Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi
katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mwikongi Kigosi (kushoto)
akiwasilisha taarifa ya ya maendeleo ya Elimu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dokta Binilith Mahenge wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa katika
Manispaa ya Dodoma hivi karibuni.
………………..
Na Ramadhani Juma
Ofisi ya Mkurugenzi
HALMASHAURI ya Manispaa ya
Dodoma imeweka mkakati kabambe utakaowezesha kufikia lengo la ufaulu wa
asilimia 100 kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi kuanzia mwaka 2018.
Hayo yamebainishwa katika taarifa
ya Manispaa hiyo iliyowasilishwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi
Manispaa ya Dodoma Mwikongi Kigosi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta
Binilith Mahenge alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Elimu na Afya
hivi karibu katika Manispaa hiyo.
Kwa kujibu wa taarifa hiyo,
miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kuhakikisha
wanafunzi wote wanamudu stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu
katika madarasa ya chini kabla ya kujiunga na madarasa yanayofuata.
Kigosi alisema mkakati mwingine ni
kusimamia mahudhurio ya Walimu na Wanafunzi pamoja na kudhibiti
matumizi ya simu kwa Walimu wawapo darasani.
Aidha, alisema Idara ya Elimu
Msingi itateua shule 25 za serikali ambazo zitashindanishwa na shule za
binafsi ili kubadilishana uzoefu na kuinua ufaulu katika Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma.
Vilevile alisema Idara imejipanga
kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji na kusimamia utendaji kazi wa
walimu, sambamba na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya
vizuri.
“Pia tutakuwa na mitihani, mazoezi
na majaribio ya kufikirisha, pamoja na kambi za masomo… haya yote
tutayafanya na tunaamini yatatupa matokeo tunayotarajia” alisema Kigosi.
Kwa mwaka 2017 jumla ya Wanafunzi
9,509 wakiwemo Wavulana 4,500 na Wasichana 5,009 walifanya mtihani wa
kuhitimu Elimu ya Msingi katika Manispaa ya Dodoma ambapo Wanafunzi
6,488 wakiwemo Wavulana 3034 na Wasichana 3454 walifaulu, sawa na
asilimia 68.
SHARE
No comments:
Post a Comment