Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefunguka na kudai amerudi nchini
akiwa na unyenyekevu mkubwa zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri
alioonyeshwa na Mbunge Tundu Lissu pindi alipokwenda kumjulia hali
katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Zitto ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa facebook asubuhi ya leo na
kusema japo Lissu ameumizwa sana lakini hakuacha kumuonyesha ucheshi
licha ya kuwa na maumivu makali aliyokuwa nayo katika mwili wake.
"Siku mbili hizi nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa mawazo sana,
nimerudi nchini nikiwa kwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na
ujasiri ambao ndugu yangu amenionesha licha ya kuwa kwenye maumivu
makali. Siyo mara nyingi hapa nchini kusikia tukiongelea ujasiri lakini
namfikiria lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi,
najua hivyo ndivyo alivyo", ameandika Zitto.
Pamoja na hayo, Zitto ameendelea kwa kusema "waliomshambulia wamemuumiza
kweli na bado wakati tuliokuwa naye amenionesha shukrani, ari na pia
ucheshi. Huo ni ujasiri, alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu siyo
kitu rahisi kwa mtu yeyote kutafakari. Kufikiria hali ile kungeniacha
niumie moyo kama asingesema maneno haya kwangu kuwa 'tumeshinda.
Tumeshashinda", amesisitiza Zitto.
Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana
Septemba 7, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye
kusafirishwa kwenda jijini Nairobi Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu
kufuatia majeraha aliyopata, ambapo mpaka sasa yuko huko kwa matibabu.
SHARE
No comments:
Post a Comment