Wananchi Wanatumia Vituo Vya Afya Vya Serikali Na Kusubiri Chini Ya Saa Moja Kumuona Daktari
Wananchi wengi wanatumia vituo vya afya vya serikali
na husubiri chini ya saa moja kumuona daktari
Wakati huo huo, wananchi 7 kati ya 10 wanasema changamoto
ipo katika upatikaji wa dawa na vifaa tiba
30
Agosti 2017, Dar es Salaam: Wananchi wanapopata majeraha ama kuugua, 6
kati ya 10 (61%) huenda katika kituo cha afya cha serikali. Kiwango hiki
kimeongezeka kutoka 45% mwaka 2014 na kubaki hivyo hivyo tangu mwaka
2016. Kwa kiasi kikubwa hii imesababishwa na kupungua kwa watu
wanaojitibu wenyewe kwa kwenda kwenye maduka ya dawa (9%), maduka ya
kawaida kupata dawa (7%), wasiofanya chochote (1%) au wanaotafuta aina
nyingine za matibabu (5%). Takwimu zilizokusanywa toka mwaka 2014
zinaonesha kupungua kwa matumizi ya njia hizo. Idadi ya wananchi
wanaotumia vituo binafsi, vya kanisa ama vya mashirika yasiyo ya
kiserikali haijabadilika katika kipindi hiki (16% mwaka 2017).
Pamoja
na ongezeko la idadi ya wagonjwa, utaratibu wa wananchi kusubiri kwa
saa moja ama chini ya hapo ili kumuona daktari haujabadilika toka mwaka
2014. Wananchi 7 kati ya 10 (70%) walisubiri kwa saa moja ama chini ya
hapo mwaka 2014 ukilinganisha na wananchi 3 kati ya 4 (76%) mwaka 2017.
Hata hivyo, wagonjwa husubiri kwa saa moja ama chini ya hapo katika
vituo binafsi, vya kanisa ama vya mashirika yasiyo ya kiserikali (88%
walisubiri kwa muda huu) ukilinganisha na vituo vya serikali (74%
walisubiri kwa saa moja ama chini ya hapo).
Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Afya kwanza! Wasemavyo wananchi kuhusu huduma za afya. Muhtasari unatokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika, wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo
haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,801
kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye
utafiti huu) mwezi Mei 2017.
Wananchi
wengi wanaridhishwa na usafi katika vituo vya afya. Wananchi wanaosema
hili bado ni tatizo wamepungua kutoka 29% mwaka 2015 hadi 9% mwaka 2017
na 42% walilalamikia kiwango cha kuheshimiwa na kujaliwa na wahudumu
mwaka 2015 ukilinganisha na 26% mwaka 2017.
Pamoja
na maboresho haya, wananchi wanaendelea kukumbana na changamoto kubwa
wakati wakipata huduma za afya. Wananchi watatu kati ya kumi ambao
walimsindikiza mtu hospitali mwaka uliopita (29%) walikuta wagonjwa
wawili ama zaidi wakichangia vitanda na magodoro. Kuna mabadiliko kutoka
mwaka 2016 ambapo karibu wananchi 4 kati ya 10 (36%) walishuhudia
wagonjwa wakichangia vitanda/magodoro.
Inatia
mashaka zaidi linapokuja suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Toka mwaka 2015, kumekuwa na ongezeko la wananchi waliokutana na
upungufu wa dawa/vifaa tiba mara ya mwisho walipoenda katika kituo cha
afya cha serikali. Vilevile, kuna ongezeko la wananchi ambao
wanalalamikia muda wa kusubiri, kutoka 53% mwaka 2015 hadi 63% mwaka
2017.
Linapokuja
suala la upatikanaji wa madaktari na gharama za huduma, idadi ya
wananchi waliokuwa wanalalamikia masuala haya walipungua kati ya mwaka
2015 na 2016, lakini idadi imeongezeka tena mwaka 2017.
·
Ukosefu wa madaktari lilikuwa ni tatizo kwa 43% mwaka 2015, likashuka
mpaka 18% mwaka 2016 na kupanda mpaka 29% mwaka 2017.
· Gharama za huduma ilikuwa ni tatizo kwa wananchi 34% mwaka 2015, 19% mwaka 2016 na 28% mwaka 2017.
Twaweza pia iliwauliza wananchi iwapo sera ya serikali inatekelezwa kwa uzoefu wao,
·
Watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wazee na wajawazito wanapaswa
kupata matibabu bure katika vituo vya afya vya serikali. Tangu mwaka
2016 kumekuwa na ongezeko dogo la idadi ya watu kutoka kwenye makundi
hayo wanaopata huduma za matibabu bila malipo lakini wengi wao
wanalazimishwa kulipa. Miongoni mwa wananchi waliowasindikiza watoto,
wajawazito na wazee, 35% walilazimika kulipia matibabu ya mtoto, 28% ya
wajawazito na 37% ya wazee.
·
Pamoja na kauli za serikali na wananchi 84% kuwa waathirika wa ajali,
ugomvi au majeraha watibiwe kabla ya kupata kibali kutoka polisi,
wananchi 6 kati ya 10 waliowasindikiza waathirika hao ili kupata
matibabu walitakiwa kupata kibali cha polisi kabla ya kupata matibabu.
·
Bima, hususani kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa, ni mkakati
mkubwa wa serikali wa kupanua upatikanaji wa huduma za afya. Kati ya
mwaka 2014 na 2017 idadi ya watu wenye bima ya afya imeongezeka kutoka
21% hadi 27%. Kwa ujumla, 13% ya wananchi wanasema ni wanachama wa Mfuko
wa Afya ya Jamii (ulioboreshwa). Kwa kiwango cha ongezeko la sasa,
Tanzania huenda ikafikia kiwango cha kimataifa cha wananchi wake
kufikiwa na bima ya afya ndani ya miaka 40 ijayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze, anasema: “Tunaweza
kuyafurahia baadhi ya matokeo haya. Wananchi wanatumia zaidi vituo vya
afya vya serikali na baadhi ya masuala katika utoaji wa huduma za afya
yameboreshwa. Lakini tatizo la dawa na vifaa tiba, sambamba na uchache
wa watendaji wa afya, bado ni tatizo kubwa.”
“Jambo
lingine linalotia mashaka,” anaendelea “ni namna ambavyo sera ya
serikali inapuuzwa na watoa huduma za afya. Kwani pamoja na kauli kali
za serikali na kampeni za kuelimisha umma, huduma bure ya afya haitolewi
ipasavyo kwa makundi ya wananchi wanaostahili huduma bure. Lazima
tuendelee kufuatilia na kukumbushana kuwa utamaduni wa uwajibikaji ni
kiungo muhimu sana kwa maendeleo ya sekta yetu ya afya.”
SHARE
No comments:
Post a Comment