Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa
Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania
(CHAMAUMAVITA) Bw. Hilally Said (katikati), akisisitiza jambo mbele ya
Waaandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya maadhimisho ya Watoto wenye
Mtindio wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6 oktoba mwaka huu leo jijini
Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa CHAMAUMAVITA Taifa, Bi. Mwanahamis
Hussein, na Mweka Hazina wa CHAMAUMAVITA Taifa Bi. Jane Kim.
Katibu wa Chama cha Wazazi wa
Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania
(CHAMAUMAVITA) Taifa, Bi. Mwanahamis Hussein (katikati) akizungumza
mbele ya waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya maadhimisho ya
watoto wenye Mtindio wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6, Oktoba mwaka
huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa CHAMAUMAVITA Bw.
Hilali Said na Mweka Hazina wa CHAMAUMAVITA Taifa Bi. Jane Kim.
Mweka Hazina wa Chama cha Wazazi
wa Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania
(CHAMAUMAVITA), Bi. Jane Kim akielezea maadhimisho ya Watoto wenye
Mtindio wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6, Oktoba mwaka huu mbele ya
Waandishi wa Habari (hawapo pichani, Kushoto ni Mwenyekiti wa
CHAMAUMAVITA Bw. Hilali Said.
Picha zote na: Thobias Robert, MAELEZO
………………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chama cha Wazazi na Watoto wenye
Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo,Akili na Viungo Tanzania (CHAWAUMAVITA)
kitafanya maadhimisho ya siku ya mtindio wa ubongo duniani kwa lengo la
kuipa jamii uelewa juu ya changamoto wanazozipata watoto wenye matatizo
hayo na kuwaleta pamoja familia zinazolea watoto hao ili wabadilishane
uzoefu.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na mwenyekiti wa chama hicho, Hilali Said alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.
“Kwa kawaida Siku ya Mtindio wa
Ubongo duniani huadhimishwa kila Jumatano ya kwanza ya mwezi Oktoba
lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa tarehe 6, ambapo yanategemewa
kufanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mjimwema vilivyopo wilaya
ya Kigamboni na tunategemea mgeni rasmi wa maadhimisho hayo atakuwa
Mkuu wa Wilaya hiyo”, alisema Said.
Said ameongeza kuwa nchi
mbalimbali Duniani huadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu ya ulemavu wa
aina hiyo kwa wananchi ili kupunguza athari zinazojitokeza kwa wazazi na
watoto wenyewe pamoja na kuwasaidia wanachama kutetea na kupata haki
zao kwa mujibu wa sheria.
Ameelezea mambo sita ambayo
yamegundulika kuwa ni changamoto zitokanazo na matatizo hayo duniani
kuwa ni fursa za matibabu kwa watoto hao, ukosefu wa dawa, ufahamu mdogo
kwa jamii, ukosefu wa elimu, hali halisi ya kimaisha pamoja na mchango
wao katika nchi kama binadamu wengine.
Aidha, Said amefafanua kuwa chama
hicho kwa sasa kinafanya kazi Jijini Dar es Salaam pekee ambapo kuna
jumla ya vituo kumi vinavyowasaidia watoto wenye matatizo hayo kupata
huduma ya mazoezi ya viungo vilivyoathirika mara moja kwa wiki.
Alivitaja vituo hivyo kuwa vipo katika manispaa za Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Ubungo na Temeke jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake mweka hazina wa
chama hicho, Jane Kim ameiomba Serikali kuwasaidia watoto hao kwa
kuwapatia mazingira mazuri ya kusomea pamoja na walimu wa kutosha wenye
elimu stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapatia ulinzi wa kutosha wanapokuwa
shuleni ili nao waweze kupata elimu na kutimiza ndoto zao kama watoto
wengine.
“Watoto wenye mtindio wa ubongo
wana haki sawa na watoto wengine hivyo wanatakiwa kupata haki zote
wanazopatiwa watoto wasio na tatizo hilo zikiwemo za mazingira mazuri ya
kusomea pamoja na viwanja vya michezo vinavyolingana na hali
zao”,alisema Jane.
Chama hicho cha kilisajiliwa
mwezi Machi, 2013 kupitia Msajili wa Vyama vya Kiraia, Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi na kinawahusisha na wazazi wenye watoto walio na
mtindio wa ubongo ambao wanafanya mazoezi tiba katika vituo vilivyopo
Jijini Dar es Salaam.
SHARE
No comments:
Post a Comment