Rais wa
Urusi, Vladmir Putin amekutana na baraza lake la usalama, siku moja
baada ya Putin kuishutumu Ukraine kwa kuchochea mzozo kwenye eneo
linalogombaniwa la Crimea, ambalo Urusi ililitwaa mwaka 2014.
Rais
Putin alikutana na maafisa waandamizi wa kijeshi pamoja na maafisa wa
kijasusi jana usiku na kutathmini upya hatua za kuchukua katika
kupambana na ugaidi kwenye eneo la mpaka, bahari na eneo la anga la
Crimea.
Rais
Putin ameahidi kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Ukraine, ambayo
ameishutumu kwa kupanga mashambulizi ya kigaidi kwenye rasi ya Crimea,
tuhuma ambazo zimekanushwa na Ukraine, ikiziita ni za uongo ambazo
zinaonekana kama njama ya Urusi kutaka kueneza uhasama zaidi.
''Nadhani
ni dhahiri kwamba maafisa wa Ukraine hawatafuti njia za kuyatatua
matatizo haya kwa mazungumzo, bali kupitia vitendo vya kigaidi. Suala
hili ni la kutisha sana,'' alisema Putin.
Hayo
yanajiri wakati ambapo Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetangaza kuwa kikosi
cha jeshi la majini cha nchi hiyo, ambacho kimeweka kambi katika Bahari
Nyeusi, Crimea, kitaanza kufanya mazoezi ya kivita kwenye eneo hilo
katika kujibu mashambulizi ya kwenye maji yatakayofanywa na wahujumu.
Ukraine katika hali ya tahadhari
Rais wa
Ukraine, Petro Poroshenko ameamuru kwamba vitengo vyote vya kijeshi
karibu na Crimea na mashariki mwa Ukraine kuwekwa katika hali ya juu ya
tahadhari, baada ya idara ya usalama ya Urusi kusema imefaulu kuyazima
mashambulizi ya kigaidi ya jeshi la Ukraine katika Bahari Nyeusi wiki
hii, shutuma ambazo zimekanushwa na serikali ya Ukraine.
Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko
Rais
Poroshenko amesema anatafuta njia ya kufanya mazungumzo ya dharura na
Rais Putin, pamoja na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Makamu wa Rais wa
Marekani, Joe Biden na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.
Wakati
huo huo, Marekani imezitolea wito Ukraine na Urusi kujiepusha na
malumbano kati yao na kuhimiza mazungumzo baina ya pande hizo mbili
yaanze tena. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Elizabeth
Trudeau, amesema nchi hiyo ina wasiwasi mkubwa na imezitaka nchi hizo
kupunguza mvutano.
Aidha,
Balozi wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa, Volodymyr Yelchenko,
amewaambia waandishi wa habari kwamba, katika kikao cha ndani cha Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ukraine imeitaka Urusi kuonyesha
ushahidi wa tuhuma dhidi yake kuhusu jaribio la mashambulizi ya kigaidi.
Katika
mkutano huo uliofanyika kwa ombi maalum la Ukraine ili kuujadili mzozo
kati yake na Urusi, Yelchenko, ameonya kuwa Urusi imepeleka zaidi ya
wanajeshi 40,000 kwenye eneo la Crimea na kwamba hatua hiyo inaweza
ikasababisha hali mbaya zaidi. DW
SHARE
No comments:
Post a Comment