Mawakili kutoka nje ya nchi wanaomtetea bilionea wa kampuni ya kufua
umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh
Sethi, kuhusu kupewa dhamana, jana walikwamisha usikilizwaji wa maombi
hayo.
Bilionea huyo na mwenzake James Rugemalira, wanakabiliwa na kesi ya
uhujumu uchumi wakidaiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka katika
Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), isivyo
halali.
Pia, wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo ni miongoni
mwa mashtaka yasiyo na dhamana, lakini washtakiwa, kila mmoja kwa wakati
wake wameamua kusaka dhamana katika Divisheni ya Makosa ya Uhujumu
Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka amemuwekea pingamizi bilionea huyo
katika maombi yake hayo, ambalo lilipangwa kusikilizwa jana na Jaji
Winfrida Korosso, lakini usikilizwaji wa pingamizi hilo ulikwama baada
ya bilionea huyo kuamua kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Seth aliamau kuyaondoa mahakamani maombi hayo kutokana na kuhusisha
mawakili kutoka nchini Afrika Kusini, ambao aliwakodi kuongeza nguvu kwa
kushirikiana na mawakili wazawa kumpigania katika dhamana yake hiyo.
Maombi ya kuyaondoa maombi hayo mahakamani yalitolewa na kiongozi wa
jopo la mawakili wanaomtetea bilionea huyo, Melkizedeck Lutema, baada ya
kubainika mawakili hao wa nje hawakuwa na sifa za kufanya kazi nchini.
Ingawa mawakili hao walikuwa hawajatambulishwa mahakamani, lakini katika
nyaraka mbalimbali zinazohusiana na maombi hayo, wametajwa kuwa
miongoni mwa mawakili wake.
Kutokana na kasoro hiyo Wakili Lutema aliiomba mahakama iyaondoe maombi
hayo kwa lengo la kuanza upya mchakato wa kuyawasilisha mombi ambalo
mahakama iliridhia.
Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango, alisema mawakili hao hawana
cheti cha kufanya kazi katika mahakama za hapa nchini kutoka kwa Jaji
Mkuu.
Wakili Mango alisema kuwa ili wakili kutoka nje ya nchi aruhusiwe
kufanya kazi katika mahakama za ndani ni lazima aombe kibali kutoka kwa
Jaji Mkuu ambacho analazimika pia kukilipia, jambo ambalo mawakili hao
hawakuwa wamelifanya.
Seth na Rugemalira wanakabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye
jumla ya mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mujibu
wa sheria za Tanzania mashtaka hayo hayana dhamana na hadi sasa
washtakiwa wanasota mahabusu.
SHARE
No comments:
Post a Comment