TRA

TRA

Sunday, January 21, 2018

‘Kugundua saratani mapema ni njia bora zaidi ya kuitibu’

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


 

Mwandishi wetu, TJNCDF

TAFITI mbalimbali za hapa nchini zinaonyesha kuwa watu wengi wanaougua saratani huwa hawajifahamu hadi hali zao zinapokuwa mbaya.

Taarifa ya Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) inaeleza wagonjwa wengi hufikishwa katika hospitali hiyo wakiwa katika hali mbaya na wengine huwa ni vigumu kupona.

Wanaeleza ya kuwa ni ukweli kwamba saratani nyingi zinaweza kutibiwa kirahisi iwapo mgonjwa atawahi kupata matibabu.

Hii ndiyo kusema elimu ya ugonjwa huo ni ya msingi sana katika kuwafanya watu wawahi hospitali mapema wanapoona dalili za saratani.



Kulingana na wataalamu wa afya, saratani ni ugonjwa unaosababishwa na seli za eneo fulani la mwili kubadili tabia na kuzaliana kwa kasi bila mpangilio na kuathiri utendaji wa mwili.

Zipo saratani za aina nyingi na kila moja ina dalili zake. Mfano ni saratani ya koo, ubongo, damu, kibofu cha mkojo, shingo ya kizazi, matiti na ngozi.

Takwimu za ORCI zinaonesha kuwa wastani wa watu 30-35 kwa kila 100,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na saratani ya mfumo wa chakula, koo na ini.

Saratani si kwamba huwapata watu wazima pekee, bali hata watoto, na katika nchi nyingi saratani ni chanzo kikubwa cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri kati ya miaka mitano na 14.

Takribani asilimia 50 ya watu wanaopata saratani katika nchi zinazoendelea ni wale wenye umri chini ya miaka 65.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani inaeleza kuwa asilimia 30 ya vifo vyote vitokanavyo na saratani husababishwa na mambo matano.

Mambo hayo yanatajwa kuwa ni unene wa kupindukia, ulaji usiofaa hasa kutokupata matunda na mboga kwa wingi, kutokufanya mazoezi, utumiaji wa tumbaku na unywaji wa pombe.
Mambo mengine yanayochangia ongezeko la saratani hasa katika nchi zinazoendelea ni pamoja na matumizi ya vifaa vinavyotoa mionzi mikali na sumu ya ‘aflatoxin’ inayopatikana katika nafaka zilizovunda wakati wa kuhifadhiwa.

Mambo mengine yanayosababisha saratani ni uchafuzi wa mazingira ya hewa kwa moshi wa tumbaku na wa mabaki ya plastiki.

Vile vile vitu vingine vinavyochochea saratani ni maambukizi ya magonjwa kama vile Virusi Vya Ukimwi (VVU), virusi vya homa ya ini, virusi vinavyosababisha asilimia 90 au zaidi ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) na virusi vya Epstein Barr vinavyosababisha saratani ya uvumbe wa taya kwa watoto.

Utafiti wa Dk Catherine de Martel na wenzake uliochapishwa mwaka 2012 katika jarida la The Lancet Oncology, unaonyesha kuwa katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 32.7 ya saratani zote hutokana na maambukizi ya vimelea vya magonjwa.

Vimelea vingine ni Helicobacter pylori wanaosababisha vidonda vya tumbo na wadudu wa kichocho wanaosababisha saratani ya kibofu cha mkojo.
Kwa wanaume saratani zinazoongoza ni ya mapafu, saratani ya ngozi (Kaposi’s sarcoma), saratani ya tezi dume na saratani ya tumbo la chakula.

Kwa upande wa wanawake saratani zinazoongoza ni za mlango wa kizazi, ikifuatiwa na ya matiti na ya utumbo.

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania, Nsachris Mwamaja anaelezea juu ya gharama za matibabu ya saratani:

“Pale Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), wagonjwa wanaotibiwa bure ni wengi na tiba yao inagharimu fedha nyingi. Kwa mfano mgonjwa mmoja wa saratani huweza kutibiwa kwa Sh. milioni 2. Ndiyo maana kuna changamoto kubwa katika swala hili.”

Wachunguzi wengine wa masuala ya tiba wanasema kuwa, kuna dawa nyingine za saratani ya damu inayowapata watoto zinazogharimu Sh milioni moja mfano dawa aina ya Asparaginase.

Wataalamu wa afya wanashauri jamii kuchunguza saratani mara kwa mara ili kuepuka gharama kubwa za matibabu. Ikigundulika ikiwa katika hatua za mwanzo inatibika kirahisi. Saratani ikikomaa inakuwa ni vigumu kuitibu na huchukua muda mrefu kuikabili.

Uchunguzi unaonyesha kuwa familia masikini zinaathirika zaidi na kuongeza ufukara pale mmoja wa wanafamilia anapokuwa anagua magonjwa sugu ya saratani.

Nguvu kubwa ya familia huwekezwa kujaribu kuokoa maisha ya mgonjwa hivyo raslimali nyingi kupotea na wakati huo kukwama baadhi ya shughuli za kipato.

Kugundua saratani mapema ni njia bora zaidi ya kuitibu kuliko kuiacha hadi inaathiri mwili kwa kiwango kikubwa na kusababisha kuwa kwenye usugu hivyo kuhatarisha maisha.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maswali, maoni na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam au tjncdf@gmail.com

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger