Baraza la Wazee wa Yanga wamesema
kuwa wanamtakia mafanikio mema kiungo mshambuliaji wake, Simon Msuva
anayetarajia kujiunga na Klabu ya Difaa El Jadidi inayoshiriki Ligi Kuu
ya Morocco.
Katibu wa Baraza la Wazee la
Yanga, Ibrahim Akilimali amesema kuwa kwa upande wao wanatoa baraka zote
kwa mchezaji huyo ili aweze kufanikiwa zaidi baada ya kuitumikia Yanga
kwa mafanikio makubwa.
“Leo (jana) tulikuwa na kikao cha
Baraza la Wazee wa Yanga na kikubwa ilikuwa ni kujadili suala la kijana
wetu Msuva ambaye ameuzwa kwenda kucheza soka Morocco, wazee wa Yanga
kwa upande wetu tumeridhia kuondoka kwake.
“Unajua kwa upande wetu ni heshima
kubwa kwa klabu yetu kufungua milango ili vijana wetu waweze kucheza
soka la kulipwa, mafanikio aliyotuachia ni makubwa na tunayaheshimu kwa
sababu siku akiamua kurejea kucheza hapa atarudi kwenye timu yake ambayo
imemkuza na kumpa mafanikio,” alisema Akilimali.
Klabu hiyo ya Morocco iliyoshika
nafasi ya pili msimu uliopita, imekubali kumlipa Msuva mshahara wa dola
4,000 (Sh 9m), kiasi ambacho awali aligoma akidai ni kidogo kwa sababu
anakwenda kuishi ugenini.
Wakati huohuo, Msuva amesema
anajua mazingira anayoenda kukutana nayo huku akipanga kuonyesha uwezo
wa juu ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza.
“Kabla ya kukubali dili la
kutimkia Difaa El Jadidi, nilipata muda wa kuitazama ligi yao kubaini
aina gani ya mbinu wanazitumia na nimegundua ni kama hapa Tanzania tu
yaani hakuna tofauti yoyote ile.
“Kule wanatumia mawinga zaidi
kwenye kutengeneza mabao kwa kupiga mipira mirefu pamoja na pasi za
haraka, sasa ukiangalia mbinu hiyo mimi nimeicheza sana Yanga na ndiye
nilikuwa injini ya kutengeneza mabao, jambo hilo linanipa matumaini ya
kuona kwamba sitapata shida ya kufiti na kuingia kwenye mfumo wao,”
alisema Msuva.
SHARE
No comments:
Post a Comment