Asa Mwaipopo
Kampuni ya madini ya Acacia imemtangaza aliyekuwa meneja mkuu wa uendelevu, Asa Mwaipopo kuwa mkurugenzi mtendaji wake Tanzania.
Taarifa ya uteuzi huo imeambatana na
ripoti ya matokeo ya hesabu za fedha kwa miezi 12 ilioishia Desemba 2017
iliyotolewa na ofisa mtendaji mkuu, Peter Geleta.
Katika ripoti hiyo iliyotolewa jana,
Geleta alisema anaamini zuio la kusafirisha mchanga wa dhahabu
(makinikia) huenda likaondolewa mwaka huu kutokana na mazungumzo
yanayoendelea baina ya Barrick na Serikali ya Tanzania.
Uteuzi wa Mwaipopo ni mkakati wa kampuni
hiyo wa kuhakikisha miradi yote nchini inaendeshwa na wafanyakazi wa
ndani badala ya wageni ulioanza kutekelezwa miaka minne iliyopita.
Hadi sasa kampuni hiyo imeripoti kuwa
idadi ya wafanyakazi wa kigeni imepungua kutoka asilimia 15 miaka minne
iliyopita hadi nne mwaka jana.
Kwa mujibu wa hesabu za kampuni hiyo za
mwaka 2017, biashara iligubikwa na changamoto nyingi zilizosababisha
ishindwe kutoa gawio kwa wanahisa wake.
“Mwaka ulioisha, akiba ya fedha katika
kampuni ilishuka kutoka Sh700 bilioni hadi Sh180 bilioni, upungufu wa
Sh520 bilioni kwa mwaka ukijumuisha ongezeko la kodi ya thamani.
Kutokana na haya, bodi ya wakurugenzi imeamua kutotoa gawio la faida la
mwisho wa mwaka kwa wanahisa,” alisema Geleta.
“Tunaendelea kutathmini hatua za kulinda
mzunguko wa fedha pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni,
uchimbaji wa upanuzi huko North Mara, utafiti wa machimbo mapya na
kulinda thamani ya dhahabu dhidi ya kushuka kwa bei kwenye masoko ya
kimataifa.”
Alisema kwa kuzingatia viwango
vinavyotumika vya kihasibu, wamerudia hesabu ya thamani ya mali zao kwa
kulinganisha na vipengele vichache vya mpango uliyotangazwa na Barrick
na Serikali ya Tanzania wakati wa makubaliano yao, matokeo yameonyesha
kupungua kwa thamani ya mali zao zote.
“Athari kubwa ipo katika mgodi wetu wa
Bulyanhulu, kutokana na hatua ya kupunguza uzalishaji na uhai wa mgodi
wenyewe. Upungufu huu umepelekea thamani ya sasa ya mgodi kutoka Dola za
Kimarekani 1.2 bilioni hadi Dola za Kimarekani 600 milioni, Pia tumeona
nyongeza ya matumizi ya Dola za kimarekani 12 milioni (Sh25 milioni)
kwa mradi wa Nyanzaga ikiakisi athari za sheria mpya za madini za
thamani ya sasa ya mradi, Mporomoko huu wa thamani ya mali zetu hauna
athari katika mapato yetu,” alisema Geleta.
Hata hivyo, Acacia ilisema bado
inasubiri matokeo ya mazungumzo na mapendekezo yaliyofikwa kati ya
Barrick na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mapitio kabla ya
kutekelezwa.
Alisema kampuni hiyo imeendelea kuwa na
nidhamu kwenye matumizi na kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha biashara
yao inaendelea kukua.
Matarajio ni kwamba Barrick inategemea
kuwasilisha mapendekezo ya mazungumzo yake na serikali ya Tanzania
kwenye kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018.
“Tunaendelea kutathmini hatua zaidi za
kulinda mzunguko wa fedha pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa
kampuni, uchimbaji wa upanuzi huko North Mara, utafiti wa machimbo mapya
pamoja na kulinda thamani ya dhahabu dhidi ya kushuka kwa bei kwenye
masoko ya kimataifa,” alisema Geleta.
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi
SHARE
No comments:
Post a Comment