TRA

TRA

Wednesday, September 6, 2017

Umoja wa Ulaya wadai nafasi kamili kuwafikia Wahingya

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Umoja wa Ulaya unadai nafasi kamili kuwafikia Warohingya Waislamu wanaoteseka kufuatia ghasia zilizotokea Myanmar tangu wiki iliyopita. Rais Erdogan asema masaibu ya Warohingya Myanmar yamewaghadhabisha Waislamu duniani
Umoja wa Ulaya unadai nafasi kamili ili kuwafikia Warohingya Waislamu wanaoteseka kufuatia ghasia zilizotokea Myanmar tangu wiki iliyopita. Umoja huo umeitaka Myanmar kumaliza ukiukaji wa haki za binaadamu unaoendelea dhidi ya jamii hiyo ndogo. Wakati huo huo Malaysia imemuita balozi wa Myanmar nchini mwake kumuarifu kutoridhishwa kwa Malaysia na ghasia katika jimbo la Rakhine ambazo zimesababisha takriban watu 125, 000 wengi wao wakiwa waislamu wa jamii ya Warohingya kuyakimbia makaazi yao. 
Kamishna wa Halmashauri kuu ya  Umoja wa Ulaya Christos Stylianides amesema leo kuwa wengi wa Warohingya wanateseka kwa sababu  ya kuikimbia nchi hiyo. Kufuatia idadi kubwa ya Warohingya ambao wametoroka Myanmar, huduma za misaada zinazotolewa na Bangladesh zimelemewa huku kambi za wakimbizi hao zikijaa kupindukia.
Misaada kwa Bangladesh kuwasaidia wakimbizi
Waandamanaji New Delhi wakikupinga mateso dhidi ya Warohingya wa Myanmar Waandamanaji New Delhi wakikupinga mateso dhidi ya Warohingya wa Myanmar
Stylianides amesema juhudi za Umoja wa Ulaya kuwasaidia maafisa wa Bangladesh kuwapa wakimbizi hao usalama na misaada mingine itaendelea hadi watakaporudi makwao. Catherine Ray ambaye ni msemaji wa idara ya mambo ya nje, usalama na sera za Umoja wa Ulaya amesema wataendelea kushirikiana na Bangladesh kutoa misaada.
Bibi Catherine anaendelea kusema "Ninatumai taarifa yetu inaeleweka kuwa hakika hali ni mbaya na tunafaa kuchukua hatua muhimu, na ndiyo sababu kamishna Stylianides ametoa taarifa hiyo yenye uzito. Na tutaendelea kuzungumza na maafisa kuhakikisha tunapata nafasi kamili  kufikisha misaada ya kibinadamu inayotolewa."
Waziri wa mambo ya nje wa Malaysia Anifah Aman amesema machafuko ya hivi karibuni yameonesha kuwa serikali ya Myanmar haijafanya lolote au imechukua hatua ndogo sana katika juhudi za kutafuta suluhisho la amani kwa matatizo yanayoikumba jamii ndogo ya Rohingya, inayoishi Kaskazini Magharibi karibu na mpaka wa Bangladesh. Balozi wa Myanmar ametakiwa kujiwasilisha mbele ya serikali ya Malaysia ambapo ataelezewa kutoridhishwa kwa Malaysia na ghasia katika jimbo la Rakhine.
Masaibu ya Warohingya yaibua ghadhabu
Mkutano wa Waislamu wa Grozny Akhmat kuonesha umoja na wenzao wa Myanmar Mkutano wa Waislamu wa Grozny Akhmat kuonesha umoja na wenzao wa Myanmar
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ambaye amesema kuwa machafuko dhidi ya Waislamu Warohingya  ni sawa na mauaji ya kimbari, amemwambia rais wa Myanmar Suu Kyi kuwa ghasia hizo zinasababisha wasiwasi mwingi kwa Waislamu duniani kote na kuwa anamtuma waziri wake wa mambo ya nje kwenda  Bangladesh kuzungumzia hali hiyo.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi naye anaanza ziara yake leo nchini Myanmar ambapo atakutana na maafisa wakuu akiwemo kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi
Kwa upande mwengine Pakistan , imeelezea masikitiko yake kuhusu masaibu yanayowakumba Warohingya wa Myanmar.
Kulingana na takwimu za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, Warohingya 123, 600 wameikimbia Myanmar tangu tarehe 25 Agosti na  kuingia Bangladesh.
Mapigano haya ya hivi karibuni yalianza wiki iliyopita pale wanamgambo wa Rohingya walipofanya misururu ya mashambulizi katika kambi za walinda usalama wa Myanmar. Inakadiriwa kuwa jumla ya watu 400 wameuawa, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Rohingya. Kadhalika askari wa  usalama wa Myanmar wameripotiwa kuviteketeza  kwa moto vijiji vya Warohingya.

CHANZO: DW

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger