Kaya 6019 halmashauri ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga kunufaika na TASAF
Walengwa wa mpango wa kunusuru
kaya maskini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
wilayani Kishapu wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku katika kijiji cha
Mwigumbi kata ya Mondo.
Sehemu ya walengwa wa kaya maskini wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku kijij cha Mwigumbi
Sehemu ya walengwa wa kaya maskini wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku kijij cha Mwigumbi.
…………………………………………………………………………..
Na Robert Hokororo
Kaya 6019 katika halmashauri ya
wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, zinatarajia kunufaika na fedha sh.
milioni 204.6 zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu
ya tatu
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa
TASAF wilayani humo, Sospeter Nyamuhanga ofisini kwake wakati
akizungumzia zoezi la uhawilishaji fedha hizo linalotarajiwa kuvifikia
jumla ya vijiji 78.
Alisema kuwa zoezi hilo
linatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Agosti 7 hadi 11 mwaka huo katika
vijiji lengwa kwenye kata zilizo katika mpango wa TASAF III wilayani
humo .
Nyamuhanga alifafanua kwa kusema
kuwa zoezi la uhawilishaji fedha kwa kaya hizo linaanza kwa lengo la
kuziwezesha kaya maskini ili zikwamuke kutoka hali ya umaskini.
Mratibu huyo alisema kuwa katika
kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya wanakaya 54 wameingizwa kwenye
mpango huo wa TASAF III wakiwemo watoto waliozaliwa katika kipindi
hicho.
“Lengo la mpango wa TASAF ni
kuhakikisha walengwa wanatimiza masharti kama ya kuwapeleka watoto shule
ili baadaye wapate elimu ambayo itawaondoa katika umaskini na pia
kuhakikisha wanawapeleka kwenye huduma za afya kupitia fedha hizi,”
alisema.
Mratibu huyo aliongeza kwa
kubainisha kuwa mpango wa TASAF wilayani Kishapu umeonesha mafanikio
yakiwemo baadhi ya kaya kubadilika kimaisha kwa kufuga mifugo kama
ng’ombe na mbuzi.
Alisema kuwa baadhi ya walengwa
tayari wamebadilisha aina za makazi yao kutoka nyumba za tembe na nyasi
na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali inayoleta matumaini
katika miradi kama hii.
Mratibu huyo amesema mfuko huo
unatoa ruzuku za aina mbili, ya msingi inayotolewa kwa kaya zote
masikini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine ni ya utimizaji
masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa kwenda shule
na vituo vya kutolea huduma za afya
Aidha, Nyamuhanga aliwataka
wanufaika kuwa na matumizi sahihi ya fedha wanazopata ili lengo la TASAF
la kuwatoa katika umaskini na kuwafanya wajitegemee litime.
Kishapu ni miongoni mwa
halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba
zinazotekeleza Mpango wa TASAF III ili kuongeza kipato na fursa za
kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.
SHARE
No comments:
Post a Comment