TANZANIA
SOCIAL SUPPORT FOUNDATION
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu
MFUKO WA ELIMU YA JUU
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
YAH: KUANZISHWA KWA MFUKO WA ELIMU YA JUU WA TSSF
1
Utangulizi
Ndugu
Wanahabari,
Tanzania Social
Support Foundation inayo heshima kubwa mbele yenu kwanza kumshukuru Mwenyenzi
Mungu aliyetujaalia uzima na nguvu za kuweza kufika hapa tulipo, pamoja afya
njema, vitu ambavyo vimetufanya leo hii tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa
ufanisi, kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii.
Pia TSSF inawashukuru sana
kwa kuwa mmekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mnaihabarisha jamii na
hivyo kuutekeleza wajibu wenu vema na kwa ufanisi mkubwa.
Vilevile TSSF
inachukua fursa hii kutoa salamu za pole kwenu kutokana na changamoto
mbalimbali ambazo zinaikabili sekta ya habari hapa nchini lakini tunawasihi
kwamba mzidi kujiimarisha ili muweze kukabiliana na misukosuko mbalimbali
ambayo itakuwa inaathiri shughuli zenu.
Aidha TSSF inawahakikishia kwamba, ipo
pamoja na ninyi na itakuwa tayari kutoa msaada wake kwenu pale itakapo hitajika
kufanyika hivyo.
2. Mfuko wa Elimu ya Juu wa TSSF
Ndugu
Wanahabari,
Tangu kurasimishwa
kwa Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya Mwaka 1999, kumekuwepo na ongezeko la
watanzania wengi ambao wana hitaji la kupata elimu ya juu walau kwa ngazi ya
stashahada pamoja na shahada ya kwanza.
Hitaji hili ndilo lililofanya
kuanzishwa kwa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
Sura ya 178 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Mfuko wa
Elimu, Sura ya 412 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha kwa Mwaka 2016/2017 Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ilidahili wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 69,539 ambapo idadi hiyo ya wanafunzi wa elimu ya juu iliongezeka ikilinganishwa na Mwaka 2015/2016 ambapo wanafunzi waliodahiliwa ni 64,919 na tofauti ya ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa katika elimu ya juu kwa takwimu za miaka 2015/2016 na 2016/2017 ni 4,620.
Aidha
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Sura ya 178 ya Sheria za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambapo bodi hiyo ina jukumu la kutoa mikopo na ruzuku
kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini. Katika Mwaka wa Masomo 2016/2017
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilipokea maombi 88,163 ambapo
waliopata mikopo ni wanafunzi 28,785
sawa na 32.7% ya waombaji wote ambao waliomba mkopo wa elimu kutoka bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Vilevile waombaji waliokosa mikopo kutoka
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ni 59,378 sawa na 67.3% ya waombaji
wote ambao waliomba mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Kwa
upande mwingine, Mfuko wa Elimu ambao umeanzishwa chini ya sheria ya Mfuko wa
Elimu, Sura ya 412 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa ukihamasisha
uchangiaji ili kuongeza nguvu za Serikali katika kugharamia miradi ya elimu.
Miradi ya Mfuko wa Elimu ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania imekuwa
ikijikita katika kuimarisha miundombinu ya taasisi za elimu ambazo zinamilikiwa
na serikali na zile zinazomilikiwa na sekta binafsi.
Hivi
karibuni, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ilitangaza kwamba, haitodahili wanafunzi
wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018
kupitia mfumo wa udahili wa pamoja ambao unafahamika kitaalam kama
“Central Admission System” badala yake wanafunzi wanapaswa kuomba nafasi za
kujiunga na chuo kwenye chuo husika moja kwa moja. Utaratibu huu mpya wa
udahili ambao ulikuwepo kipindi cha nyuma kabla ya mwaka 2010 umeleta ushindani
mkubwa kwa vyuo vikuu hasa vyuo binafsi kutokana na ukweli kwamba, vyuo vikuu
ambavyo vinamilikiwa na sekta binafsi hutegemea zaidi mapato yanayotokana na
ada ili viweze kujiendesha ikitofautishwa na vyuo vikuu ambavyo vinamilikiwa na
serikali ambavyo hupokea ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kujiendesha,
sanjari na watumishi wake kulipwa mishahara yao na serikali.
Kutokana
na changamoto hiyo, vyuo vikuu vingi hasa vinavyomilikiwa na sekta binafsi vipo
hatarini kufa au kufungwa kutokana na sababu kwamba vipo vyuo vikuu maarufu
ambavyo vitajizolea wanafunzi wengi kutokana na umaarufu wake, na vile vyuo
vikuu ambavyo ni vichanga vitapata wanafunzi wachache sana na hivyo kupelekea
kushindwa kujiendesha. Siyo kwamba vyuo vilivyopo hapa nchini vimekuwa vingi
sana la hasha! bali uhitaji wa watanzania ambao wanataka kupata elimu ya juu ni
mkubwa hasa unapolinganisha takwimu za wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo
vikuu dhidi ya takwimu za wale ambao wanaomba mikopo kutoka bodi ya mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu kama zilivyokwisha kufafanuliwa hivi punde.
