RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi
aliyewahi kuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mpwapwa Mkoani
Dodoma Bw. Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa
familia yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea nchini
Uganda.
Watu hao wamefariki dunia baada ya
basi walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana
na lori jana tarehe 17 Septemba, 2017 majira ya saa 4:00 Usiku katika
barabara ya Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea Tanzania.
“Nimepokea taarifa ya vifo hivi
kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya
watu, nampa pole Ndg. Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa,
nawapa pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi.
“Nawaombea marehemu wote
wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata
matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani” amesema
Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka
wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu
katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu
waliowategemea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Septemba, 2017
SHARE
No comments:
Post a Comment