TRA

TRA

Friday, August 11, 2017

MICHEZO YA KUBAHATISHA SASA KULIPIA KODI KWA KAMISHNA WA KODI ZA NDANI

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


pic+TRA
Na Agness Moshi – MAELEZO.
Waendesha michezo ya kubahatisha na wadau waliokua wakilipa kodi kwenye Bodi ya Michezo Tanzania (Gaming board of Tanzania) wametakiwa kulipia kodi  na mawasilisho ya  makusanyo yao kwa kamishna wa kodi za ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya imesema kuwa kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Fedha namba 4 ya mwaka 2017 yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Sheria ya Michezo ya kubahatisha sura namba 166, TRA imepewa jukumu la kukadiria,kukusanya na kuhasibu kodi kwenye michezo hiyo kuanzia Julai 1, mwaka huu.
Katika kutekeleza majukumu hayo taarifa hiyo imeeleza kuwa, wadau pamoja na waendesha michezo hiyo wana wajibu wa  kuwasilisha makusanyo yao pamoja na kulipa kodi stahiki kwa kamishna wa kodi za ndani  wa mamlaka hiyo kwa muda uliowekwa kisheria ili kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa.
Aidha , taarifa hiyo imewataka walipaji kodi hao kuzingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja  na kusajili biashara hiyo ili kupatiwa namba ya mlipakodi (TIN) kwa wasiosajiliwa,kuwasilisha makusanyo ya kodi ya michezo hiyo na kulipia kodi hizo kwa kuzingatia viwango vilivyoainishwa kwenye Sheria ya michezo ya kubahatisha.
 Walipa kodi wametakiwa  kutumia namba za utambulisho wa michezo hiyo ‘GFS CODE’ pindi wafanyapo malipo na kuwasilisha makusanyo yao  kwenye ofisi walizofanyia usajili.
“Kwa waendesha biashara hiyo walioko jijini  Dar es Salaam ambao walipata namba za utambulisho kwenye mikoa ya kikodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke wanatakiwa kuwasilisha  makusanyo yao  kwenye ofisi ya TRA iliyopo  Mtaa wa Lumumba, wilaya ya Ilala ghorofa ya tatu summit Tower. Kwa waliopo  mikoa mingine watahudumiwa kwenye mikoa ya kodi walikopatia utambulisho wa mlipakodi”,ilifafanua taarifa hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo amesema kuwa kodi hiyo kwa waendeshaji michezo ya kubahatisha sio kitu kipya ila kilichobadilika ni mahali pa kulipia.
“Mabadiliko haya yanatokana na marekebisho ya Sheria ya michezo ya kubahatisha sura namba 166 yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sheria ya fedha namba 4 ya mwaka 2017” amesema Kayombo.
Hata hivyo, Mamlaka ya mapato Tanzania  imetoa wito kwa walipakodi wote kulipa kodi na kuwakilisha makusanyo yao  kwa wakati ili kujiepusha na adhabu na gharama zisizo za lazima zitakazotokana kutokulipa kodi kwa wakati.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger