,Hamza Temba, Lushoto
Katika
kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha
utalii wa Misitu ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la
taifa tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.
Hayo
yamesemwa jana wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani
humo kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali ya uhifadhi.
Alisema
sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau
vivutio
vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe
hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.
“Tumezoea
zaidi utalii wa wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa
wanyamapori, kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na
viumbe hai mbali mbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa
kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata
watalii wengi zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.
Kwa
mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina
jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na
hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa
fursa pana ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akiteta jambo na Mkuu
wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti Lugangika katika kijiji cha Shume Nywelo
wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
(Picha na Hamza Temba – Wizara ya
Maliasili na Utalii)
Akizungumzia
mafanikio, Makani alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa
na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema pamoja na faida hizo,
sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu
ya asili ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.
“Ni
lazima tutafute njia endelevu ya ulinzi wa misitu, hatuwezi kuwa na askari wa
kutosha, walinzi na mitutu, njia sahihi ni ulinzi shirikishi, tuwaelimishe
wananchi umuhimu wa misitu na tuwaeleze watanufaikaje, tofauti na zile faida za
ujumla za upatikanaji wa mvua na hali nzuri ya hewa, hii itasaidia sana kuwaleta
karibu kwenye uhifadhi wa pamoja”, alisema Makani.
Akizungumza
na wananchi wa kijiji Nywelo wilayani humo kuhusu mgogoro wa mpaka
baina ya kijiji hicho na shamba la miti Shume, Makani alisema tatizo
lililopo ni uelewa tofauti kuhusu mpaka huo baina ya pande hizo mbili,
hivyo akuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
kutuma wataalamu wa upimaji waliopima eneo hilo awali waje wafanye
uhakiki wa mpaka huo kwa kushirikisha uongozi wa wilaya, halmashauri na
kijiji hicho ili kuondoa tofauti hizo na kumaliza mgogoro huo ndani ya
wiki mbili zijazo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika alisema wilaya yake
inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji
wa miti ya asili, uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto
misitu na uhaba wa watumishi.
Katika
ziara yake hiyo wilayani Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea
Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na Shamba la Miti la Shume, alifanya
pia vikao vinne vya ndani na mkutano mmoja wa hadhara ambapo alijibu
kero mbalimbali za wananchi.
SHARE
No comments:
Post a Comment