Imeelezwa kuwa watu wengi wanaendelea
kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutokana na kuanza
mahusiano ya kimapenzi bila kutambua afya zao hali inayosababisha waanze
kuishi kama mume na mke bila kujua hali zao za kiafya.
Hayo yamesemwa Februari 14,2018 na wahudumu wa jamii wanaosaidia
kazi katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na Maambukizi
ya VVU vilivyopo katika halmashauri 7 za wilaya mkoani Mwanza
yanayofanyika katika ukumbi wa hotel ya Midland jijini Mwanza.
Wahudumu hao wapo katika mafunzo ya msaada na huduma za kisaikolojia
yanayotolewa na Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare
Initiative (AGPAHI) kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Centres for
Disease Control (CDC).
Wahudumu walisema kitendo cha kuanza mahusiano ya kimapenzi na kuoana
bila kutambua afya ni miongoni mwa tabia hatarishi zinazochangia kwa
kiasi kikubwa kuambukizana VVU.
Mmoja wa washiriki hao Chausiku Sitta kutoka halmashauri ya wilaya ya
Kwimba alieleza kuwa vijana wanapata maambukizi ya VVU kutokana na
kukosa elimu sahihi juu ya VVU na Ukimwi na wengi wao kutawaliwa na
tamaa ya ngono isiyo salama na kudhani kuwa kila mtu anayeonekana kuwa
na umbo zuri basi hana maambukizi ya VVU.
“Vijana wanakurupuka tu,tena wakiona mwanaume ana mvuto ama mwanamke
ana makalio makubwa wao wanaita ‘wowowo’ wanachanganyikiwa kabisa,ndugu
zangu huwezi kumtambua mtu mwenye maambukizi ya VVU kwa kumwangalia kwa
macho mpaka apimwe”,aliongeza Chausiku.
Naye Musa Ordas kutoka halmashauri ya wilaya ya Buchosa aliitaka jamii
kutoendekeza waganga wa jadi kwani baadhi yao wanawadanganya watu
wanaoishi na VVU kuwa wamerogwa kwa kuwalaghai kuwa wametupiwa majini
mahaba.
Kwa upande wake, Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa
aliwataka wanaume kuacha tabia ya kutumia majibu ya wake zao wanapopima
VVU kwani majibu yanatofautiana na hutokea wakati mwingine mmoja kati
yao kuwa na maambukizi na mwingine kutokuwa nayo.
Dk. Musagasa aliwashauri akina mama kupima afya zao kabla ya kubeba
ujauzito,na kujifungulia katika vituo vya afya ili kuzuia maambukizi ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Siyo watoto wote wanaozaliwa na mama mwenye maambukizi ya VVU wana
VVU,hivyo mama unapotaka kubeba mimba pima kwanza afya yako,ukibainika
una maambukizi utashauriwa na wataalamu wa afya namna ya kufanya ili
usimwambukize mtoto wako”,alieleza Dk. Musagasa.
ANGALIA PICHA WAKATI WA MAFUNZO KUHUSU MSAADA NA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WAHUDUMU WA JAMII SIKU YA TATU
Mwezeshaji katika mafunzo ya msaada na huduma za kisaikolojia, Dk.
Joseph Musagasa akielezea umuhimu wa kupima afya kabla ya kuanzisha
mahusiano ya kimapenzi au kuingia katika ndoa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Dk. Musagasa akizungumza wakati wa mafunzo hayo. Aliwataka watu
wanaoishi na maambukizi ya VVU kuzingatia matumizi sahihi ya dawa
zinazofubaza makali ya VVU pamoja na kuzingatia lishe bora.
Chausiku Sita kutoka kituo cha afya na matunzo cha hospitali ya Ngudu
halmashauri ya wilaya ya Kwimba akielezea namna vijana wanavyopata
maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu VVU na Ukimwi.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa muwazi unapobainika kuwa una maambukizi ya
VVU.
Musa Ordas kutoka kituo cha afya Nyehunge kilichopo katika halmashauri
ya wilaya ya Buchosa akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo.
Mhudumu wa afya kituo cha afya Sengabuye iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela, Bahati Balekele Boyi.
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia
Yona akielezea faida za kuzingatia lishe bora kwamba inasaidia kuwa na
afya njema.
Cecilia Yona akielezea kuhusu madhara ya kutozingatia lishe bora.
Washiriki wakijifunza kwa njia ya picha (video)
PICHA ZA MATUKIO KWENYE MAFUNZO SIKU YA PILI
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gaston Kakungu ambaye ni Afisa Muuguzi
Mstaafu akitoa mada kuhusu umuhimu wa kuwa muwazi unapopata maambukizi
ya VVU.
Kakungu akiendelea na mada ya uwazi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya kazi za makundi.
Mshiriki wa mafunzo hayo Shija Mashimba kutoka kituo cha tiba na matunzo
cha hospitali ya Rufaa ya Bugando akiwasilisha kazi ya kundi lake
kuhusu tabia hatarishi zinazochangia kuwepo kwa maambukizi ya VVU,mfano
kudanganywa na waganga wa kienyeji kwa kupewa dawa za kuongeza nyota
zao.
Mhudumu ngazi ya jamii, Winfrida Meshack kutoka hospitali ya Sekouture
akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu tabia hatarishi zinasobabisha
maambukizi ya VVU kama vile ngoma za usiku ambazo zinawakutanisha
wanaume na wanawake.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
SHARE
No comments:
Post a Comment