
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
Deogratius Ndejembi akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali wa
Tarafa ya Nzoisa wilayani humo katika semina ya kujenga uelewa wa namna
ya kutekeleza majukumu yao kwa pamoja.

Katibu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM)mkoa wa Dodoma Jamila Yusuph akifungua semina hiyo kwa
viongozi wa chama na serikali ngazi ya Tarafa ambapo amesisitiza
ushirikiano,upendo na umoja katika kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM
iliyopo.

Baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wa Tarafa ya Nzoisa walioshiriki semina hiyo.

Katibu wa CCM mkoa wa Dodoma
akiongoza viongozi wa Chama na Serikali wa wilaya ya Kongwa kuimba wimbo
wa Chama katika semina hiyo,miongoni mwa viongozi hao yupo mkuu wa
wilaya hiyo Deogratius Ndejembi,katibu wa CCM wilaya Mfaume Kizigo na
mwenyekiti wa halmashauri White Zubeir.
…………………
Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya
Kongwa mkoani Dodoma kimewakutanisha viongozi wa serikali na wa Chama
ngazi ya Tarafa katika semina ya siku moja lengo likiwa ni kuwapa uelewa
wa pamoja wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Akifungua semina hiyo katika kata
ya Nzoisa wilayani Kongwa Katibu CCM mkoa wa Dodoma Jamila Yusuph
amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa pamoja ili kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya Chama hicho kama ilivyoahidiwa.
Ili hilo litekelezeke amewaasa
kujenga umoja na maelewano katika sehemu zao za kazi kwa kuelezana
ukweli pale wanapoona kuna jambo haliendi sawa na kutatua kero za
wananchi kama walivyoahidi.
Alisema viongozi wa Chama na
Serikali wakiwa tofauti ilhali kazi ya kupeleka maendeleo kwa wananchi
kutokana na Ilani iliyopo inapaswa kufanya kwa ushirikiano wanakuwa
wanawakosea wananchi walioichagua CCM na kuiweka madarakani.
“Huwezi leo mtendaji wa kijiji au
Kata unataka kukutana na wananchi lakini mwenyekiti wa CCM Kata au tawi
hajui chochote,hujamshirikisha hapo tegemea mkutano wako kutofanikiwa
maana Chama ndio kinakuwa na wananchi wakati wote na kina
ushawishi,”alisema Jamila.
Aliwataka kufanya kazi kwa bidii
ili yale anayoyafanya rais John Magufuli yaweze kuonekana mpaka nchini
kwa kuitekeleza Ilani kwa vitendo,kutatua kero na changamoto za
wananchi,kutii sheria za nchi,kukemea kwa vitendo suala la rushwa na
ubadhirifu wa mali za umma.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi ndani
ya chama uliomalizika katika ngazi ya Kata amewataka wote walioshinda
kuwaunganisha wana CCM popote walipo na waimarishe matawi na mashina.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya
Kongwa Deo Ndejembi akizungumza katika kikao hicho aliwahimiza viongozi
wa serikali kuitekeleza Ilani iliyopo na viongozi wa Chama wawasimamie
ili kuhakikisha viongozi hao wanatimiza wajibu wao katika kutekeleza
kile kilichoahidiwa kwa wananchi.
“Mwenyekiti wa Kata au Tawi lazima
uulize lini mara ya mwisho kusomwa mapato na matumizi,lazima ujue
mkutano umefanyika lini,bila ya kutatua kero za wananchi
watanung’unika,watakuwa na nyongo na nyongo hiyo kuitema wataitema
kwenye karatasi wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu
wa 2020,
“Kuna watu wanasema mimi ni
mkali,lakini jamani mfano wewe afisa elimu Kata,kuna mwalimu yupo mjini
siku zote lakini hujui kama anafundisha,wananchi wanakereka na hali hiyo
maana watoto wao hawafundishwi sasa nikae kimya?nikiuliza useme mi ni
mkali?kwa kweli niiteni tu mkali lakini siwezi kukaa kuona mambo
hayaendi halafu nikawa kimya,lazima kila kiongozi atekeleze wajibu wake
na Ilani,”alisisitiza Ndejembi.
Naye katibu wa CCM wilaya ya
Kongwa Mfaume Kizigo alisema lengo la kuwakutanisha pamoja viongozi hao
ni kuhakikisha wanajenga nyumba ya CCM pamoja,kuepuka migogoro kati yao
baada ya kila mtu kujua mipaka yake ya kazi na wanatarajia kuitoa katika
tarafa zote zilizobaki ndani ya wilaya hiyo.
SHARE
No comments:
Post a Comment