WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,
ametoa maelekezo ya namna ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa
zaidi ya miaka sita, kati ya uongozi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya na
wananchi wa kijiji cha Nanyala, wilayani Mbozi.
Mgogoro huo, umetokana na
Kiwanda cha Saruji Mbeya, kupewa eneo la kijiji hicho chenye ekari
2,315 na uongozi wa mkoa wa Mbeya bila ya makubaliano na wanakijiji hali
iliyosababisha wagome kuondoka.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza
wakuu wa Mikoa ya Songwe Luteni Mstaafu Chiku Gallawa na wa Mbeya Bw.
amos Makalla kukutana na kufanya mazungumzo ya kulirudisha eneo hilo
mkoa wa Songwe.
Waziri Mkuu alitoa uamuzi huo
leo (Jumatatu, Julai 24, 2017) baada ya wananchi wa kijiji hicho kuzuia
msafara wake kwa lengo la kumuelezea changamoto yao ya kudhulumiwa ardhi
yao na kukabidhiwa kwa muwekezaji bila ya kushirikishwa.
Amesema Serikali ya awamu ya
tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ni sikivu na inawajali
wanyonge ndio maana amesimama ili aweze kusikiliza kero zao na kuzipatia
ufumbuzi, hivyo amewaomba waendelee kuiamini na watarudishiwa ardhi
yao.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza
Kampuni ya Saruji Mbeya kuondoa kesi iliyoifungua mahakamani dhidi ya
wananchi wa eneo hilo, ili waweze kukutana na Serikali pamoja na
wananchi hao kwa ajili ya kujadili namna bora ya uwekezaji katika eneo
hill.
Amesema kiwanda hicho kilipewa
eneo hilo la mkoa wa Songwe kimakosa na mkoa wa Mbeya kwa ajili ya
kupata malighafi ya kutengenezea saruji, amesema Serikali haiwazuii
kulitumia eneo hilo ila wakubaliane na wananchi kwanza.
“Hatuzuii kiwanda kufanya kazi
ila tunataka mkubaliane na wananchi kwanza ili kuondoa migogoro.
Wananchi wanahitaji viwanda ila si kwa migogoro. Wananchi nawaomba
muendelee kuwa na amani na hakuna atakayechukua ardhi yao bila ya ridhaa
yao.”
Eneo hilo lilikuwa mali ya
Serikali toka mwaka 1987, ambapo wakati Kampuni ya Saruji Mbeya ilikuwa
inamilikiwa na Serikali, kabla ya kubinafsishwa.
Wananchi hao wamesema
wamefurahishwa na uamuzi huo wa Waziri Mkuu wa kutatua mgogoro huo
ambapo wananchi hao walidai kwa muda mrefu ulikuwa ukiwasumbua kwa
kutakiwa kuondoka katika eneo lao bila na kukabidhiwa kwa muwekezaji
bila ya kushirikishwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa
wa Songwe amemshukuru Waziri Mkuu kwa kulitolea tamkoa suala hilo na
kwamba atakutaka na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya utekelezaji wa
agizo hili ili wananchi waweze kuishi kwa amani katika ardhi yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 24, 2017
SHARE
No comments:
Post a Comment