Sanjari
na hilo, hali ya kiuchumi ya watanzania walio wengi inafahamika kuwa ni masikini
ambao hawawezi kugharamia elimu ya juu na kwamba; chanzo maarufu cha kufadhili
masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaosoma hapa nchini
ni kimoja na ni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo Bodi hiyo
kwa sasa imezidiwa na maombi ya wanaotaka mikopo hiyo kutokana na ukomo wa
bajeti yake jambo ambalo limeisababisha TSSF kufikiri namna ya kuwasaidia
watanzania wanaotamani kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza ilhali wamekosa
ufadhili kutoka bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na vyanzo
vingine vya ufadhili.
Ni katika
fikra hizo ambapo TSSF kwa kushirikiana na mfadhili wake anayeitwa CDF
International kutoka Seattle, Washington, Nchini Marekani imeanzisha Mfuko wa
Elimu ya Juu wa TSSF ambao utakuwa ukitoa ufadhili wa masomo ya shahada ya
kwanza kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao hawana uwezo wa kujisomesha chuo
kikuu na wamekosa ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza kutoka bodi ya mikopo
ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na vyanzo vingine vya ufadhili wa masomo ya
shahada ya kwanza.
Wanafunzi
watakaofadhiliwa na Mfuko wa Elimu ya Juu wa TSSF ni wale ambao wanasoma kwenye
vyuo vikuu vilivyopo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tu. Kwa
Mwaka huu wa 2017, TSSF kupitia mfuko wake wa elimu ya juu imeshatangaza
kupokea maombi ya ufadhili kupitia tovuti yake ya https://tssf-org-tz.weebly.com/news.html
vilevile taarifa ya kupokea maombi hayo imeshatumwa kwa vyuo vikuu vyote
nchini.
Mwanzoni
mwa Mwaka 2018 TSSF itafanya warsha kubwa
ya vyuo vikuu nchini kwa ajili ya kuanzisha mpango wa msaada wa ufadhili
wa masomo vyuoni (Financial Aid Programme) ambapo mpango huo utafadhiliwa na
Mfuko wa Elimu ya Juu wa TSSF ili kuhakikisha kwamba Mtanzania hakosi fursa ya
kujiunga na elimu ya juu kwa sababu ya kushindwa kujilipia. Mpango huo utakuwa
ni kwa vyuo vikuu vyote nchini na kila chuo kikuu kitakuwa na afisa wa dawati la
kushughulikia mpango huo. Mpango wa ufadhili wa masomo ya chuo kikuu ni mpya
kwa hapa Tanzania lakini umezoeleka katika vyuo vikuu vilivyopo nchini
Marekani, Canada, Uingereza pamoja na nchi za bara la Ulaya. Ni imani ya TSSF
kwamba, kupitia mpango huu TSSF italeta mapinduzi makubwa na kutoa mchango wake
katika kufadhili na kuwezesha elimu ya juu hapa Tanzania.
TSSF
inawaomba watanzania wote, wanafunzi wa elimu ya juu, na taasisi za elimu ya
juu kushirikiana kwa pamoja katika kufanikisha mpango huu ili vijana wetu wa
kitanzania waweze kuwezeshwa kupata elimu ya juu yenye tija, maarifa, na ujuzi
utakaowawezesha kumudu maisha yao na hatimaye kuharakisha michakato ya
upatikanaji wa maendeleo katika nchi yetu.
Aidha
tunawaomba ninyi ndugu wahariri wa vyombo vya habari pamoja wanataaluma wote wa
habari kuipa uzito taarifa hii na kutupa ushirikiano wa dhati ili vijana wetu
waweze kujiunga na kupata elimu ya juu hapa nchini. Tukumbuke kwamba ngao ya
taifa lolote ambalo limeendelea ni elimu bora iletayo maarifa na ujuzi wa
kujitambua na kumiliki mazingira ipasavyo na hivyo sisi TSSF tupo kwa ajili ya
kuwawezesha vijana wetu wa kitanzania kiuchumi ili waweze kuipata elimu hiyo itakayowawezesha
kujitambua na kumiliki mazingira yao ipasavyo na hatimaye tuweze kufikia
malengo yetu ya kuwa Taifa la Uchumi wa Viwanda.
Asanteni kwa kunisikiliza!
Imetolewa na
Donati Salla
MKURUGENZI MKUU
SHARE
No comments:
Post a Comment