
Mbunge wa jimbo la
Chalinze ,Ridhiwani Kikwete akizungumza jambo na madiwani na watendaji
wa halmashauri ya Chalinze katika kikao cha baraza la madiwani(picha na
Mwamvua Mwinyi)

Baadhi ya madiwani
na watendaji wa halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza Mbunge wa jimbo
hilo ,Ridhiwani Kikwete hayupo pichani(picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete,amekerwa kwa kusuasua kwa utekelezaji wa
miradi ya maendeleo katika halmashauri ya Chalinze licha ya kuwa ya tatu
nchini kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani.
Kutokana na hilo
amewataka wataalamu na watendaji wa halmashauri ya Chalinze kuacha
visababu vinavyokwamisha kumaliza viporo vya miradi ya maendeleo
vilivyopo tangu mwaka wa fedha 2016/2017.
Aidha ameeleza
,halmashauri hiyo inakusanya zaidi ya milioni 300 kwa mwezi ambapo kwa
miezi mitatu inafikia milioni 900 hadi bilioni moja lakini utekelezaji
wa miradi umekua haukidhi mahitaji.
Pamoja na hilo
,Ridhiwani ameutaka wakala wa barabara Vijijini na Mjini (TARURA)
kuhakikisha wanashirikiana na madiwani wa kata ili waweze kupewa
vipaombele vya mahitaji halisi ya barabara zinazohitajika kwasasa.
Akitoa rai hiyo ,wakati
wa baraza la madiwani la kawaida la halmashauri hiyo,alieleza hiyo ni
halmashauri moja wapo kati ya zinazofanya vizuri kimkoa na kitaifa
lakini haifikii malengo yanayotakiwa.
Ridhiwani alisema
atakuwa mkali kwa hilo na hatosita kulikemea hadi hapo halmashauri
itakaposimama kushirikiana na matakwa ya madiwani kwa maslahi ya
wananchi.
Alielezea hofu yake
ikifikia 2020 watashindwa kuisemea ilani kwa kudorora kwa miradi
kutokana na kupelekwa fedha chache kwenye miradi hiyo wakati fedha zipo.
Ridhiwani alisema kila
eneo la mradi kwenye kabrasha limewekwa deshi ama bado ,na kudai kwa
mwendo huo ni kuididimiza halmashauri.
Alieleza ifikie wakati wa kusimamia mapato ya ndani na miradi ya mendeleo kwa maslahi mapana ya wananchi na sio vinginevyo .
“Ikifikia hatua ya
kuanza kusigana kutokana na matumizi ya fedha humu ndani kutakuwa
hakukaliki ,ni wakati wa kufanya yale yenye tija kwa watanzania tuache
mchezo kwenye fedha hizi”
“Kama fedha inapangwa
kwenda kutekelezwa miradi kwanini isifanye kazi husika ,kwanini kila
mradi haujamalizwa ” haya masuala tuayaache haiwezekani kwenye kabrasha
kila sehemu ya mradi ni deshi ,deshi jamani hatutafika kwa dizaini hii
“alisema Ridhiwani.
Akizungumzia suala la
TARURA alisema,ni changamoto kwani wamekuwa wakienda kujenga barabara
kwenye kata mbalimbali bila kuwashirikisha madiwani wala wananchi.
Ridhiwani alisema zipo
barabara zenye mahitaji makubwa kwa sasa zinazotakiwa kuboreshwa na
kujengwa ili kuondoa kero kwa wananchi .
Alieleza ni lazima TARURA wafuate mahitaji na vipaombele vinavyotakiwa kuliko kujiamulia vipaombele vyao visivyokidhi malengo.
“Tofauti na ambavyo
tulitegemea tunashauri ikiwezekana tukutane na huyu mtendaji mkuu wa
TARURA Mkoa wa Pwani kama Taifa tuzungumze nae kuhusu barabara zetu za
Chalinze na tujadiliane nini kifanyike” alisema Ridhiwani.
Alisema wamekua
wakipanga miradi ya barabara ambayo inahitaji kutekelezwa lakini
utekelezaji wake umekua ukisuasua changamoto ikiwa ni ushirikishwaji
mdogo kati ya ya TARURA, Halmashauri na baraza la madiwani.
Nae diwani wa kata ya
Kibindu ,Suleimani Mkufya alisema katika kata yake barabara yenye urefu
wa kilomita 12 TARURA wamejenga kilomita tano .
Walipohojiwa walidai kuwa fedha waliyopewa ni ya kilometa tatu na kilomita mbili wameongeza wenyewe.
Kauli hiyo ilizua utata
kwa madiwani kwani wanashindwa kuelewa kwanini barabara hazikamiliki
kwa wakati na pia utaratibu wa TARURA kuongeza kilometa zake fedha hizo
wanazitoa kwenye mfuko upi.
Diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi alisema kilio chake
kipo katika fedha za makusanyo ambapo zinapangiwa matumizi ambayo
hayatekelezwi kwa wakati.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa halmashauri hiyo Said Zikatimu alisema kiasi cha
sh.milioni 225 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya barabara kwa mwaka wa
fedha 2016/2017 na tayari baadhi ya miradi inaendelea kutekelezwa.
Kuhusu kusuasua kwa miradi alisema watahakikisha wanasimamia fedha zinazotengwa kwenda kwa wananchi zinaleta matokeo chanya.
SHARE








No comments:
Post a Comment