa muda wa miaka 15 mfululizo, na kumchagua, bila
kupingwa, vipindi vyote vitatu kuanzia mwaka 2000.
Alisisitiza kwamba
hastahili hata kidogo kupewa heshima na shukrani bali yeye ndiye angewashukuru
Wananchi na angelikuwa na uwezo angeliwaandalia hafla Wananchi wote wa Rungwe
Mashariki ili kuwashukuru! Aliuliza, kati yake na Wananchi, nani hasa apewe
shukrani? Jibu lake ni Wananchi. Bila wao kumkubali,alisema, asingeweza kufanya
lolote. Yeye alikuwa ni chachu tu ya maendeleo.
Pili aliwasihi waendeleze elimu kwa kila hali na kila hatua
kwani bila elimu maendeleo ya binadamu ni duni. Amewaomba wasiridhike na idadi
na ukubwa wa shule zilizopo kwani idani ya wananchi inaongezeka kwa kasi, kiasi
cha kwamba miaka 15 ijayo tatizo la mwaka 2000 litajitokeza tena.
Amewaomba viongozi
kusimamia ujenzi wa vituo vya mafunzo ya wakulima ili kilimo kiwa cha kisasa na
sio cha ujima. Aliwakumbusha kwamba Katika Mkoa wa Kilimanjaro barabara za lami
zimefika kila Tarafa. Hivyo basi wasicheleweshe ujenzi wa barabara ya lami ya
Katumba-Lwangwa- Tukuyu kwa kuipeleka Serikali Mahakamani kwa madai ya kulipwa
fidia kwanza, hasa pale ambapo tayari uthamini umefanywa, akisisitia kwamba
fedha za Serikali ni chache. Zinagombaniwa. Zinaenda pale zinapohitajika zaidi.
Aliwakumbusha na
kuwashukuru kwamba walikubali ushawishi wake wa kutotaka fidia ili umeme
usambazwe kila kata hata kabla ya Mradi wa Umeme Vijijini.
Aliwaomba viongozi
wa Halmashauri na Dayosisi ya Konde KKKT kuhakikisha kwamba ujenzi wa Chuo
Kikuu Kishiriki, Manow unakamilika, licha
ya changamoto zilizojitokeza.
Tatu alikiri kwamba alisononeshwa sana na baadhi ya wananchi
wa Wilaya ya Rungwe kuchoma kwa kutumia
matairi barabara kuu ya kutoka Uyole kwenda Kasumulu na Malawi kutokana na
tofauti za kisiasa mwaka 2015, akisema kuwa barabara hiyo ni mshipa wa damu
katika maendeleo ya Wilaya, Mkoa na Taifa.
Aliwaahidi yeye, familia yake, na marafiki zake wataendelea
kushirikiana na Wananchi wa Busokelo katika kusukuma maendeleo, na kusisitiza
wasiridhike kabisa na hali waliyonayo, akisisitiza elimu, elimu, elimu, elimu.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa pia na Mheshimiwa Njobelo,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo; Mheshimiwa Atupele Mwakibete,
Mbunge wa Busokelo; Mheshimiwa Cynthia Hilda Ngoye, Mkuu wa Wilaya na Mbunge
Mstaafu (Viti Maalum Mkoa wa Mbeya); Ndugu Meckson Mwakipunga, aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo; Walimu Wakuu; Viongozi wa
Dini, na wawakilishi kutoka kila kata.
Globu ya jamii pia
inachukua nafasi hii ya kumpongeza Profesa Mark Mwandosya, mmoja wa watu wa
kwanza kabisa kututia moyo na kutupa msaada mkubwa wa mawazo na kubwa kuliko
yote ni kuonesha waziwazi kuamini kwamba tufanyalo ni sahihi na daima
alisisitiza tusichoke na tuendelee kuendesha Michuzi Blog kiweledi huku tukifuata
misingi yote ya taaluma, |
No comments:
Post a Comment