Muwakilishi
wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi
Sekta ya Mipango na Uratibu Bw.Samweli Tenga akizungumza wakati
akifungua mafunzo kwa watumiaji wa Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mipango
na bajeti za Serikali za Mitaa uitwao PlanRep yanayofanyika Mjini
Kigoma kwa siku 8 kuanzia jana.
Mkurugenzi
wa Mradi wa PS3 Dkt. Emmanuel Malangalila akitoa maelezo kuhusu mradi
wa Maboresho ya Sekta za Umma unaotekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya
Rais TAMISEMI kwa Ufadhili wa USAID.
Muwakilishi
wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Elisa Rwamiago akizungumzia faida za
mfumo huo katika kuongeza tija wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa
watumiaji wa mfumo huo leo mjini Kigoma.
Mkuu wa Timu ya Mifumo ya TEHAMA kutoka PS3 Bw. Desderi Wengaa akitoa maelezo kuhusu mradi huo Leo mjini Kigoma.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi.
Mgeni
Rasmi katika Hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo akiwa kwenye picha ya
pamoja na washiriki mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo.
Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo Kigoma
……………………
Frank Mvungi-Maelezo Kigoma
Maboresho
katika Mifumo ya Sekta za umma yametajwa kuwa Kichocheo cha Mafanikio
ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa yatasaidia kutoa mrejesho wa mara
kwa mara kwa ngazi zote za Utawala kwa wakati.
Akizungumza
wakati akifungua Mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo kutoka Mikoa ya
Kigoma, Katavi na Rukwa, Mwakilishi wa Katibu tawala wa Mkoa wa Kigoma
Bw. Samwel Tenga ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema dhamira ya Serikali
ni kuona watoa huduma wanaweza kujipima kwa kuangalia matokeo kwa kuwa
mfumo huu ulioboreshwa utaongeza uwazi,ufanisi na uwajibikaji katika
utoaji huduma kwenye sekta za umma.
“Kutokana
na maboresho na kurahisishwa kwa Teknolojia,mfumo huu mpya wa PlanRep
umefanywa kuwa ‘web based’ hivyo utawezesha Halmashuri kuingiza taarifa
za Mipango na Bajeti moja kwa moja kwa njia ya mtandao na kuweza kutumwa
kwenye mfumo mmoja uliopo Ofisi ya Rais TAMISEMI na hatimaye kuingizwa
kwenye bajeti kuu ya mwaka husika,” Alieleza Tenga.
Akifafanua Tenga amesema kuwa utaratibu wa awali wa kuandaa bajeti na
Mipango ulitumia rasilimali nyingi ikiwemo fedha na muda hali
iliyozorotesha utoaji wa huduma ambapo kwa sasa changamoto hizo
zitaondolewa na mfumo mpya ulioboreshwa.
Ameeleza
kuwa mfumo utasaidia kuongeza tija na kuwawezesha watumishi katika
maeneo ya kutolea huduma kuwa na muda wa ziada katika kuwahudumia
wananchi kwa kuwa mipango na bajeti vitafanyika katika vituo vya kutolea
huduma.
Aliongeza
kuwa Halmashuri sasa zitatakiwa kuongeza tija katika kuwahudumia
wananchi kwa kuwa PS3 imekuwa katika zoezi la kufunga mitambo ya
intaneti Local area network-LAN katika Halmashuri 93 zilizopo katika
mradi hivyo alizitaka Halmashauri zote kuhakikisha kuwa zinatumia vyanzo
vyake vya mapato kuweka LAN ili kuongeza kasi yakuwahudumia wananchi.
Pia
alipongeza PS3 kwa kuandaa mafunzo yakuwajengea uwezo watumiaji wa
mfumo huo,Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa Maboresho ya Sekta za Umma
kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani USAID ambao
wamekuwa washirika wa maendeleo wa Serikali kwa muda mrefu hali
iliyopelekea kuwepo kwa mafanikio makubwa siku hadi siku katika Mikoa na
halmashuri hapa nchini.
Akizungumzia
faida za mfumo huo amesema kuwa utasaidia Serikali kuokoa rasilamli
fedha zilizokuwa zikitumika awali kuandaa bajeti na mipango yake kuanzia
ngazi ya watoa huduma hadi Taifa hivyo matokeo ya kuwepo kwa mfumo wa
PlanRep ulioboreshwa yataonekana kupitia huduma wanazopata wananchi
mara utakapoanza kutumika mwaka wa fedha 2018/2019.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa mradi wa PS3 Dkt. Emmanuel Malangalila
amesema Dhamira ya mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni
kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo hiyo ili kuongeza
tija na kuboresha huduma za Serikali kwa jamii hasa zile zenye uhitaji
zaidi.
Akifafanua
Dkt. Malangalila amesema mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitano na
utakamilika ifikapo mwaka 2020, Mfumo huo utatumika kuleta uwiano kati
ya matumizi na huduma zitolewazo.
Aliongeza
kuwa mafunzo ya PlanRep yanawashiriksha washiriki takribani 92 kutoka
Halmashuri 16 za mikoa ya Kigoma,Rukwa na Katavi.
Naye
muwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bw. Elisa Rwamiago
akizungumza wakati wa mafunzo hayo amesema kuwa dhamira ya Serikali ni
kuleta mabadiliko katika mifumo ya kiutendaji Serikalini hasa katika
swala zima la Kupanga Bajeti,Mipango na Kutoa ripoti hali itakayosaidia
kufikiwa kwa maendeleo ya kweli kwa wananchi kupitia huduma na miradi
inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuzingatia vipaumbele vyao.
Mradi
wa PS3 unalenga kushirikiana na Serikali katika kuboresha matumizi ya
rasilimali zilizopo ikiwemo fedha na rasilimali watu katika ngazi ya
kutolea huduma kama vile vituo vya Afya,Zahanati,Hosipitali na katika
sekta ya elimu.
SHARE
No comments:
Post a Comment