
Jonas Kamaleki – MAELEZO
Ajali za barabarani zimepungua
kwa asilimia 40 katika kipindi cha Julai- Septemba 2017 ikilinganishwa
na kipindi hicho hicho mwaka jana.
Hayo yameelezwa leo katika
mahojiano maalum kati Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Deus Sokoni na Idara ya Habari (MAELEZO).
Sokoni amesema katika kipindi cha
Julai – Septemba mwaka 2016 ajali za barabarani zilikuwa 2639 wakati
mwaka huu katika kipindi hicho hicho jumla ya ajali 1375 zimetokea
nchini.
Kwa mujibu wa Kamanda Sokoni,
idadi ya vifo pia imepungua kutoka 923 hadi 652 na ajali za pikipiki
zimepungua kutoka 653 hadi 367 ambayo ni sawa na asilimia 44.
“Kupungua kwa ajali hizo na vifo
imetokana na madereva kutii sheria bila shuruti, ushirikiano baina ya
wananchi na jeshi la polisi na elimu kwa umma ambayo tumekuwatukiitoa
kwa wadau mbalimbali, ikiwemo wanafunzi, vituo vya bodaboda na kambi za
jeshi la wananchi,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni amesema makosa
yanayotokana na ulevi yameongezeka kutoka 7589 hadi 7617 jambo ambalo
limeelezwa kuwa elimu bado inahitajika ili kupunguza changamoto hiyo.
Majeruhi wa ajali za barabarani
wamepungua kutoka 570 hadi 284 ambayo ni sawa na takriban asilimia 50
jambo ambalo linaonyesha mabadiliko makubwa katika kuzingatia sheria za
usalama barabarani.
Sokoni aliongeza kuwa elimu
inayotolewa kwa waendesha pikipiki imesaidia kupunguza ajali na vifo vya
waendesha pikipiki na abiria kiasi kwamba kwa mwaka 2016 katika kipindi
husika vifo vilikuwa 246 na kwa mwaka huu ni 182.
Kupungua kwa ajali, majeruhi na
vifo kumetokana na Mkakati wa Kitaifa chini ya Kikosi cha Usalama
Barabarani wa kupunguza ajali za barabarani zinasosababisha majeruhi na
vifo.
Kamanda Sokoni amewataka
madereva, watembea kwa miguu, abiria na wadau wote wa usafiri kuzingatia
sheria kanununi na taratibu za usalama barabarani.
Katika kutekeleza Mkakati huo
zimefanyika operesheni za usalama barabarani katika mikoa ya Njombe,
Tanga, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Katika operesheni hizo
madereva 64 wamefungiwa leseni, wengi wao wakiwa madereva wa mabasi ya
abiria ambapo madereva 14 wamefungwa jela.
Usalama barabarani ni jukumu la
kila mtu, kwani watanzania karibu wote ni watumia barabara, hivyo kila
mmoja inabidi awe mwangalifu katika sula hilo.
Ikumbukwe Kauli Mbiu ya Wiki ya
Nenda kwa Usalama Barabarani ya mwaka huu ilisema Zuia ajali, Tii
Sheria, Okoa Maisha. Hivyo, madereva na waenda kwa miguu pamoja na
abiria inabidi watii sheria bila shuruti ili kuzuia ajali na kuokoa
maisha.
SHARE








No comments:
Post a Comment