Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga, wakati
alipotembelea Mfuko huo, jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga, akifafanua jambo kwa
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani,
namna Mfuko huo unavyohakikisha mawasiliano ya simu na data unapatikana
hususan vijijini, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watendaji wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani), wakati
alipowatembelea na kuzungumza nao changamoto na namna ya kufanikisha
malengo ya Mfuko huo, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA), kuhusu uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini
leo, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA), Bw. Salim Msangi akitoa taarifa ya utendaji wa
Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani, wakati alipokuwa akizungumza nao leo, jijini Dar es
Salaam.
………………….
Serikali imeutaka Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), kuona namna ya kuboresha huduma za
mawasiliano ya simu na data vijijini ili kuwawezesha wananchi kufikiwa
na huduma hiyo kwa urahisi.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika ofisi za Mfuko huo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amesisitiza kwa Mfuko huo
kuhakikisha unafikisha mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa na
huduma hiyo kabisa lengo likiwa ni kufanya usawa na kuwezesha vijiji
vyote kufikiwa na huduma hiyo.
“Hakikisheni mnapeleka mawasiliano
katika vijiji ambavyo hakuna mawasiliano kabisa kwani wananchi wamekuwa
wakilalamika kutofikiwa na huduma”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Aidha, ameutaka Mfuko huo
kuwasimamia watoa huduma nchini kuhakikisha wanafunga minara na mitambo
sahihi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuepusha usumbufu kwa
wananchi.
Ameutaka Mfuko huo kushirikiana na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara ili kuhakikisha maeneo ambayo watoa huduma wamejenga minara
yanakuwa ni ya uhakika.
Ameongeza kuwa Mfuko huo una
wajibu wa kutafuta vifaa vingine vitakavyowawezesha kusaidia kufanya
ukaguzi kwa haraka badala ya kukaa na kusubiri vifaa vya TCRA.
Ametoa rai kwa makampuni ya simu
nchini hususan yanayochangamkia zabuni za Serikali kupitia mfuko huo
kutoa taarifa sahihi za usimikaji wa minara na utendaji wake kwa mfuko
huo ili kusaidia kuboresha mawasiliano vijijini kwa nia moja.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Eng. Peter Ulanga,
amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa wataendelea kuwasimamia watoa
huduma nchini kuhakikisha wanajenga minara na kuhakikisha inafanya kazi
masaa yote.Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ngonyani ametembelea Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), na kuwasisitiza kuwajibika katika kuongeza mapato na kuendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini ili kukuza sekta ya usafiri wa anga.
Naibu Waziri ameendelea na ziara
yake ya kikazi jijini Dar es Salaam ambapo ametembelea na kuzungumza na
uongozi wa UCSAF na TAA.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
SHARE
No comments:
Post a Comment