TRA

TRA

Tuesday, December 29, 2015

Tuanzishe Kampeni ya Reading Books Everywhere

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



Julian Msacky
OKTOBA 15, mwaka huu nilikuwa nazungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashir Ali kuhusu umuhimu wa watu kupenda kusoma vitabu.
Wakati tukiwa katika mazungumzo yaliyotokana na makala yake aliyoandika kuhusu Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Ali alifunga mjadala wa mazungumzo kwa kusema maneno yafuatayo:
"Ahsante. Tusichoke kupiga kelele kwani kazi ya kujenga taifa haiwezi kukamilika ikiwa tutashindwa kujenga utamaduni wa kupenda kusoma vitabu na magazeti yenye maarifa na
taarifa kuhusu mapambano ya ukombozi wa taifa letu na watu wake"
Ni ukweli usiofichika kuwa kama tunataka kujenga taifa la watu wenye uelewa mpana (wide scope) wa mambo ni lazima tuhimize watoto wetu kusoma vitabu.
Lakini pia, kazi hiyo haitafanikiwa vizuri kama sisi wenyewe (wazazi na walimu) hatutakuwa na utamaduni huo.
Ili kufanikisha hilo nilimshauri Dk Ali tuanzishe Kampeni ya Reading Books Everywhere.
Hii ikiwa na maana kila tutakapokuwa tuwe na kitabu cha kujifunza jambo lolote ili kushibisha ubongo wetu maarifa ambayo yatakuwa mtaji mzuri kwa taifa letu.
Unapojenga taifa la watu wanaosoma vitabu maana yake hata shughuli wanazofanya zitakuwa na mabadiliko makubwa. Watazifanya kitaalamu zaidi.
Na hili la mwisho ni changamoto kubwa inayotukabili kama taifa. Mambo yetu mengi hayafanikiwi kwa sababu hatupendi kusoma vitabu.
Matokeo yake vichwa vyetu tunajaza mambo ya ovyo ovyo ambayo hayatusaidii. Kwa maana hiyo tukianzisha kampeni hiyo ni imani yangu taifa letu litabadilika katika mambo mengi.
Tutajenga mijadala yenye afya tunapojadili masuala muhimu yanayogusa ustawi wa nchi na watu wake. Si hivyo tu.
Hata mikataba tutakayoingia kati ya nchi wahisani itafanyika kwa uangalifu mkubwa tofauti na sasa kwa sababu bongo zetu zitafanya kazi vizuri.
Kampeni hiyo ni lazima iende pamoja na kuhakikisha shule zetu zina vitabu vya kutosha. Si bora vitabu tu, bali vikidhi viwango vya kutumiwa katika shule zetu.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha vitabu vyetu haviwachanganyi watoto au kuwaondoa kwenye reli.
Wote tunafahamu kuwa kabla ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) haijavunjika mwaka 1977, Tanzania, Uganda na Kenya walikuwa wanatumia vitabu vya aina moja.
Kulikuwa na vitabu vinafahamika kama East Africa Book One, Two, Three, Four, Five na Six. Vilikuwa vya kumjenga mwanafunzi kufahamu kwa usahihi Lugha ya Kiingereza.
Ni ukweli usiofichika kuwa watu wengi waliosoma vitabu hivyo miaka hiyo wanazungumza vizuri Kiingereza bila tatizo lolote pamoja na Kiswahili.
Kwa kusema hivi sina maana kuwa Kiswahili tukiweke pembeni hapana.
Hapa nina lengo la kuhakikisha tunasoma vitabu vya aina mbalimbali ili vitusaidie kupanua wigo wetu kama Watanzania kwa ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa kufanya hivyo maana yake mfugaji atasoma kitabu kinachohusu masuala ya ufugaji.
Akifanya hivyo kitamsaidia kufuga kisasa na kuachana na mfumo wa kienyeji ambao unasababisha hasara kubwa kuliko faida.
Hii ina maana kuwa si lazima kuwa na mifugo mingi ndipo uwe tajiri. Unaweza kuwa na ng'ombe 20 na ukafugaji kitaalamu na kupata faida lukuki na kuepuka uharibifu wa mazingira.

Ufugaji wa aina hiyo unamsaidia mfugaji kuacha kutangatanga na mifugo.Tunapofuga kitaalamu kuna faida nyingi.
Kwanza tunakuwa tumejiajiri, lakini pia tunakuwa  na kipato cha uhakika kwa ajili ya familia zetu. Mfumo huo wa ufugaji unakwenda sanjari na kulima kitaalamu.
Ilivyo sasa tunalima kwa mazao ili mradi siku ziende. Kwa maana hiyo usomaji wa vitabu utatusaidia mambo mengi. Ndiyo maana ninasisitiza kampeni hiyo.
Kwa kufanya hivyo maana yake tutakuwa na uelewa mzuri hata wa chimbuko la dini zetu (Ukristo na Uislamu) na namna gani tuziendeshe katika jamii yetu.
Jamii isiyo na maarifa ni sawa na jamii iliyo gizani. Tunataka tuondoke kwenye giza hilo kwa kusoma vitabu.
Tukisoma vitabu kwa kina ikiwa ni pamoja na kupitia katiba za mataifa mengine jamii itakuwa na upeo mpana kuandaa katiba inayokidhi kiu ya wengi.
Hata tunapokataa katiba hii na ile tutakuwa na hoja za kutosheleza badala ya kudandia hoja za wengine. Faida za kusoma vitabu ni nyingi.
Wakati ninaandika makala haya nilipofungua intaneti nilikutana na jambo linahusu mada hii ya kusoma vitabu. Nilikutana na watu waliosoma vitabu vingi kwa mwaka huu.
Wengine wamesoma vitabu 25. Miongoni mwa vitabu ambavyo Watanzania wenzetu wamefanikiwa kusoma ni pamoja na 
The truth shall make you free- Gustavo Gutiérrez.
Kwa maana Ukweli Utawaweka Huru. Sowing the mastard seed cha Yoweri Museven, The 21 Irrefutable Laws of Leadership cha John C. Maxwell, Hisa, Akiba na Uwekezaji cha Emilian Busara, YES, In My Life Time cha Profesa Haroub Othman na vingine vingi.
Kuna umuhimu wa kubadilika na kuanza kusoma vitabu ambavyo ni nyenzo muhimu kwa kizazi hiki hasa tunapozungumzia dhana ya sayansi na teknolojia.
Tusikubali kuwa maskini wa fikra. Tutafute mitaji kwa kusoma vitabu. Tuwaige wenzetu wa dunia ya kwanza ambao wakiwa wanasafiri wanatembea na vitabu.
Badala ya kupotezea fikra zetu zote kwenye Facebook, Instram, Twitter, WhatSap na mitandao mingine ya kijamii, tuvikumbuke pia vitabu ambavyo vina maarifa lukuki.
Mitandao hiyo inatudumaza kifikra na kiakili. Hebu tubadilike kwa sababu hata waasisi (founders) wa hiyo mitandao hawaipi nafasi kwa kiwango hicho.
Kama kweli walikuwa wanaipa nafasi, wasingesafiri na vitabu wanapokuwa safarini.
Wasomi na waandishi wa habari wawe mstari wa mbele kupigania kampeni hiyo ili kujenga taifa la watu wanaopenda kusoma vitabu.
Kwa kufanya hivyo ile dhana kwamba ukitaka kumficha Mtanzania jambo liweke kwenye maandishi, litakwisha kwa vile wanasoma vitabu ambavyo vina hazina ya mambo mengi mazuri.
msackyj@yahoo.co.uk, 0718981221

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger