Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita na Mahakama ya Wilaya Geita likiwa katika hatua za awali za ujenzi
Jengo
la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe likiwa katika hatua za awali za ujenzi
wake katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe
Jengo
la Mahakama ya wilaya ya Chato likiwa katika hatua ya Msingi. Majengo
haya yote yanajengwa kwa Teknolojia ya Gharama nafuu na ya muda mfupi
iitwayo Moladi na yanajengwa na Kampuni ya Moladi Tanzania. Ujenzi wake
unatarajiwa kutumia muda wa miezi sita.
……………………
Na Lydia Churi-Geita
Katika
kutekeleza dhamira yake ya kuboresha huduma za Mahakama na kusogeza
huduma hizo karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania kwa
kushirikiana na Benki ya Dunia imeanza rasmi ujenzi wa majengo matatu ya
Mahakama katika mkoa wa Geita pamoja na wilaya zake za Bukombe na
Chato.
Ujenzi
wa Mahakama hizi ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano
(2015/16 hadi 2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa
Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka
2015. Miradi hii kwa pamoja inalenga kuboresha huduma na kusogeza huduma
karibu zaidi na wananchi.
Mahakama
imeanza ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Geita ambalo
litajumuisha pia na Mahakama ya wilaya ya Geita. Majengo mengine
yanayojengwa ni ya Mahakama za wilaya za Bukombe na Chato.
Majengo
haya yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita kutoka sasa
na yanajengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na gharama nafuu na ya
muda mfupi iitwayo Moladi ambapo kampuni ya Moladi Tanzania ndiyo
imepewa dhamana ya kujenga majengo hayo. Jumla ya majengo ya Mahakama za
Mkoa, wilaya na Mwanzo sita tayari yameshajengwa kwa kutumia teknolojia
ya Moladi katika jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.
Majengo
haya ni yale ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya
Wilaya ya Kibaha, Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga
pamoja na jengo la Mahakama ya wilaya ya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo
Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kawe jijini Dar es salaam.
Mhandisi
wa Kampuni ya Moladi Tanzania anayesimamia ujenzi wa Mahakama za Geita,
Bukombe na Chato, Camilius Mihambo akielezea ujenzi wa Mahakama hizo
alisema ujenzi huo unaendelea vizuri na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika
katika kipindi cha miezi sita kilichopangwa . Mhandisi Mihambo amesema
hatua ya ujenzi iliyofikiwa sasa ni hatua ya awali ya kujenga msingi
katika majengo yote matatu.
“Kazi
kubwa na inayochukua muda mrefu kwa sasa ni ya kujenga msingi, hatua
inayofuata ya kuweka ukuta ni ya muda mfupi kwa kuwa tunatumia
teknolojia ya Moladi ambayo kuta zinaweza kusimama ndani ya siku tatu na
kuendelea, alisema Mhandisi huyo.
Akizungumzia
hatua ya Mahakama ya Tanzania kuanza ujenzi katika Mkoa wa Geita,
Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Geita, Lothan Simkoko anaelezea
kufurahishwa kwake kwa uamuzi wa Mahakama kujenga Majengo ya Mahakama za
wilaya na Mkoa katika mkoa wa Geita. Anasema ujenzi huo utasaidia
upatikanaji wa haki kwa wakati kwa wananchi wanaofika Mahakamani
kutafuta haki zao pia kumaliza changamoto ya ufinyu wa ofisi. Alisema,
jengo la Mahakama ya Mkoa litakapomalizika litatoa nafasi zaidi na
kuboresha huduma. Mahakama ya Mkoa wa Geita ina upungufu wa chumba cha
Mahabusu, chumba cha kuhifadhi ushahidi pamoja na ofisi kwa ajili ya
watumishi wake.
Mtendaji
huyo alisema Mahakama Mkoani Geita haina jengo la Mahakama ya wilaya na
badala yake jengo linalotumika sasa kwa Mahakama ya wilaya na Mwanzo ni
la kuazima na pia haliko katika hali nzuri. Alisema kukamilika kwa
jingo jipya la Mahakama mkoani humo kutasaidia kwa kiasi kikubwa
kuboresha huduma za Mahakama.
Hata
hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa juu ya ujenzi wa Mahakama hizo
walionyesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Mahakama kujenga majengo yake
mapya. Bwana Mika Jonathan Shija ambaye ni Mkazi wa Geita anaelezea
kufurahishwa kwake na ujenzi wa Mahakama ya Mkoa na ya Wilaya ya Geita
na kusema kuwa ujenzi huo utakapokamilika utawarahisishia wananchi
kupata huduma. “kama tulivyoambiwa kuwa Mahakama ya Mkoa na wilaya
zitakuwa kwenye jengo moja hivyo kwetu sisi ni rahisi kwa kuwa itakuwa
ni rahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine”, alisema.
Naye
Pili Malongo Mkazi wa Bukombe yeye alisema amefurahishwa na ujenzi wa
Mahakama wilayani humo kwa kuwa anaamini jengo jipya la Mahakama
litakuwa na sehemu iliyotengwa kwa ajili ya wananchi kupumzika wakati
wakisubiri kupatiwa huduma mahakamani hapo.
Pamoja
na ujenzi wa Mahakama hizo tatu katika Mkoa wa Geita, Mahakama ya
Tanzania tayari imeanza kutekeleza program ya ujenzi wa majengo 18 ya
Mahakama katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 anabainisha Mkuu wa
Kitengo cha Majengo (Estate Management) wa Mahakama ya Tanzania Mhandisi
Khamadu Kitunzi.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Kitunzi, kati ya majengo 18 yaliyoanza kujengwa
nchini, majengo mawili ni ya Mahakama Kuu yanayojengwa kwenye Mikoa ya
Mara na Kigoma, matano ni ya Mahakama za Hakimu Mkazi yanayojengwa
katika mikoa ya Geita, Njombe, Lindi, Simiyu, na Katavi. Aidha jumla ya
majengo 11 ya Mahakama za Wilaya yanajengwa katika wilaya za Kasulu,
Rungwe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Kilindi, Sikonge, Kondoa, Bunda na
Longido.
Aidha,
Mahakama pia imefanikiwa kujenga Mahakama za Mwanzo na pia kumalizia
baadhi ya Mahakama zilizoanza kujengwa kwa nguvu ya wananchi katika
maeneo mbalimbali nchini kama vile Itinje-Meatu, Robanda-Serengeti,
Wasso-Loliondo, na Karatu Arusha. Maeneo mengine ni Beleko-Kondoa,
Mahakama ya Old Korogwe-Korogwe, Mvomero Morogoro, Mahakama ya Mwanzo
Totoe iliyopo Mkoani Songwe na Mahakama ya Mwanzo Iguguno mkoani
Singida.
Akifafanua
zaidi kuhusu ujenzi wa majengo ya Mahakama, Mhandisi Kitunzi anaeleza
kuwa hivi sasa zipo Mahakama Kuu 14 na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa
Mahakama kuu katika mikoa ya Mara na Kigoma kutakuwa na jumla ya
Mahakama kuu 16 nchini na kubaki na uhitaji wa Mahakama Kuu 10 katika
mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Mahakama ya Tanzania inalenga kujenga
majengo ya Mahakama kuu ambayo yatatumika kama Kituo Jumuishi cha kutoa
huduma za kimahakama yaani Intergrated Justice Centre. Mahakama
tayari ilifanya ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya
Mbeya ambapo hivi sasa Mahakama hiyo inafanya kazi kama kituo Jumuishi
cha huduma za Kimahakama.
Mhandishi
Kitunzi anasema Mahakama inao mpango wa kujenga Majengo ya Mahakama Kuu
ambayo yatatoa huduma kama kituo Jumuishi cha kutoa Huduma za
Kimahakama kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika mikoa ya Dar es
salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Mwanza na Arusha.
SHARE
No comments:
Post a Comment