Daktari Bingwa wa Magonjwa Moyo
kwa Watoto Dkt.Naiz Majani akielezea umuhimu wa akina mama wajawazito
kufanya kipimo cha‘Fetal Echocardiography’ katika mahojiano maalum na
mwandishi wa habari hii mapema hivi karibuni. Kipimo hicho ni maalum kwa
ajili ya kupima wajazito ili kubaini kama watoto waliotumboni wana
ugonjwa wa moyo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa Moyo
kwa Watoto Dkt.Naiz Majani akielezea umuhimu wa akina mama wajawazito
kufanya kipimo cha‘Fetal Echocardiography’ katika mahojiano maalum na
waandishi wa habari mapema hivi karibuni. Kipimo hicho ni maalum kwa
ajili ya kupima wajazito ili kubaini kama watoto waliotumboni wana
ugonjwa wa moyo.
Picha na Idara ya Habari (MAELEZO)
……………………………………………………………………………
Na Agness Moshi -MAELEZO.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
imewashauri wajawazito walio kwenye hatari ya kujifungua watoto wenye
magonjwa ya moyo kufanya kipimo cha‘Fetal Echocardiography’ ili waweze
kugundua tatizo mapema na kulipatia tiba.
Akiongea na waandishi wa habari
katika mahojiano maalum,Daktari Bingwa wa Magonjwa Moyo kwa Watoto
Dkt.Naiz Majani amesema ni vyema wajawazito walio kwenye hatari ya
kujifungua watoto wenye magonjwa ya moyo kuhakikisha wanafanya kipimo
hicho mapema ili kujua hali ya mtoto tumboni kufanya kipimo cha
magonjwa hayo ili kuweza kugundua tatizo mapema na kujiandaa
kukabiliana nalo.
Dkt.Naiz alitaja baadhi ya
wajawazito walio kwenye hatari ambao ni pamoja na waliowahi kuzaa mtoto
mwenye tatizo la moyo,wanaotumia dawa za muda mrefu kama vile dawa za
kifafa,wenye mimba ya mapacha ,wanaougua ugonjwa wa kisukari, wenye
mgonjwa wa moyo kwenye familia zao au ambao kwenye vipimo walivyofanya
wamekuta mtoto anatatizo lolote.
“Magonjwa mengi ya moyo ya
kuzaliwa yanatibika lakini yanasharti kubwa la kujulikana mapema na
yanahitaji tiba kwa wakati muafaka, inaumiza sana unapogundua mtoto
anatatizo la moyo halafu unamwambia hatuwezi kufanya upasuaji kwa sababu
tu amechelewa”, alisema Dkt.Naiz.
Dkt.Naiz alisema kuwa kuna wakati
mtoto anagundulika na tatizo lakini anashindwa kufanyiwa upasuaji si
kwasababu hakuna tiba bali kwasababu amefika kliniki ya moyo kwa wakati
usiosahihi kwa upasuaji, hivyo ni vyema kwa mjamzito kuwahi kufanya
kipimo ili aweze kumsaidia mtoto kupata tiba kwa wakati.
“ Kuna magonjwa ya moyo
yanatakiwa yatibiwe ndani ya mwezi baada ya kuzaliwa,mengine ndani ya
miezi sita au mwaka mmoja inategemea na tatizo alilonalo mtoto, hivyo
kwa kufanya kipimo cha Fetal Echocardiography tutaweza kugundua tatizo
la mtoto mapema angali akiwa tumboni mwa mama na kujiandaa na matibabu
kwa muda muafaka”,alisema Dkt.Naiz.
Aidha, Dkt.Naiz amesema kuwa
kipimo hicho ni salama kwa mama na mtoto kwasababu hakina mionzi ambayo
ingeleta madhara na kinafanya kazi kwa mimba ya umri wowote japo
inapendeza zaidi mimba ifikishe walau miezi minne hadi saba kwa
sababu kwa wakati huo tatizo linaonekana vizuri.
“Kipimo cha Fetal
Echocardiography ni ‘ultrasound ‘ ambayo inapima magonjwa ya moyo kwa
mtoto aliye tumboni hivyo wajawazito wasiwe na wasiwasi wowote kwa
sababu hakina utofauti na ultrasound aanazofanya wakati wa
ujazito”,alisisitiza Dkt.Naiz.
Hata hivyo, Dkt.Naiz amesema si
lazima mjamzito mwenye hatari ya kujifungua mtoto mwenye ugonjwa wa moyo
ndio anatakiwa apime hata wasio kwenye hatari wanakaribishwa kufanya
kipimo hicho kwa tahadhari kwani tafiti zinaonyesha mtoto mmoja kati
ya 100 huzaliwa na ugonjwa wa Moyo hivyo ni vyema kujua hali ya mtoto
mapema kwasababu mtoto wa yeyote anaweza kuzaliwa na tatizo.
Kwa sasa ,huduma hii inapatikana
kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pekee na tayari
wajawazito 35 wamefanyiwa ambapo watano kati yao wamegundulika na
tatizo na tayari maandalizi ya matibabu yao yameanza.
SHARE
No comments:
Post a Comment