Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga
Bw. Charles Maugila akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa Dreams
Innovation Challenge wilayani humo.
Baadhi ya wasichana na wanawake wadogo watakaofikiwa na mradi katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wilayani Kahama.
…………………
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la IDLO kimezindua
mradi wa Kuwajengea Uwezo wa Kisheria Wasichana na Wanawake Wadogo
mkoani Shinyanga ili Kuweza Kuiwajibisha Jamii Kutoa Huduma Bora za Afya
ya UKIMWI.
Katika uzinduzi wa mradi huo
uliofanyika Septemba 14 katika manispaa ya Shinyanga na Septemba 15
katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, makundi lengwa ya mradi huo ikiwemo
wasichana na wanawake wadogo, wazazi, viongozi wa serikali na Jamii kwa
ujumla yameonyesha kuvutiwa na malengo na matokeo tarajiwa ya mradi
huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga wakati wa kuzindua mradi huo Afisa Tawala wilaya ya
Shinyanga Bw. Charles Maugila amesema ujio wa mradi huo katika Manispaa
ya Shinyanga ni wa kufurahiwa kwani mkoa wa Shinyanga kwa ujumla
unakabiliwa na changamoto kubwa ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa
kijinsia na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hususani kwa wasichana na
wanawake wadogo. “Kumekuwa na miradi mingi inayolenga kukabiliana na
ukatili wa kijinsia na UKIMWI lakini mradi huu ni wa kipekee kwa vile
unalenga kuwajengea uwezo wa kisheria wasichana na wanawake wadogo ambao
ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia na maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI waweze kuwajibisha jamii kwa kudai huduma bora za afya ya
UKIMWI” Alisema Maugila.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Kahama, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bw. Anthony Ndanya ameitaka Jamii
ya Kahama kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika utekelezaji
wa mradi huo ili kuweza kufikia malengo ya mradi huo na kupata matoke
tarajiwa.
Akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa Fedha
na Utawala, Bw. Ezekiel Massanja alisema “kwa mujibu wa Ripoti ya Haki
za Binadamu Tanzania 2016, ukatili wa kijinsia ukijumuisha ukatili wa
majumbani, ukatili wa kingono, mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja
na vitendo vingine vya kikatili kwa watoto na wanawake vimezidi
kuongezeka maradufu mbali na kuwepo kwa sheria zinazolinda kundi hilo.
Moja ya matokeo ya changamoto za ukatili kwa wanawake ni kuambukizwa
virusi vya UKIMWI”.
“Sambamba na ongezeko la vitendo
vya kikatili, Jamii inakosa uwezo wa kuwawajibisha watekelezaji wa
vitendo vya kikatili na kushindwa kukabilianan na madhara ya ukatili wa
kijinsia kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na namna ya kudai
upatikanaji wa huduma bora za afya” – Aliongeza Massanja.
Mradi huu ni moja ya miradi mingi
ya Dreams Innovation Challenge inayotekelezwa nchini. Mradi umejikita
kuwajengea uwezo wasichana wa miaka 15 hadi 24 na jamii kwa ujumla juu
ya masula ya kisheria, afya na ukatili wa kijinsia. Mradi unalenga
kuwapa uwezo wasichana kuiwajibisha jamii pale haki zao za msingi
zinapokosekana hasa kwenye masuala ya afya ya UKIMWI.
Lengo kuu la mradi ni kuimarisha
uwezo wa jamii kuboresha huduma za afya ya UKIMWI kwa wasichana na
wanawake wadogo kupitia mbinu ya uwezeshaji kisheria na uwajibikaji
kijamii.
Mradi unalenga kufikia jumla ya
wasichana 1000 wenye umri kati ya miaka 15 – 24. Wasichana 500 Shinyanga
na 500 wilayani Kahama. Wanufaika wengine ni pamoja na wanaume ambao ni
wapenzi wa wasichana hao, wazazi, watoto, vyombo vya sheria, wahudumu
afya pamoja na jamii yote kwa ujumla.
SHARE
No comments:
Post a Comment