Afisa Muelimishaji Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka akiwaelimisha Wafanyakazi wa
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi na
Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017/18 katika ukumbi wa mikutano
wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chama Siriwa
akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi ya Majengo, katika ukumbi wa
mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Valentine Baltazar
akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Taratibu za Kiforodha, katika ukumbi
wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018. (PICHA ZOTE NA BENEDICT
LIWENGA-TRA)
Na: Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wadau mbalimbali
wakiwemo wafanyakazi wa ofisi za Serikali na Asasi za Kiraia kwa ajili
ya kuongeza ufahamu na kuwa mabalozi wa masuala yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mafunzo ya elimu ya kodi kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara (TANTRADE) yaliyofanyika ofisini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa
mamlaka hiyo Bw. Edwin Rutageruka amesema TRA inastahili kupongezwa kwa
kazi inayoifanya ambayo imepelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
"Ni dhahiri kwamba, sasa hivi
TRA inafanya kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato na kutoa elimu ya kodi
kwa vikundi na taasisi mbalimbali, hivyo, fursa hii tuliyoipata tuitumie
vizuri ili kuongeza uelewa wa kutosha kuhusu kodi ili tuwe mabalozi
wazuri kwa wengine", amesema Rutageruka.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa
Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania Bi. Rose
Mahendeka, akiwasilisha mada ya Kodi na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya
mwaka 2017 amesema, kila mwananchi anajukumu la kudai risiti kila
anaponunua bidhaa na kila mfanyabiashara anatakiwa kutoa risti kila
anapofanya mauzo.
"Suala la kulipa kodi lipo kwa
mujibu wa sheria hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kudai risiti wakati
wote anaponunua bidhaa na vivyo hivyo kwa upande wa wafanyabiashara
wanapaswa kutoa risiti kila wanapofanya mauzo", amesisitiza Mahendeka.
Muelimishaji mwingine kutoka
TRA aliyewasilisha mada kuhusu Kodi ya Majengo Bw. Chama Siriwa
amewahimiza wafanyakazi hao wa TANTRADE kuwahi kulipa kodi ya majengo ya
mwaka huu wa fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na
msongamano wa watu ambao mara nyingi hujitokeza kulipa mwishoni.
"Watu wengi wana tabia ya
kusubiri tarehe za mwisho kulipia kodi ya majengo suala ambalo
linasababisha msongamano usio wa lazima na hivyo kuchelewa kupata huduma
kwa wakati", amefafanua Bw. Siriwa.
Siriwa ameongeza kuwa, Kodi ya
Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai Mosi ya mwaka wa fedha husika hadi
Juni 30 ya mwaka unaofuatia na kusisitiza kuwa muda huu ni muafaka
kabisa wa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe
30 Juni, 2018.
Mamlaka ya Mapato Tanzania,
katika kipindi cha miezi 6 iliyopita imefanya jumla ya semina 137 kwa
wafanyakazi wa Serikali, Asasi za Kiraia, wafanyabiashara na vikundi
mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na kuongeza uhiari katika ulipaji wa
kodi.
SHARE
No comments:
Post a Comment