TRA

TRA

Tuesday, October 24, 2017

RAIS MAGUFULI AWATUNUKU VYETI WAJUMBE WA KAMATI ZA MADINI

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewatunuku vyeti wajumbe wa Kamati za Madini jana Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni shukrani kwa kazi ya kizalendo waliyoifanya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amesema kuwa watu hao wamefanya kazi kubwa na ya kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya watanzania hivyo wanastahili pongezi.
“Ninashukuru sana kwa kweli mmetengeneza ukurasa wa pekee kwani kazi mliyoifanya ni ya kujitoa sadaka,”alisema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa watanzania wengi wanaunga mkono juhudi hizi za kulinda raslimali za taifa licha ya kuwepo watu wachache wanaobeza jitihada hizo na kusema hao inabidi wapuuzwe.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa wameonyesha uzalendo kwa taifa ambalo lina raslimali nyingi lakini lilikuwa halifaidiki nazo bali zilikuwa zikiwafaidisha watu wachache.
Rais amesema kuwa katika suala la kutetea na kulinda raslimali za nchi hasa madini, hakuna hata mahakama ambayo ingeinyima Serikali ya Tanzania ushindi kwani unyonyaji uliokuwa ukifanyika ulikuwa wa wazi, hivyo ameipongeza Kamati ya majadiliano chini ya Mwenyekiti wake, Prof. Paramagamba Kabudi.
Amewataka watanzania kuwa na moyo wa kizalendo kwa kujali na kulinda raslimali za nchi bila kuangalia manufaa yao binafsi.
“Ningekuwa na ubinafsi mii ningekeuwa tajiri sana kwani nimefanya kazi katika Wizara ya Ujenzi kwa miaka 16, hivyo ningetaka kujitajirisha ningeweza, lakini hivyo vyote vya nini,” aliuliza Rais Magufuli.
Katika makubaliano kati ya Tanzania na Barrick Gold Company Limited, mgawanyo wa faida itokanayo na madini utakuwa 50 kwa 50, jambo ambalo halifanyiki katika nchi yoyote ya Kiafrika, aliongeza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya majadiliano upande wa Tanzania, Prof. Paramagamba Kabudi amesema kuwa Rais Magufuli anapaswa kupongezwa kwa msimamo wake katika suala zima la usimamizi wa raslimali za nchi hasa madini.
Prof. Kabudi amenukuu magazeti ya Zambia jinsi yalivyompongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo. Amesema kuwa hakika nabii hakubaliki kwao, nje ya nchi wanampongeza Rais wakati baadhi ya watanzania wanabeza jitihada hizo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amempongeza Rais magufuli kwa hatua anazozichukua katika kulinda raslimali za nchi na kuwataka wapinzani wenzie kumuuunga mkono.
“Mhe. Rais shikilia hapo hapo ili raslimali zetu ziweze kulindwa na kutunufaisha watanzania wote,”alisema Prof. Lipumba.
Baadhi ya waliotunukiwa vyeti hivyo ni Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, Prof. Paramagamba Kabudi, Prof. Abdulkadir Mruma, Prof. Nehemiah Ossolo, James Dotto, Dkt. Yamungu Kayandabila, Prof. Lwoga, Andrew Massawe, Prof. Rwezaula Ikingula, Dr. Ambrose Joseph na Prof. Longinus Lutasitara.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mawaziri, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya Siasa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Wanahabari, na wageni wengine ambao walionyesha kufurahishwa na hatua za Serikali ya Awamu ya Tano katika kulinda raslimali za nchi.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mke wa Spika Bibi. Fatma Ndugai kwa niaba ya Spika Job Ndugai ikiwa ni cheti cha utambuzi wa mchango wake katika kusimamia rasilimali za nchi hasa madini katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. Katika ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika kusimamia rasilimali za nchi mjumbe wa kamati zilizoshughulikia masuala ya Makinikia Bibi. Monica Philip wakati wa  hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia jana Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika kusimamia rasilimali za nchi Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia Ikulu Jijini Dar es Salaam. Katika ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi. Profesa Kabudi alikuwa Mwenyekiti wa majadiliano kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika kusimamia rasilimali za nchi aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kwanza ya Makinikia Profesa Abdulkarim Mruma katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia Ikulu Jijini Dar es Salaam. Katika ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika kusimamia rasilimali za nchi mjumbe wa kamati zilizoshughulikia masuala ya Makinikia ambaye pia ameteuliwa kuwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) Profesa Florens Luoga  wakati wa  hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) aliyeteuliwa  leo kushika wadifa huo Profesa Florens Luoga akisalimiana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Juma Zuberi katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia  Ikulu Jijini Dar es Salaam. Nyuma ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi William Lukuvi akisalimiana na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Mussa Salum.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Haruna Lipumba  walipokutana katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati zilizohusika katika sakata la Makinikia jana Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger