Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Salome Kitomari
………………………..
George Binagi @BMGHabari
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya
Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika MISA tawi la Tanzania (MISA
Tanzania), umeonesha kwamba bado kuna changamoto kwenye upatikanaji wa
taarifa za umma katika ofisi mbalimbali za serikali nchini.
Matokeo ya utafiti huo yanaashiria
kwamba bado hakuna uwajibikaji wa moja kwa moja kwenye sheria ya Haki
ya kupata taarifa ya mwaka 2016 na pia sera ya serikali kuhimiza
matumizi ya teknolojia katika kutoa taarifa za umma.
Ripoti hiyo ya MISA Tanzania ya
mwaka 2017 ililenga kubaini ni ofisi gani ya serikali kati ya Serikali
Kuu (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa) na Serikali za Mitaa (Ofisi za Halmashauri
za Majiji na Manispaa) inatoa taarifa za umma kwa urahisi na ipi ni
kikwazo kwa utoaji wa taarifa hizo.
Utafiti huo uliodumu kwa muda wa
siku 21 ulihusisha mikoa saba ambayo ni Dodoma, Mbeya, Kigoma, Arusha,
Mwanza, Mtwara pamoja na Dar es salaam ambapo watafiti walitumia njia za
simu, barua pepe na ana kwa ana kuomba na kufuatilia taarifa katika
ofisi husika.
Maksi za chini kwenye utafiti huo
zilikuwa ni 0 na maksi za juu zilikuwa ni 20 ambapo kuliwa na dodoso
mbili za utafiti na hivyo kufanya jumla ya maksi za juu kuwa 40.
Ufafanuzi wa maksi hizo ni kwamba ofisi iliyopata maksi 0-6 inaashiria
ina usiri katika utoaji ya taarifa za umma, maksi 07-13 ni ofisi
iliyoonesha kiwango cha kawaida katika utoaji wa taarifa za umma na
maksi 13-20 ni ofisi iliyoonesha uwazi wa kutia matumaini katika utoaji
wa taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
ilipata maksi 16/40 huku Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ikipata maksi
25/40 na hivyo ofisi ya Manispaa ya Dodoma kuongoza kwa utoaji wa
taarifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya
ilipata maksi 21/40 huku ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikipata
maksi 36/40 hivyo ofisi inayotoa taarifa za umma kwa uwazi mkoani Mbeya
kuwa halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya Manispaa ya Kigoma ikipata maksi 13/40
na hivyo kufanya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa ofisi inayotoa
taarifa za umma kwa uwazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha
ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha ikipata
maksi 30/40 na hivyo kufanya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwa ofisi
inayotoa taarifa za umma kwa uwazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
ilipata maksi 09/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikipata
maksi 09/40 na hivyo kuashiria kwamba ofisi zote zina usiri kwenye
utoaji wa taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
ilipata maksi 12/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara kupata
maksi 08/40 na kuashiria kwamba ofisi zote zina usiri kwenye utoaji wa
taarifa za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam ilipata maksi 03/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es
salaa ikapata maksi 22/40 na hivyo kufanya ofisi ya Halmashauri ya Jiji
la Dar es salaam kuwa ofisi inayongoza kutoa taarifa za umma.
Utafiti huu unaashiria kwamba
asilimia kubwa ya wananchi hawanufaiki moja kwa moja na sheria ya Haki
ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 katika ofisi za umma huenda kutokana na
kutoijua vyema sheria hiyo jambo linalosababisha taarifa zenye maslahi
kwa umma kuendelea kuwa siri na wakati mwingine kuibua mkanganyiko
katika jamii.
Baadhi ya viongozi wa serikali nao
bado wanaonekana kuwa wagumu katika utoaji wa taarifa za umma huenda
kutokana na kutoitambua vyema sheria hiyo hivyo kuna kila sababu pande
zote mbili kwa maana ya viongozi na wananchi kuendelea kujengewa uwezo
ili kuitambua vyema kwa ajili ya manufaa ya jamii, kwani utoaji wa
taarifa kwa uwazi ni kichocheo cha maendeleo.
Taasisi ya MISA Tanzania inahimiza
ripoti ya utafiti huo uliotokana na mkoa mmoja mmoja kila kanda nchini,
kutumiwa na ofisi nyingine katika kujitathmini namna zinavyotoa taarifa
zake kwa umma huku ikitaka teknolojia kupewa kipaumbele ikiwemo
matumizi ya barua pepe badala ya wananchi kujazana kwenye ofisi za
serikali kufuatilia majibu kutoka kwa watumishi wa serikali na hivyo
kupoteza raslimali pesa na muda.
SHARE
No comments:
Post a Comment