Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Suleiman Jaffo akiongea na wajumbe wa Mkutano wa Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika kutoka Tanzania na Afrika Kusini walipokuwa
ziarani Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa
Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia ni Katibu Mkuu Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mawasiliano Serikalini Bi. Plumla Williams akitoa neno kwa niaba ya
wajumbe kutoka Afrika Kusini walipotembelea maeneo ya ukombozi yaliyopo
Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya agenda ya Mkutano
kuhusu utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Suleiman Jaffo (wa pili kushoto) akisalimiana na
Mkurungenzi Mkuu wa Kazi za Umma kutoka Afrika Kusini Bw. Mziwonke
Dlabantu (kulia). Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe.
Deogratius Ndejembi.
Baadhi ya Viongozi kutoka Afrika
Kusini wakiangalia makaburi ya Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini yaliopo
Wilayani Kongwa, Dodoma.
Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
…………………
Na Bearice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Suleiman Jaffo amesema kuwa Programu ya Urithi wa Ukombozi
wa Bara la Afrika (ALHP) una historia adhim kati ya Tanzania na Afrika
Kusini na itasaidia kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Mhe. Jaffo ameyasema hayo leo
Wilayani Kongwa, Dodoma wakati wa ziara ya Makatibu Wakuu, Wakurugenzi
na Watalamu wa Programu hiyo kutoka Tanzania na Afrika Kusini kujionea
maeneo yaliyotumika wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika
Kusini.
“Nchi ya Tanzania na Afrika Kusini
zina urafiki mkubwa na wa karibu kuliko nchi nyingine yeyote Afrika,
hivyo kupitia Programu hii tutazidi kuimarisha udugu na uhusiano uliopo”
amefafanua Mhe. Jaffo.
Ziara hiyo ilihusisha maeneo ya
makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini, Kambi walipokuwa wanaishi,
mahandaki walipokuwa wanajihifadhi dhidi ya maadui pamoja na madarasa
yaliyotumika kwa ajili ya mafunzo kwa wapigania uhuru.
Akizungumzia ziara hiyo Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuona maeneo yaliyotumika
wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika Kusini na kujadili
jinsi ya kutunza maeneo hayo kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi
vijavyo.
Aidha, Prof. Elisante ameongeza
kuwa ziara hiyo ina umuhimu kwa nchi zote ikizingatiwa Tanzania ndio
ilikuwa kinara wakati wote wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika
hatua inayopelekea kuthamini mchango uliotolewa na Tanzania kwa kusaidia
kwa hali na mali katika ukombozi wa wananchi wa Afrika Kusini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa viongozi waliokuwepo
katika ziara hiyo kutoka Afrika Kusini kuona umuhimu wa maeneo hayo ya
kumbukumbu ya historia ya nchi yao kwa kuyatunza na kuyaendeleza kwa
ajili ya vizazi vijavyo ili watambue mchango wa Watanzania katika
Ukombozi wa Bara la Afrika.
Akiongea kwa niaba ya viongozi
kutoka Afrika Kusini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Serikalini
Plumla Williams ameametoa wito kwa Serikali zote mbili kuwa suala la
Ukombozi wa Afrika lifundhishwe shuleni ili kuweza kutunza na kuimarisha
Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.
Mbali na hayo Bi. Plumla kwa niaba
ya Serikali ya Afrika Kusini ameahidi kuwa wataendeleza kasi ya
utekelezaji wa programu hiyo ili uweze kuwa na tija kwa pande zote
mbili.
Programu ya Urithi wa Ukombozi wa
Bara la Afrika ina wajibu wa kukusanya, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na
kukumbuka nakishi ya Urithi wa Afrika tangu harakati za kupigania Uhuru
wa Afrika hadi Bara zima lililokombolewa.
SHARE
No comments:
Post a Comment